Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Nyakati 19

19
Yehu amkemea Yehoshafati
1Mfalme Yehoshafati wa Yuda akarudi salama kwenye jumba lake la kifalme huko Yerusalemu. 2Yehu mwonaji, mwana wa Hanani, akapanda kwenda kuonana naye akamwambia Mfalme Yehoshafati, “Je, utawasaidia waovu na kuwapenda wale wanaomchukia Mwenyezi Mungu? Kwa sababu ya jambo hili, ghadhabu ya Mwenyezi Mungu iko juu yako. 3Hata hivyo, kuna mema yaliyoonekana kwako, kwa kuwa umeondoa katika nchi nguzo za Ashera na umeukaza moyo wako katika kumtafuta Mungu.”
Yehoshafati aweka waamuzi
4Yehoshafati aliishi huko Yerusalemu, naye akatoka akaenda tena miongoni mwa watu, kuanzia Beer-Sheba hadi nchi ya vilima ya Efraimu na kuwageuza wakamrudia Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zao. 5Akawaweka waamuzi katika nchi, kwenye miji yote ya Yuda yenye ngome. 6Akawaambia, “Angalieni kwa makini yale mnayotenda, kwa kuwa hamkuhukumu kwa ajili ya mwanadamu bali kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ambaye yu pamoja nanyi kila mtoapo hukumu. 7Basi sasa kicho cha Mwenyezi Mungu na kiwe juu yenu. Hukumuni kwa uangalifu, kwa kuwa kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, hakuna jambo la dhuluma, wala upendeleo, wala rushwa.”
8Pia huko Yerusalemu, Yehoshafati akaweka baadhi ya Walawi, makuhani na viongozi wa jamaa za Waisraeli ili kutoa hukumu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kuamua magomvi. Nao waliishi huko Yerusalemu. 9Akawapa maagizo haya: “Ni lazima mtumike kwa uaminifu na kwa moyo wote katika kicho cha Mwenyezi Mungu. 10Katika kila shauri lifikalo mbele yenu kutoka kwa ndugu zenu wanaoishi katika miji, ikiwa ni la umwagaji wa damu au mambo mengine kuhusu sheria, amri, hukumu au maagizo, inawapasa ninyi kuwaonya kwamba wasiingie katika hatia dhidi ya Mwenyezi Mungu, la sivyo ghadhabu yake itakuja juu yenu na ndugu zenu. Tendeni hivyo, nanyi hamtatenda dhambi.
11“Amaria kuhani mkuu atakuwa juu yenu katika jambo lolote linalomhusu Mwenyezi Mungu naye Zebadia mwana wa Ishmaeli, kiongozi wa kabila la Yuda, atakuwa juu yenu kwa jambo lolote linalomhusu mfalme, nao Walawi watatumika kama maafisa mbele yenu. Tendeni kwa ujasiri, naye Mwenyezi Mungu atakuwa pamoja na wale watendao vyema.”

Iliyochaguliwa sasa

2 Nyakati 19: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia