2 Wafalme 25:22-30
2 Wafalme 25:22-30 NENO
Nebukadneza mfalme wa Babeli akamteua Gedalia mwana wa Ahikamu, mwana wa Shafani, awe msimamizi wa watu aliowaacha Yuda. Maafisa wote wa jeshi na watu wao waliposikia kwamba mfalme wa Babeli amemteua Gedalia kuwa mtawala, wakamjia Gedalia huko Mispa. Hawa walikuwa Ishmaeli mwana wa Nethania, Yohanani mwana wa Karea, Seraya mwana wa Tanhumethi Mnetofathi, na Yezania mwana wa Mmaaka, pamoja na watu wao. Gedalia akaapa ili kuwatia moyo wao na watu wao. Akasema, “Msiwaogope maafisa wa Wakaldayo. Kaeni katika nchi na kumtumikia mfalme wa Babeli, na itakuwa vyema kwenu.” Hata hivyo, katika mwezi wa saba Ishmaeli mwana wa Nethania mwana wa Elishama, aliyekuwa wa uzao wa mfalme, akaja pamoja na watu kumi, nao wakamuua Gedalia, na pia watu wa Yuda, pamoja na Wakaldayo waliokuwa naye huko Mispa. Baada ya haya, watu wote kuanzia aliye mdogo sana hadi aliye mkubwa kabisa, pamoja na maafisa wa jeshi, wakakimbilia Misri kwa kuwaogopa Wakaldayo. Katika mwaka wa thelathini na saba tangu Yehoyakini mfalme wa Yuda apelekwe uhamishoni, katika mwaka ule ambao Evil-Merodaki alifanyika mfalme wa Babeli, alimwacha huru Yehoyakini kutoka gerezani siku ya ishirini na saba ya mwezi wa kumi na mbili. Alizungumza naye kwa upole na kumpa kiti cha heshima kuliko wafalme wengine aliokuwa nao huko Babeli. Hivyo Yehoyakini akayavua mavazi yake ya gerezani, na siku zote za maisha yake zilizobaki alikula mezani mwa mfalme. Siku kwa siku mfalme alimpa Yehoyakini posho siku zote za maisha yake.