1 Wafalme 11:26-43
1 Wafalme 11:26-43 NENO
Pia, Yeroboamu mwana wa Nebati aliasi dhidi ya mfalme. Alikuwa mmoja wa maafisa wa Sulemani, Mwefraimu kutoka Sereda, ambaye mama yake alikuwa mjane aliyeitwa Serua. Haya ndio maelezo ya jinsi alivyomwasi mfalme: Sulemani alikuwa amejenga Milo naye akawa ameziba mwanya katika ukuta wa mji wa Daudi baba yake. Basi Yeroboamu alikuwa mtu mwenye nguvu na hodari; naye Sulemani alipoona jinsi kijana alivyofanya kazi yake, akamweka kuwa kiongozi wa kazi yote ya mikono ya nyumba ya Yusufu. Karibu na wakati ule Yeroboamu alikuwa anatoka nje ya Yerusalemu, Ahiya nabii Mshiloni akakutana naye njiani, akiwa amevaa joho jipya. Hawa wawili walikuwa peke yao mashambani, naye Ahiya akachukua joho jipya alilokuwa amevaa akalirarua vipande kumi na viwili. Kisha akamwambia Yeroboamu, “Jichukulie vipande kumi, kwa kuwa hivi ndivyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, asemavyo: ‘Tazama, ninaenda kumnyang’anya Sulemani ufalme na kukupa makabila kumi. Lakini kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi na mji wa Yerusalemu, ambao nimeuchagua miongoni mwa makabila yote ya Israeli, atakuwa na kabila moja. Nitafanya haya kwa sababu wameniacha na kuabudu Ashtorethi mungu wa kike wa Wasidoni, Kemoshi mungu wa Wamoabu, na Moleki mungu wa Waamoni, nao hawakuenda katika njia zangu wala kufanya yaliyo sawa machoni pangu, wala kushika amri na sheria zangu kama Daudi, babaye Sulemani, alivyofanya. “ ‘Lakini sitauondoa ufalme wote mkononi mwa Sulemani; nimemfanya mtawala siku zote za maisha yake kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu, niliyemchagua na ambaye aliyatunza maagizo na amri zangu. Nitauondoa ufalme kutoka mikononi mwa mwanawe na kukupa wewe makabila kumi. Nitampa mwanawe kabila moja ili Daudi mtumishi wangu awe na taa mbele zangu daima katika Yerusalemu, mji ambao nimeuchagua kuweka Jina langu. Lakini wewe, Yeroboamu, nitakutwaa, nawe utatawala yale yote moyo wako unayotamani; utakuwa mfalme wa Israeli. Ikiwa utafanya kila nitakalokuamuru, kuenenda katika njia zangu na kufanya yaliyo sawa mbele za macho yangu kwa kushika amri zangu na maagizo yangu kama alivyofanya Daudi mtumishi wangu, nitakuwa pamoja nawe. Nitakujengea ufalme utakaodumu kama ule niliomjengea Daudi, nami nitakupa Israeli. Nitawatesa wazao wa Daudi kwa ajili ya haya, lakini siyo milele.’ ” Sulemani akajaribu kumuua Yeroboamu, lakini Yeroboamu akakimbilia Misri, kwa Mfalme Shishaki, naye akakaa huko hadi Sulemani alipofariki. Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Sulemani, yote aliyoyafanya na hekima aliyoionesha, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za Sulemani? Sulemani alitawala Israeli yote miaka arobaini, akiwa Yerusalemu. Kisha Sulemani akalala na baba zake, akazikwa katika mji wa Daudi, baba yake. Naye Rehoboamu mwanawe akawa mfalme baada yake.