2 Wakorintho 11:16-24
2 Wakorintho 11:16-24 Biblia Habari Njema (BHN)
Tena nasema: Mtu asinifikirie kuwa mpumbavu. Lakini kama mkifikiri hivyo, basi, nichukueni kama mpumbavu ili nami nipate kuwa na cha kujivunia angaa kidogo. Ninachosema sasa si kile alichoniagiza Bwana; kuhusu jambo hili la kujivuna, nasema tu kama mtu mpumbavu. Maadamu wengi hujivuna kwa sababu za kidunia, nami pia nitajivuna. Nyinyi ni wenye busara, ndiyo maana hata mnawavumilia wapumbavu! Mnamvumilia hata mtu anayewafanya nyinyi watumwa, mtu mwenye kuwanyonya, mwenye kuwakandamiza, mwenye kuwadharau na kuwapiga usoni! Kwa aibu nakubali kwamba sisi tulikuwa dhaifu. Iwe iwavyo, lakini kama kuna mtu yeyote anayethubutu kujivunia kitu – nasema kama mtu mpumbavu – mimi nathubutu pia. Je, wao ni Waebrania? Hata mimi. Je, wao ni Waisraeli? Hata mimi. Wao ni wazawa wa Abrahamu? Hata mimi. Wao ni watumishi wa Kristo? Hata mimi – nanena hayo kiwazimu – ni mtumishi wa Kristo zaidi kuliko wao. Mimi nimefanya kazi ngumu zaidi, nimekaa gerezani mara nyingi zaidi, nimepigwa mara nyingi zaidi na nimekaribia kifo mara nyingi. Mara tano nilichapwa vile viboko arubaini kasoro kimoja vya Wayahudi.
2 Wakorintho 11:16-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nasema tena, mtu asidhani ya kuwa mimi ni mpumbavu; lakini mjaponidhania hivi, mnikubali kama mpumbavu; ili mimi nami nipate kujisifu angaa kidogo. Ninenalo silineni agizo la Bwana, bali kama kwa upumbavu, katika ujasiri huu wa kujisifu. Kwa sababu wengi wanajisifu kwa jinsi ya mwili, mimi nami nitajisifu. Ninyi, kwa kuwa mna akili, mnachukuliana na wajinga kwa furaha. Maana mwachukuliana na mtu akiwatia utumwani, akiwameza, akiwateka nyara, akijikuza, akiwapiga usoni. Nanena kwa jinsi ya kujidhili kana kwamba sisi tulikuwa dhaifu. Lakini, ikiwa mtu anao ujasiri kwa lolote, (nanena kipuuzi), mimi nami ninao ujasiri. Wao ni Waebrania? Na mimi pia. Wao ni Waisraeli? Na mimi pia. Wao ni uzao wa Abrahamu? Na mimi pia. Wao ni wahudumu wa Kristo? (Nanena kiwazimu), mimi ni zaidi; katika taabu kuzidi sana; katika vifungo kuzidi sana; katika mapigo kupita kiasi; katika mauti mara nyingi. Kwa Wayahudi mara tano nilipata mapigo arubaini kasoro moja.
2 Wakorintho 11:16-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nasema tena, mtu asidhani ya kuwa mimi ni mpumbavu; lakini mjaponidhania hivi, mnikubali kama mpumbavu; ili mimi nami nipate kujisifu ngaa kidogo. Ninenalo silineni agizo la Bwana, bali kama kwa upumbavu, katika ujasiri huu wa kujisifu. Kwa sababu wengi wanajisifu kwa jinsi ya mwili, mimi nami nitajisifu. Ninyi, kwa kuwa mna akili, mnachukuliana na wajinga kwa furaha. Maana mwachukuliana na mtu akiwatia utumwani, akiwameza, akiwateka nyara, akijikuza, akiwapiga usoni. Nanena kwa jinsi ya kujidhili kana kwamba sisi tulikuwa dhaifu. Walakini, akiwa mtu anao ujasiri kwa lo lote, (nanena kipuuzi), mimi nami ninao ujasiri. Wao ni Waebrania? Na mimi pia. Wao ni Waisraeli? Na mimi pia. Wao ni uzao wa Ibrahimu? Na mimi pia. Wao ni wahudumu wa Kristo? (Nanena kiwazimu), mimi ni zaidi; katika taabu kuzidi sana; katika vifungo kuzidi sana; katika mapigo kupita kiasi; katika mauti mara nyingi. Kwa Wayahudi mara tano nalipata mapigo arobaini kasoro moja.
2 Wakorintho 11:16-24 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Nasema tena: mtu yeyote asidhani kwamba mimi ni mjinga. Lakini hata mkinidhania hivyo, basi nipokeeni kama mjinga ili nipate kujisifu kidogo. Ninayosema kuhusiana na huku kujisifu kwa kujiamini, sisemi vile Bwana angesema, bali kama mjinga. Kwa kuwa wengi wanajisifu kama vile ulimwengu ufanyavyo, mimi nami nitajisifu. Ninyi mwachukuliana na wajinga kwa sababu mna hekima sana! Kweli ni kwamba mnachukuliana na mtu akiwatia utumwani au akiwatumia kwa ajili ya kupata faida, au akiwanyangʼanya, au akijitukuza mwenyewe, au akiwadanganya. Kwa aibu inanipasa niseme kwamba sisi tulikuwa dhaifu sana kwa jambo hilo! Lakini jambo lolote ambalo mtu mwingine angethubutu kujisifia, ninene kama mjinga, nami nathubutu kujisifu kuhusu hilo. Je, wao ni Waebrania? Mimi pia ni Mwebrania. Je, wao ni Waisraeli? Mimi pia ni Mwisraeli. Je, wao ni wazao wa Abrahamu? Mimi pia ni mzao wa Abrahamu. Je, wao ni watumishi wa Kristo? (Nanena kiwazimu.) Mimi ni zaidi yao. Nimefanya kazi kwa bidii zaidi yao, nimefungwa gerezani mara kwa mara, nimepigwa mijeledi sana, na nimekabiliwa na mauti mara nyingi. Mara tano nimepigwa na Wayahudi mijeledi arobaini kasoro moja.