Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wakorintho 11:25-33

2 Wakorintho 11:25-33 NENO

Mara tatu nilipigwa mijeledi, mara moja nilipigwa kwa mawe, mara tatu nilivunjikiwa na meli, nilikaa kilindini usiku kucha na mchana kutwa; nimekuwa katika safari za mara kwa mara. Nimekabiliwa na hatari za kwenye mito, hatari za wanyang’anyi, hatari kutoka kwa Wayahudi wenzangu, hatari kutoka kwa watu wa Mataifa; hatari mijini, hatari nyikani, hatari baharini; na hatari kutoka kwa ndugu wa uongo. Nimekuwa katika kazi ngumu na taabu, katika kukesha mara nyingi; nimejua kukaa njaa na kuona kiu; nimefunga kula chakula mara nyingi; nimehisi baridi na kuwa uchi. Zaidi ya hayo yote, nakabiliwa kila siku na mzigo wa wajibu wangu kwa makundi yote ya waumini. Je, ni nani aliye mdhaifu, nami nisijisikie mdhaifu? Je, nani aliyekwazwa, nami nisiudhike? Kama ni lazima nijisifu, basi nitajisifia yale mambo yanayoonesha udhaifu wangu. Mungu na Baba wa Bwana wetu Isa, yeye ambaye anahimidiwa milele, anajua ya kuwa mimi sisemi uongo. Huko Dameski, mtawala aliyekuwa chini ya Mfalme Areta aliulinda mji wa Dameski ili kunikamata. Lakini niliteremshwa kwa kapu kubwa kupitia dirisha ukutani, nikaokolewa kutoka mkononi mwake.