Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 2:1-11

1 Wafalme 2:1-11 NEN

Siku zilipokaribia za Daudi kufa, akampa mwanawe Solomoni agizo. Akasema, “Mimi ninakaribia kwenda njia ya dunia yote. Hivyo uwe hodari, jionyeshe kuwa mwanaume, shika lile BWANA Mungu wako analokuagiza: Enenda katika njia zake, ushike maagizo na amri zake, sheria zake na kanuni zake, kama ilivyoandikwa katika Sheria ya Mose, ili upate kustawi katika yote ufanyayo na popote uendako, ili kwamba BWANA aweze kunitimizia ahadi yake: ‘Kama wazao wako wakiangalia sana wanavyoishi, na kama wakienenda kwa uaminifu mbele zangu kwa mioyo yao yote na kwa roho zao zote, kamwe hutakosa kuwa na mtu kwenye kiti cha ufalme cha Israeli.’ “Sasa wewe mwenyewe unafahamu lile Yoabu mwana wa Seruya alilonitendea, lile alilofanya kwa majemadari wawili wa majeshi ya Israeli, Abneri mwana wa Neri, na Amasa mwana wa Yetheri. Aliwaua, akimwaga damu yao wakati wa amani kama vile ni kwenye vita, tena akaipaka damu ile kwenye mkanda uliokuwa kiunoni mwake na viatu alivyovaa miguuni mwake. Shughulika naye kwa kadiri ya hekima yako, lakini usiache kichwa chake chenye mvi kishukie kaburi kwa amani. “Lakini uwaonyeshe wema wana wa Barzilai wa Gileadi na uwaruhusu wawe miongoni mwa wale walao mezani pako. Walisimama nami nilipomkimbia ndugu yako Absalomu. “Ukumbuke, unaye Shimei mwana wa Gera, Mbenyamini kutoka Bahurimu, ambaye alinilaani kwa laana kali siku niliyokwenda Mahanaimu. Aliposhuka kunilaki huko Yordani, nilimwapia kwa BWANA: ‘Sitakuua kwa upanga!’ Lakini sasa, usidhani kwamba hana hatia. Wewe ni mtu wa hekima, utajua la kumtendea. Zishushe mvi zake kaburini kwa damu.” Kisha Daudi akapumzika pamoja na baba zake naye akazikwa katika Mji wa Daudi. Daudi alikuwa ametawala juu ya Israeli miaka arobaini: huko Hebroni alitawala miaka saba, na katika Yerusalemu akatawala miaka thelathini na mitatu.