1 Wafalme 8:54-66
1 Wafalme 8:54-66 NEN
Wakati Solomoni alipomaliza dua hizi zote na maombi kwa BWANA, akainuka kutoka mbele ya madhabahu ya BWANA, mahali alipokuwa amepiga magoti, mikono yake ikawa imekunjuliwa kuelekea juu mbinguni. Akasimama na kubariki kusanyiko lote la Israeli kwa sauti kubwa akisema: “Ahimidiwe BWANA, aliyewapa pumziko watu wake Israeli kama vile alivyokuwa ameahidi. Hakuna hata neno moja lililopunguka kati ya ahadi zote nzuri alizozitoa kupitia mtumishi wake Mose. BWANA Mungu wetu na awe pamoja nasi kama alivyokuwa na baba zetu, kamwe asituache wala kutukataa. Yeye na aielekeze mioyo yetu kwake, ili tutembee katika njia zake zote na kuzishika amri na maagizo na masharti aliyowapa baba zetu. Nami maneno yangu haya, ambayo nimeyaomba mbele za BWANA, yawe karibu na BWANA Mungu wetu usiku na mchana, ili kwamba atetee shauri la mtumishi wake na la watu wake Israeli kulingana na hitaji lao la kila siku, ili kwamba mataifa yote ya dunia wajue kwamba BWANA ndiye Mungu na kwamba hakuna mwingine. Lakini ni lazima mwiweke mioyo yenu kikamilifu kwa BWANA Mungu wetu, kuishi kwa maagizo yake na kutii amri zake, kama ilivyo wakati huu.” Kisha mfalme na Israeli wote pamoja naye wakatoa dhabihu mbele za BWANA. Solomoni akatoa dhabihu sadaka za amani kwa BWANA: ngʼombe 22,000, pamoja na kondoo na mbuzi 120,000. Hivyo ndivyo mfalme na Waisraeli wote walivyoweka wakfu Hekalu la BWANA. Siku iyo hiyo mfalme akaweka wakfu sehemu ya katikati ya ua uliokuwa mbele ya Hekalu la BWANA na hapo akatoa sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka na mafuta ya sadaka za amani, kwa sababu madhabahu ya shaba iliyokuwa mbele za BWANA ilikuwa ndogo sana kuweza kubeba sadaka hizo za kuteketezwa, sadaka za nafaka na mafuta ya sadaka ya amani. Hivyo Solomoni akaiadhimisha sikukuu kwa wakati ule, na Israeli wote pamoja naye. Walikuwa kusanyiko kubwa sana, watu kutoka Lebo-Hamathi hadi Kijito cha Misri. Wakaiadhimisha mbele za BWANA Mungu wetu kwa siku saba na siku saba zaidi, yaani, jumla siku kumi na nne. Siku iliyofuata, aliwaruhusu watu waondoke. Wakambariki mfalme, kisha wakaenda nyumbani, wakiwa na mashangilio na furaha rohoni kwa ajili ya mambo yote mema ambayo BWANA ametenda kwa ajili ya Daudi mtumishi wake na watu wake Israeli.