Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 22:1-13

2 Wafalme 22:1-13 NEN

Yosia alikuwa na miaka minane alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka thelathini na mmoja. Mama yake aliitwa Yedida binti Adaya, kutoka Boskathi. Akafanya yaliyo mema machoni pa BWANA na kuenenda katika njia zote za Daudi baba yake. Hakugeuka upande wa kuume wala wa kushoto. Katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wake, Mfalme Yosia akamtuma mwandishi Shafani mwana wa Azalia, mwana wa Meshulamu, kwenda katika Hekalu la BWANA. Akasema: “Panda uende kwa Hilkia, kuhani mkuu, umwambie ahesabu zile fedha ambazo zimeletwa katika Hekalu la BWANA, ambazo mabawabu wamekusanya kutoka kwa watu. Waambie waikabidhi kwa watu walioteuliwa kusimamia kazi ya Hekalu. Waamuru watu hawa wawalipe wafanyakazi ambao wanakarabati Hekalu la BWANA: wale maseremala, wajenzi na waashi. Waambie pia wanunue mbao na mawe yaliyochongwa ili kukarabati Hekalu. Lakini hawahitajiki kutoa hesabu ya fedha walizokabidhiwa, kwa sababu wanafanya kwa uaminifu.” Hilkia kuhani mkuu akamwambia Shafani mwandishi, “Nimekipata Kitabu cha Sheria ndani ya Hekalu la BWANA.” Akampa Shafani, ambaye alikisoma. Kisha Shafani mwandishi akamwendea mfalme na kumpa taarifa akisema: “Maafisa wako wametoa ile fedha ambayo ilikuwa ndani ya Hekalu la BWANA na imekabidhiwa mikononi mwa wasimamizi wa marekebisho ya Hekalu.” Ndipo Shafani mwandishi akampasha mfalme habari kwamba: “Hilkia kuhani amenipa kitabu hiki.” Naye Shafani akakisoma kile kitabu mbele ya mfalme. Mfalme aliposikia maneno ya kile Kitabu cha Sheria, akararua mavazi yake. Akatoa maagizo haya kwa Hilkia kuhani, Ahikamu mwana wa Shafani, Akbori mwana wa Mikaya, Shafani mwandishi, na Asaya mtumishi wa mfalme: “Nendeni mkamuulize BWANA kwa ajili yangu, na kwa ajili ya watu na Yuda wote kuhusu yale yaliyoandikwa ndani ya kitabu hiki ambacho kimepatikana. Hasira ya BWANA ni kubwa inayowaka dhidi yetu kwa sababu baba zetu hawakuyatii maneno ya kitabu hiki. Hawajatenda kulingana na yale yote yaliyoandikwa humo kutuhusu sisi.”

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na 2 Wafalme 22:1-13