1 Wafalme 19:15-21
1 Wafalme 19:15-21 NEN
BWANA akamwambia, “Rudi kwa njia uliyoijia, uende kwenye Jangwa la Dameski. Wakati utakapofika huko, mtie Hazaeli mafuta awe mfalme wa Aramu Pia mtie mafuta Yehu mwana wa Nimshi awe mfalme wa Israeli, na umtie Elisha mwana wa Shafati kutoka Abel-Mehola mafuta awe nabii badala yako. Yehu atamuua yeyote atakayeutoroka upanga wa Hazaeli, naye Elisha atamuua yeyote atakayeutoroka upanga wa Yehu. Hata sasa nimeweka akiba watu elfu saba katika Israeli, wote ambao hawajampigia Baali magoti, na wote ambao midomo yao haijambusu.” Hivyo Eliya akaondoka kutoka huko na kumkuta Elisha mwana wa Shafati. Alikuwa akilima kwa jozi kumi na mbili za maksai, na yeye mwenyewe aliongoza ile jozi ya kumi na mbili. Eliya akapita karibu naye, akamrushia vazi lake. Kisha Elisha akawaacha maksai wake, akamkimbilia Eliya, akamwambia, “Niruhusu nikawabusu baba yangu na mama yangu, halafu nitafuatana nawe.” Eliya akajibu, “Rudi zako, kwani nimekutendea nini?” Basi Elisha akamwacha Eliya, naye akarudi. Akachukua ile jozi yake ya maksai na kuwachinja. Akaipika ile nyama kwa kutumia miti ya nira kama kuni na kuwapa watu, nao wakala. Kisha akaondoka, akamfuata Eliya, akamtumikia.