Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wathesalonike Utangulizi

Utangulizi
Paulo katika safari yake ya pili ya kitume alitembelea mji wa Thesalonike, ambao ulikuwa kituo cha biashara. Alihudumu huko kwa majuma matatu, akahubiri katika sinagogi la Wayahudi, akithibitisha kutoka Maandiko ya Agano la Kale kwamba Yesu ndiye Kristo. Baadhi ya Wayahudi na Wayunani wakaamini, lakini ilimlazimu Paulo kuondoka huko haraka kwa sababu ya upinzani mkubwa uliozuka humo.
Baada ya kufika Athene, Paulo alipata habari kutoka kwa Timotheo kuwa ingawa walipata mateso, waumini wa Thesalonike walikuwa wamesimama imara. Paulo aliandika barua hii ili kuwatia moyo na kuwafariji waumini waliokuwa wachanga katika Kristo. Aliwaandikia ili kuimarisha imani yao kuhusu maisha yampasayo Mkristo, na pia kuhusu kurudi kwa Yesu. Yamkini waumini hawa walikuwa na wasiwasi kwamba Wakristo wenzao waliokuwa wamekufa hawangeweza kuufikia ufufuo wa wafu. Hivyo Paulo akawaandikia kuwahakikishia kwamba waliokufa wakiwa wanamwamini Kristo watafufuka kwanza.
Mwandishi
Mtume Paulo.
Kusudi
Kuwaimarisha Wakristo wa Thesalonike katika imani yao, na kuwapa hakikisho kuhusu kurudi kwa Yesu.
Mahali
Korintho.
Tarehe
Kama mwaka wa 51 B.K.
Wahusika Wakuu
Paulo, Timotheo, Silvano.
Wazo Kuu
Kuwatia waumini moyo kudumu katika utakatifu, na kuwahakikishia wale wanaoteswa kwamba Mungu yu pamoja nao na amewaahidi ushindi.
Mambo Muhimu
Paulo aliwaandikia Wathesalonike barua hii ili kuwatia moyo na kuwafariji katika Kristo, na pia kuimarisha imani yao katika misingi ya mafundisho ya Kristo.
Mgawanyo
Shukrani za Paulo kwa ajili ya Wathesalonike (1:1-10)
Huduma ya Paulo katika kanisa (2:1-16)
Maelezo ya matukio tangu kuondoka Thesalonike (2:7–3:13)
Mausia kuhusu mwenendo na maisha ya kumcha Mungu (4:1-12)
Kuhusu kurudi kwa Yesu (4:13–5:11)
Maagizo ya mwisho, na hitimisho (5:12-28).

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia