Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samweli 14

14
1Siku moja Yonathani mwana wa Sauli akamwambia kijana mbeba silaha wake, akasema, “Njoo, tuwavukie Wafilisti kwenye doria upande ule mwingine.” Lakini hakumwambia baba yake.
2Sauli alikuwa akikaa kwenye viunga vya Gibea chini ya mkomamanga huko Migroni. Alikuwa pamoja na watu wapatao mia sita; 3miongoni mwao alikuwepo Ahiya, aliyekuwa amevaa kizibau. Alikuwa mwana wa Ikabodi, nduguye Ahitubu mwana wa Finehasi, mwana wa Eli, kuhani wa Mwenyezi Mungu huko Shilo. Hakuna yeyote aliyekuwa na habari kwamba Yonathani alikuwa ameondoka.
4Kila upande wa njia ambayo Yonathani alikusudia kupita ili kuvuka kufikia doria ya Wafilisti kulikuwa na jabali; moja lilikuwa linaitwa Bosesi, na jingine Sene. 5Jabali moja lilisimama kaskazini kuelekea Mikmashi na jingine upande wa kusini kuelekea Geba.
6Yonathani akamwambia kijana wake mbeba silaha, “Njoo, tuvukie doria ya wale jamaa wasiotahiriwa. Huenda Mwenyezi Mungu atatenda kwa ajili yetu. Hakuna chochote kitakachoweza kumzuia Mwenyezi Mungu kuokoa, kwamba ni kwa wingi au kwa uchache.”
7Mbeba silaha wake akamwambia, “Fanya yale yote uliyo nayo katika moyo wako. Songa mbele; moyo wangu na roho yangu viko pamoja nawe.”
8Yonathani akasema, “Basi njoo; tutavuka kuwaelekea hao watu na kuacha watuone. 9Wakituambia, ‘Subirini hapo hadi tuje kwenu,’ tutakaa pale tulipo na hatutakwea kwao. 10Lakini kama watasema, ‘Pandeni mje kwetu,’ tutakwea, kwa sababu hiyo itakuwa ishara yetu kwamba Mwenyezi Mungu amewatia mikononi mwetu.”
11Basi wote wawili wakajionesha kwa doria ya Wafilisti. Wafilisti wakasema, “Tazama! Waebrania wanatambaa toka mashimoni walimokuwa wamejificha.” 12Wanaume wa kwenye doria wakawapazia sauti Yonathani na mbeba silaha wake, wakisema, “Njooni, pandeni kwetu, nasi tutawakomesha.”
Basi Yonathani akamwambia mbeba silaha wake, “Panda nyuma yangu; Mwenyezi Mungu amewatia mikononi mwa Israeli.”
13Yonathani akapanda juu, akitumia mikono yake na miguu, pamoja na mbeba silaha wake papo hapo nyuma yake. Wafilisti wakaanguka mbele ya Yonathani, naye mbeba silaha wake akamfuata akiwaua nyuma yake. 14Katika hilo shambulio la kwanza, Yonathani na mbeba silaha wake waliua kama watu ishirini kwenye eneo kama la nusu eka.
Waisraeli wafukuza Wafilisti
15Kisha fadhaa ikawapata jeshi lote, wale waliokuwa kambini na shambani, wale waliokuwa katika doria na makundi ya washambuliaji, nayo ardhi ilitetemeka. Ilikuwa ni hofu ya ghafula iliyotumwa na Mungu.
16Wapelelezi wa Sauli huko Gibea ya Benyamini wakaona jeshi likitokomea pande zote. 17Ndipo Sauli akawaambia watu wale waliokuwa pamoja naye, “Kagueni jeshi mkaone ni nani ameondoka kwetu.” Walipokagua, akawa ni Yonathani na mbeba silaha wake ambao hawakuwepo.
