2 Wakorintho 11:16-24
2 Wakorintho 11:16-24 NENO
Nasema tena: mtu yeyote asidhani kwamba mimi ni mjinga. Lakini hata mkinidhania hivyo, basi nipokeeni kama mjinga ili nipate kujisifu kidogo. Ninayosema kuhusiana na huku kujisifu kwa kujiamini, sisemi vile Bwana Isa angesema, bali kama mjinga. Kwa kuwa wengi wanajisifu kama vile ulimwengu ufanyavyo, mimi nami nitajisifu. Ninyi mwachukuliana na wajinga kwa sababu mna hekima sana! Kweli ni kwamba mnachukuliana na mtu akiwatia utumwani au akiwatumia kwa ajili ya kupata faida, au akiwanyang’anya, au akijitukuza mwenyewe, au akiwadanganya. Kwa aibu inanipasa niseme kwamba sisi tulikuwa dhaifu sana kwa jambo hilo! Lakini jambo lolote ambalo mtu mwingine angethubutu kujisifia, ninene kama mjinga, nami nathubutu kujisifu kuhusu hilo. Je, wao ni Waebrania? Mimi pia ni Mwebrania. Je, wao ni Waisraeli? Mimi pia ni Mwisraeli. Je, wao ni wazao wa Ibrahimu? Mimi pia ni mzao wa Ibrahimu. Je, wao ni watumishi wa Al-Masihi? (Nanena kiwazimu.) Mimi ni zaidi yao. Nimefanya kazi kwa bidii zaidi yao, nimefungwa gerezani mara kwa mara, nimepigwa mijeledi sana, na nimekabiliwa na mauti mara nyingi. Mara tano nimepigwa na Wayahudi mijeledi arobaini kasoro moja.