Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 18:30-46

1 Wafalme 18:30-46 NEN

Kisha Eliya akawaambia watu wote, “Sogeeni karibu nami.” Watu wote wakamkaribia, naye akakarabati madhabahu ya BWANA, ambayo ilikuwa imevunjwa. Eliya akachukua mawe kumi na mawili, moja kwa ajili ya kila kabila la wana wa Yakobo, ambaye neno la BWANA lilimjia, likisema, “Jina lako litakuwa Israeli.” Kwa mawe hayo, akajenga madhabahu katika jina la BWANA, na akachimba handaki kuizunguka, ukubwa wa kutosha vipimo viwili vya mbegu. Akapanga kuni, akamkata yule fahali vipande vipande na kuvipanga juu ya kuni. Kisha akawaambia, “Jazeni mapipa manne maji na kuyamwaga juu ya sadaka ya kuteketezwa na juu ya kuni.” Akawaambia, “Fanyeni hivyo tena.” Nao wakafanya hivyo tena. Akaagiza, “Fanyeni kwa mara ya tatu.” Nao wakafanya hivyo kwa mara ya tatu. Maji yakatiririka kuizunguka madhabahu na hata kujaza lile handaki. Wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, nabii Eliya akasogea mbele na kuomba, akisema: “Ee BWANA, Mungu wa Abrahamu, na Isaki na Israeli, ijulikane leo kwamba wewe ndiye Mungu katika Israeli na ya kwamba mimi ni mtumishi wako na nimefanya mambo haya yote kwa neno lako. Unijibu mimi, Ee BWANA, nijibu mimi, ili watu hawa wajue kwamba wewe, Ee BWANA, ndiwe Mungu, na kwamba unaigeuza mioyo yao ikurudie tena.” Kisha moto wa BWANA ukashuka na kuiteketeza ile dhabihu, zile kuni, yale mawe, ule udongo, na pia kuramba yale maji yaliyokuwa ndani ya handaki. Wakati watu wote walipoona hili, wakaanguka kifudifudi na kulia, “BWANA: yeye ndiye Mungu! BWANA: yeye ndiye Mungu!” Kisha Eliya akawaamuru, “Wakamateni hao manabii wa Baali. Msimwache hata mmoja atoroke!” Wakawakamata, naye Eliya akawaleta mpaka Bonde la Kishoni na kuwachinja huko. Eliya akamwambia Ahabu, “Nenda, ukale na kunywa, kwa kuwa kuna sauti ya mvua kubwa.” Hivyo Ahabu akaondoka ili kula na kunywa. Lakini Eliya akapanda kileleni mwa Karmeli, akasujudu na akaweka kichwa chake katikati ya magoti yake. Akamwambia mtumishi wake, “Nenda ukatazame kuelekea bahari.” Akaenda na kutazama. Akasema, “Hakuna kitu chochote huko.” Mara saba Eliya akasema, “Nenda tena.” Mara ya saba, mtumishi akaleta taarifa, “Wingu dogo kama mkono wa mwanadamu linainuka kutoka baharini.” Hivyo Eliya akasema, “Nenda ukamwambie Ahabu, ‘Tandika gari lako na ushuke kabla mvua haijakuzuia.’ ” Wakati ule ule anga likawa jeusi kwa mawingu, upepo ukainuka na mvua kubwa ikanyesha, naye Ahabu akaenda zake Yezreeli. Nguvu za BWANA zikamjia Eliya, naye akajikaza viuno, akakimbia mbele ya Ahabu njia yote hadi maingilio ya Yezreeli.

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha