2 Nyakati 20:14-30
2 Nyakati 20:14-30 NEN
Ndipo Roho wa BWANA akaja juu ya mtu mmoja jina lake Yahazieli mwana wa Zekaria, mwana wa Benaya, Mwana wa Yeieli, mwana wa Matania, Mlawi mzao wa Asafu alipokuwa amesimama katika kusanyiko. Akasema: “Sikilizeni, enyi Yuda wote nanyi nyote mkaao Yerusalemu, nawe Mfalme Yehoshafati! Hili ndilo BWANA asemalo kwenu, ‘Msiogope wala msifadhaike kwa sababu ya jeshi hili kubwa. Kwa maana vita hivi si vyenu, bali ni vya Mungu. Kesho shukeni kukabiliana nao. Watakwea kwa kupandia Genge la Sisi, nanyi mtawakuta mwisho wa bonde, kabla ya Jangwa la Yerueli. Hamtahitaji kupigana vita hivi. Kaeni kwenye nafasi zenu, simameni imara na mkaone wokovu BWANA atakaowapatia, enyi Yuda na Yerusalemu. Msiogope, wala msifadhaike. Kesho tokeni mwende mkawakabili, naye BWANA atakuwa pamoja nanyi.’ ” Yehoshafati akainamisha uso wake chini, nao watu wote wa Yuda na Yerusalemu wakaanguka chini ili kuabudu mbele za BWANA. Ndipo baadhi ya Walawi kutoka kwa Wakohathi na kwa wana wa Kora wakasimama na kumsifu BWANA, Mungu wa Israeli, kwa sauti kuu sana. Asubuhi na mapema wakaondoka kuelekea Jangwa la Tekoa. Walipoanza safari, Yehoshafati akasimama akasema, “Nisikilizeni, enyi Yuda, na watu wa Yerusalemu! Mwaminini BWANA Mungu wenu, hivyo mtathibitika, wasadikini manabii wake nanyi mtafanikiwa. Alipomaliza kushauriana na watu, Yehoshafati akawaweka watu wa kumwimbia BWANA na kumsifu katika utukufu wa utakatifu wake walipokuwa wametangulia mbele ya jeshi, wakisema: “Mshukuruni BWANA kwa kuwa upendo wake wadumu milele.” Walipoanza kuimba na kusifu, BWANA akaweka waviziao dhidi ya watu wa Amoni, Moabu na wale wa Mlima Seiri waliokuwa wamekuja kuishambulia Yuda, nao wakashindwa. Watu wa Amoni na Moabu wakawainukia watu wa Mlima Seiri ili kuwaua na kuwaangamiza kabisa. Baada ya kumaliza kuwachinja watu wa Seiri, wakaangamizana wao kwa wao. Yuda walipofika katika mnara wa ulinzi wa jangwani, wakaliangalia lile jeshi kubwa, wakaona ni maiti tupu zimetapakaa ardhini, wala hakuna yeyote aliyenusurika. Hivyo Yehoshafati na watu wake wakaenda kujitwalia nyara kutoka kwao, nao wakakuta humo wingi wa mifugo, mali, nguo na vitu vya thamani, ambavyo vilikuwa vingi zaidi ya vile walivyoweza kuchukua. Wakakusanya nyara kwa siku tatu kwa sababu zilikuwa nyingi mno. Siku ya nne wakakusanyika katika Bonde la Beraka kwa maana huko ndiko walikomsifu BWANA. Ndiyo sababu linaitwa Bonde la Beraka mpaka leo. Kisha watu wote wa Yuda na Yerusalemu, wakiongozwa na Yehoshafati, wakarudi Yerusalemu wakiwa na furaha kwa kuwa BWANA alikuwa amewasababisha wafurahi juu ya adui zao. Wakaingia Yerusalemu na kwenda hekaluni mwa BWANA wakiwa na vinubi, zeze na tarumbeta. Hofu ya Mungu ikazipata falme zote za nchi waliposikia jinsi BWANA alivyokuwa amepigana dhidi ya adui za Israeli. Ufalme wa Yehoshafati ukawa na amani, kwa kuwa Mungu wake alikuwa amemstarehesha pande zote.