1 Wafalme 15:1-8
1 Wafalme 15:1-8 NEN
Katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wa Yeroboamu mwana wa Nebati, Abiya akawa mfalme wa Yuda, naye akatawala huko Yerusalemu miaka mitatu. Mama yake aliitwa Maaka binti Abishalomu. Alitenda dhambi zote baba yake alizotenda kabla yake; moyo wake haukuwa mkamilifu kwa BWANA Mungu wake kama moyo wa Daudi baba yake ulivyokuwa. Pamoja na hayo, kwa ajili ya Daudi, BWANA Mungu wake akampa taa katika Yerusalemu kwa kumwinua mwana atawale badala yake na kwa kuifanya Yerusalemu kuwa imara. Kwa kuwa Daudi alifanya yaliyo mema machoni pa BWANA na hakushindwa kushika maagizo yote ya BWANA siku zote za uhai wake, isipokuwa katika habari ya Uria, Mhiti. Kulikuwa na vita kati ya Rehoboamu na Yeroboamu wakati wote wa maisha ya Abiya. Kwa habari ya matukio mengine ya utawala wa Abiya na yote aliyofanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? Kulikuwa na vita kati ya Abiya na Yeroboamu. Naye Abiya akalala na baba zake akazikwa katika Mji wa Daudi. Asa mwanawe akawa mfalme baada yake.