1 Petro 1:1-8
1 Petro 1:1-8 NENO
Petro, mtume wa Isa Al-Masihi. Kwa wateule wa Mungu, wageni katika ulimwengu, waliotawanyika kote katika Ponto, Galatia, Kapadokia, jimbo la Asia, na Bithinia. Ni ninyi ambao mlichaguliwa tangu mwanzo na Mungu Baba Mwenyezi kulingana na alivyotangulia kuwajua, kupitia kwa kazi ya utakaso wa Roho wa Mungu, katika utiifu kwa Isa Al-Masihi na kunyunyiziwa damu yake. Neema na amani ziwe kwenu kwa wingi. Ahimidiwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Isa Al-Masihi! Kwa rehema zake kuu, ametuzaa sisi mara ya pili katika tumaini lenye uzima, kupitia kwa kufufuka kwa Isa Al-Masihi kutoka kwa wafu, ili tuupate urithi usioangamia, usioharibika, na usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu. Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kupitia kwa imani, hadi utakapokuja ule wokovu ulio tayari kufunuliwa nyakati za mwisho. Katika haya yote mnafurahi sana, ijapokuwa kwa muda mfupi sasa mmehuzunishwa kwa majaribu ya aina nyingi. Haya yamewajia ili imani yenu, iliyo ya thamani kuliko dhahabu ipoteayo ingawa inasafishwa kwa moto, ionekane kuwa halisi, na imalizie kwa sifa, utukufu na heshima Isa Al-Masihi atakapodhihirishwa. Ijapokuwa hamjamwona, mnampenda; tena ingawa sasa hammwoni, mnamwamini na kujawa na furaha yenye utukufu na isiyoelezeka.