18Sauli akamwambia Ahiya, “Leta Sanduku la Mungu.” (Wakati huo lilikuwa kwa Waisraeli.) 19Sauli alipokuwa akisema na kuhani, makelele katika kambi ya Wafilisti yakaongezeka zaidi na zaidi. Hivyo Sauli akamwambia kuhani, “Rudisha mkono wako.”
20Kisha Sauli na watu wake wote wakakusanyika na kwenda vitani. Wakawakuta Wafilisti wakiwa wamechanganyikiwa kabisa, wakitiana panga kila mmoja na wenzake. 21Wale Waebrania ambao walishakuwa pamoja na Wafilisti, na waliokuwa wamepanda pamoja nao katika kambi zao, wakaenda upande wa Waisraeli waliokuwa pamoja na Sauli na Yonathani. 22Waisraeli wote waliokuwa wamejificha katika nchi ya vilima ya Efraimu waliposikia kuwa Wafilisti wamekimbia, wakajiunga vitani na kuwafuata kwa bidii. 23Hivyo Mwenyezi Mungu akawaokoa Waisraeli siku ile, navyo vita vilienea hadi kupita Beth-Aveni.
Yonathani ala Asali
24Basi Waisraeli walikuwa katika dhiki siku ile, kwa sababu Sauli alikuwa amewafunga watu kwa kiapo, akisema, “Alaaniwe mtu yeyote atakayekula chakula kabla ya jioni, kabla sijalipiza kisasi juu ya adui zangu!” Kwa hiyo hakuna mtu yeyote katika jeshi aliyeonja chakula.
25Jeshi lote liliingia mwituni, na huko kulikuwa na asali juu ya ardhi. 26Walipoingia mwituni, wakaona asali ikitiririka, hata hivyo hakuna mtu yeyote aliyetia mkono wake kinywani, kwa sababu waliogopa kiapo. 27Lakini Yonathani alikuwa hajasikia kuwa baba yake alikuwa amewafunga watu kwa kiapo, hivyo akainyoosha ncha ya fimbo iliyokuwa mkononi mwake na kuichovya katika sega la asali. Akainua mkono wake na kuutia kinywani mwake, nayo macho yake yakaangaa. 28Kisha mmoja wa askari wake akamwambia, “Baba yako alilifunga jeshi kwa kiapo kikali, akisema, ‘Alaaniwe mtu yeyote alaye chakula leo!’ Ndiyo sababu watu wanalegea.”
29Yonathani akasema, “Baba yangu ameitaabisha nchi. Ona jinsi macho yangu yalipata kuangaa nilipoonja asali hii kidogo. 30Ingekuwa bora zaidi mara ngapi kama watu wangekula leo baadhi ya nyara walizoteka kutoka kwa adui zao. Je, mauaji ya Wafilisti yasingekuwa makubwa zaidi?”
31Siku ile baada ya Waisraeli kuwaua Wafilisti kutoka Mikmashi hadi Aiyaloni, walikuwa wamechoka. 32Watu wakarukia zile nyara, wakichukua kondoo, ng’ombe na ndama, wakawachinja hapo juu ya nchi na kuwala, pamoja na damu. 33Kisha mtu mmoja akamwambia Sauli, “Tazama, watu wanatenda dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu kwa kula nyama yenye damu.”
Akasema, “Mmevunja uaminifu. Livingirisheni jiwe kubwa hapa mara moja.” 34Kisha Sauli akasema, “Nendeni miongoni mwa watu, mwaambie, ‘Kila mmoja wenu aniletee ng’ombe wake na kondoo, mwachinjie hapa na mle. Msitende dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu kwa kula nyama ikiwa na damu ndani yake.’ ”
Hivyo kila mmoja akaleta ng’ombe wake jioni ile na kumchinja hapo. 35Ndipo Sauli akamjengea Mwenyezi Mungu madhabahu, na ndiyo ilivyokuwa mara yake ya kwanza kujenga madhabahu.
36Sauli akasema, “Tuteremke tufuatie Wafilisti usiku na kuwateka nyara hadi mapambazuko, nasi tusiache hata mmoja wao hai.”
