1 Wafalme 8:54-66
1 Wafalme 8:54-66 NENO
Sulemani alipomaliza dua na maombi haya yote kwa Mwenyezi Mungu, akainuka kutoka mbele ya madhabahu ya Mwenyezi Mungu, mahali alipokuwa amepiga magoti akiwa amenyoosha mikono yake kuelekea mbinguni. Akasimama na kubariki kusanyiko lote la Israeli kwa sauti kubwa, akisema: “Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, aliyewapa pumziko watu wake Israeli kama alivyokuwa ameahidi. Hakuna hata neno moja lililopunguka kati ya ahadi zote nzuri alizozitoa kupitia mtumishi wake Musa. Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, na awe pamoja nasi kama alivyokuwa na baba zetu, kamwe asituache wala kutukataa. Yeye na aielekeze mioyo yetu kwake, ili tutembee katika njia zake zote na kushika amri, maagizo, na masharti aliyowapa baba zetu. Nami maneno yangu haya, ambayo nimeyaomba mbele za Mwenyezi Mungu, yawe karibu na Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, usiku na mchana, ili awape haki mtumishi wake na watu wake Israeli, kulingana na mahitaji yao ya kila siku, ili mataifa yote ya dunia wajue kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Mungu na kwamba hakuna mwingine. Lazima mwiweke mioyo yenu kikamilifu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, mwishi kwa maagizo yake na kutii amri zake, kama ilivyo wakati huu.” Kisha mfalme na Waisraeli wote pamoja naye wakatoa dhabihu mbele za Mwenyezi Mungu. Sulemani akatoa dhabihu sadaka za amani kwa Mwenyezi Mungu: ng’ombe elfu ishirini na mbili, pamoja na kondoo na mbuzi elfu mia moja na ishirini. Ndivyo mfalme na Waisraeli wote walivyoweka wakfu Hekalu la Mwenyezi Mungu. Siku hiyo hiyo mfalme akaweka wakfu sehemu ya katikati ya ua uliokuwa mbele ya Hekalu la Mwenyezi Mungu, na hapo akatoa sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka, na mafuta ya wanyama wa sadaka za amani, kwa sababu madhabahu ya shaba iliyokuwa mbele za Mwenyezi Mungu ilikuwa ndogo sana kuweza kubeba sadaka hizo za kuteketezwa, sadaka za nafaka, na mafuta ya wanyama wa sadaka za amani. Hivyo Sulemani akaiadhimisha sikukuu kwa wakati ule, na Waisraeli wote pamoja naye: walikuwa kusanyiko kubwa sana, watu kutoka Lebo-Hamathi hadi Kijito cha Misri. Wakaiadhimisha mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, kwa siku saba na siku saba zaidi, yaani jumla siku kumi na nne. Siku iliyofuata, aliwaruhusu watu waondoke. Wakambariki mfalme, kisha wakaenda nyumbani wakiwa na mashangilio na furaha moyoni kwa ajili ya mambo yote mema ambayo Mwenyezi Mungu alimtendea kwa ajili ya Daudi mtumishi wake na watu wake Israeli.