Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wafalme 21

21
Manase mfalme wa Yuda
(2 Nyakati 33:1-20)
1Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na mbili alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka hamsini na tano. Mama yake aliitwa Hefsiba. 2Akafanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, akafuata desturi za machukizo za mataifa ambayo Mwenyezi Mungu aliyafukuza mbele ya Waisraeli. 3Akajenga upya mahali pa juu pa kuabudia ambapo Hezekia baba yake alikuwa amepabomoa. Pia akasimamisha madhabahu za Baali na kutengeneza nguzo ya Ashera, kama Ahabu mfalme wa Israeli alivyofanya. Akalisujudia jeshi lote la angani na kuliabudu. 4Akajenga madhabahu katika Hekalu la Mwenyezi Mungu, ambamo Mwenyezi Mungu alikuwa amesema, “Katika Yerusalemu nitaliweka Jina langu.” 5Katika nyua zote mbili za Hekalu la Mwenyezi Mungu, akajenga madhabahu kwa ajili ya jeshi lote la angani. 6Akamtoa kafara mwanawe katika moto, akafanya uchawi na uaguzi, na akataka shauri kwa wapiga ramli na kwa mizimu. Akafanya maovu mengi sana machoni mwa Mwenyezi Mungu na kumghadhibisha.
7Akachukua nguzo ya Ashera aliyoichonga na kuiweka katika Hekalu, ambalo Mwenyezi Mungu alikuwa amemwambia Daudi na mwanawe Sulemani, “Katika Hekalu hili na katika Yerusalemu, mji niliouchagua kutoka makabila yote ya Israeli, nitaliweka Jina langu milele. 8Sitaifanya tena miguu ya Waisraeli itangetange kutoka nchi niliyowapa baba zao, ikiwa watakuwa waangalifu kufanya kila kitu nilichowaamuru, na kuishika Torati yote ambayo walipewa na Musa mtumishi wangu.” 9Lakini hawa watu hawakusikiliza. Manase akawapotosha, kiasi kwamba walifanya maovu mengi kuliko mataifa ambayo Mwenyezi Mungu aliangamiza mbele ya Waisraeli.
10Mwenyezi Mungu akasema kupitia watumishi wake manabii: 11“Manase mfalme wa Yuda ametenda dhambi hizi za kuchukiza. Amefanya maovu mengi kuliko Waamori waliokuwa kabla yake, na ameiongoza Yuda katika dhambi kwa sanamu zake. 12Kwa hiyo hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: Nitaleta maafa makubwa juu ya Yerusalemu na Yuda, kiasi kwamba masikio ya kila mmoja atakayesikia habari zake yatawasha. 13Nitanyoosha juu ya Yerusalemu kamba ya kupimia iliyotumika dhidi ya Samaria, na timazi iliyotumika dhidi ya nyumba ya Ahabu. Nitaifutilia mbali Yerusalemu kama mtu afutavyo sahani, nikiifuta na kuifunikiza. 14Nitawakataa mabaki wa urithi wangu na kuwatia mikononi mwa adui zao. Watapokonywa mali yao na kutekwa nyara na adui zao wote, 15kwa sababu wametenda uovu machoni pangu na kunighadhibisha tangu siku baba zao walipotoka Misri hadi leo.”
16Zaidi ya hayo, Manase pia alimwaga damu nyingi isiyo na hatia, hivi kwamba aliijaza Yerusalemu kutoka mwanzo hadi mwisho, mbali na dhambi ambayo alikuwa amesababisha Yuda kufanya, na hivyo wakatenda maovu machoni pa Mwenyezi Mungu.
17Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Manase, na yote aliyoyafanya, pamoja na dhambi alizotenda, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? 18Manase akalala na baba zake, akazikwa katika bustani ya jumba lake la kifalme, katika bustani ya Uza. Naye Amoni mwanawe akawa mfalme baada yake.
Amoni mfalme wa Yuda
(2 Nyakati 33:21-25)
19Amoni alikuwa na umri wa miaka ishirini na mbili alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka miwili. Mamaye aliitwa Meshulemethi binti Haruzi, kutoka Yotba. 20Akatenda maovu machoni mwa Mwenyezi Mungu, kama baba yake Manase alivyofanya. 21Akaenenda katika njia zote za baba yake, akaabudu sanamu ambazo baba yake aliziabudu na kuzisujudia. 22Akamwacha Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zake, wala hakuenenda katika njia za Mwenyezi Mungu.
23Watumishi wa Amoni wakampangia njama, nao wakamuua ndani ya jumba lake la kifalme. 24Kisha watu wa nchi wakawaua wale wote waliokuwa wamepanga njama dhidi ya Mfalme Amoni. Wakamfanya Yosia mwanawe kuwa mfalme mahali pake.
25Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Amoni na yale aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? 26Akazikwa kwenye kaburi lake katika bustani ya Uza. Naye Yosia mwanawe akawa mfalme baada yake.

Iliyochaguliwa sasa

2 Wafalme 21: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia