1 Wafalme 21:17-29
1 Wafalme 21:17-29 NEN
Kisha neno la BWANA likamjia Eliya, Mtishbi: “Shuka ukakutane na Ahabu mfalme wa Israeli, anayetawala Samaria. Sasa yuko katika shamba la mizabibu la Nabothi, ambapo amekwenda alimiliki. Umwambie, ‘Hivi ndivyo BWANA asemavyo: Je, hujamuua mtu na kuitwaa mali yake?’ Kisha umwambie, ‘Hivi ndivyo asemavyo BWANA: Mahali ambapo mbwa waliramba damu ya Nabothi, mbwa watairamba damu yako, naam, yako wewe!’ ” Ahabu akamwambia Eliya, “Kwa hiyo umenipata, wewe adui yangu!” Akajibu, “Ndiyo, nimekupata. Kwa sababu umejiuza mwenyewe kufanya uovu mbele ya macho ya BWANA. ‘Nitaleta maafa juu yako. Nitaangamiza uzao wako na kukatilia mbali kutoka kwa Ahabu kila mzaliwa wa mwisho wa kiume katika Israeli, wa mtumwa au wa mtu huru. Nitaifanya nyumba yako kama ile ya Yeroboamu mwana wa Nebati na ile ya Baasha mwana wa Ahiya, kwa sababu umenighadhibisha kwa kuwa umesababisha Israeli kutenda dhambi.’ “Pia kwa habari ya Yezebeli BWANA anasema, ‘Mbwa watamla Yezebeli karibu na ukuta wa Yezreeli.’ “Mbwa watawala wale wa nyumba ya Ahabu watakaofia mjini, nao wale watakaofia mashambani wataliwa na ndege wa angani.” (Hapajapata kamwe kuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza mwenyewe kutenda uovu machoni mwa BWANA, akiwa anachochewa na Yezebeli mkewe. Alitenda kwa uovu sana katika kuabudu sanamu, kama wale Waamori ambao BWANA aliowafukuza mbele ya Israeli.) Ahabu aliposikia maneno haya, akararua nguo zake, akavaa nguo za gunia na kufunga. Akalala na kujifunika nguo za gunia na kwenda kwa unyenyekevu. Ndipo neno la BWANA lilipomjia Eliya Mtishbi kusema, “Umeona jinsi Ahabu alivyojinyenyekeza mbele zangu? Kwa kuwa amejishusha mwenyewe, sitaleta maafa haya wakati akiwa hai, lakini nitayaleta juu ya nyumba yake katika siku za mwanawe.”