2 Wakorintho 10:1-11
2 Wakorintho 10:1-11 NENO
Basi, mimi Paulo ninawasihi kwa unyenyekevu na upole wa Al-Masihi, mimi niliye “mwoga” ninapokuwa pamoja nanyi ana kwa ana, lakini mwenye ujasiri nikiwa mbali nanyi! Nawaomba nitakapokuja kwenu nisipaswe kuwa na ujasiri dhidi ya watu fulani kama ninavyotazamia kwa wale wanaodhani kwamba tunaishi kwa kufuata mtazamo wa ulimwengu huu. Ingawa tunaishi duniani, hatupigani vita kama ulimwengu ufanyavyo. Silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome. Tunaangusha mawazo na kila kitu kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu, na kuteka nyara kila fikira ipate kumtii Al-Masihi. Tena tunakuwa tayari kuadhibu kila tendo la kutotii, hapo kutii kwenu kutakapokamilika. Mnayaangalia yaliyo mbele ya macho yenu tu. Kama mtu yeyote anaamini kuwa yeye ni mali ya Al-Masihi, basi kumbuka kuwa kama ulivyo wa Al-Masihi, vivyo hivyo na sisi ndivyo tulivyo. Basi hata nikijisifu zaidi kidogo kuhusu mamlaka tuliyo nayo, ambayo Bwana Isa alitupatia ili kuwajenga wala si kuwabomoa, mimi sitaionea haya. Sitaki nionekane kama ninayejaribu kuwatisha kwa nyaraka zangu. Kwa maana wanasema, “Nyaraka zake ni nzito na zenye nguvu, lakini ana kwa ana ni mdhaifu, na kuzungumza kwake ni kwa kudharauliwa.” Watu kama hao wajue ya kuwa yale tusemayo kwa barua tukiwa hatupo pamoja nanyi ndivyo tulivyo, na ndivyo tutakavyofanya tutakapokuwa pamoja nanyi.