Wakajibu, “Fanya lolote lile uonalo jema zaidi kwako.”
Lakini kuhani akasema, “Tuulize kwa Mungu mahali hapa.”
37Basi Sauli akamuuliza Mungu, akisema, “Je, niteremke kuwafuatia Wafilisti? Je, utawatia mikononi mwa Israeli?” Lakini Mungu hakumjibu siku ile.
38Kwa hiyo Sauli akasema, “Njooni hapa, ninyi nyote ambao ni viongozi wa jeshi, na tutafute ni dhambi gani imefanywa leo. 39Kwa hakika kama Mwenyezi Mungu aiokoaye Israeli aishivyo, hata kama itakuwa kwa mwana wangu Yonathani, ni lazima afe.” Lakini hakuna mtu yeyote aliyesema neno.
40Kisha Sauli akawaambia Waisraeli wote, “Ninyi simameni huko; mimi na mwanangu Yonathani tutasimama hapa.”
Watu wakajibu, “Fanya lile unaloona jema zaidi kwako.”
41Kisha Sauli akamwomba Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, akisema, “Kwa nini hujamjibu mtumishi wako leo? Ikiwa makosa ni yangu au ya mwanangu Yonathani, jibu kwa Urimu. Lakini ikiwa makosa ni ya wanaume wa Israeli, jibu kwa Thumimu.”#14:41 Maandiko ya Kiebrania hayana maneno: “Kwa nini … Thumimu.” Yana maneno: “Nipe jibu lililo sawa.” Yonathani na Sauli wakatolewa kwa kura, nao watu wakawa salama. 42Sauli akasema, “Pigeni kura kati yangu na mwanangu Yonathani.” Kura ikamwangukia Yonathani.
43Basi Sauli akamwambia Yonathani, “Niambie ni nini ulichokifanya.”
Hivyo Yonathani akamwambia, “Nilionja tu asali kidogo kwa ncha ya fimbo yangu. Je, sasa ni lazima nife?”
44Sauli akasema, “Mungu na aniadhibu vikali zaidi kama wewe Yonathani hutakufa.”
45Lakini watu wakamwambia Sauli, “Je, Yonathani atakufa, yeye ambaye ameleta ukombozi huu mkubwa kwa Israeli? Hasha! Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, hakuna hata unywele wa kichwa chake utakaoanguka juu ya ardhi, kwa kuwa alifanya jambo hili leo kwa msaada wa Mungu.” Basi watu wakamwokoa Yonathani, wala hakuuawa.
46Kisha Sauli akaacha kuwafuata Wafilisti, nao wakajiondoa na kurudi katika nchi yao.
47Baada ya Sauli kujitwalia utawala katika Israeli, alipigana dhidi ya adui zake kila upande: Moabu, Waamoni, Edomu, wafalme wa Soba, na Wafilisti. Popote alipogeukia, aliwashinda. 48Akapigana kishujaa na kuwashinda Waamaleki, akiikomboa Israeli kutoka mikono ya wale waliokuwa wamewateka nyara.
Jamaa ya Sauli
49Wana wa Sauli walikuwa Yonathani, Ishvi na Malki-Shua. Jina la binti yake mkubwa lilikuwa Merabu, naye mdogo aliitwa Mikali. 50Jina la mkewe Sauli aliitwa Ahinoamu binti Ahimaasi. Jina la jemadari wa jeshi la Sauli aliitwa Abneri mwana wa Neri, naye Neri alikuwa babaye mdogo Sauli. 51Babaye Sauli, yaani Kishi, na Neri baba yake Abneri walikuwa wana wa Abieli.
52Siku zote za utawala wa Sauli zilikuwa za vita vikali dhidi ya Wafilisti, na wakati wowote Sauli alimwona mtu mwenye nguvu au shujaa, alimchukua kwa utumishi wake.

Iliyochaguliwa sasa

1 Samweli 14: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia