Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 1:22-37

1 Wafalme 1:22-37 NEN

Alipokuwa angali anazungumza na mfalme, nabii Nathani akafika. Wakamwambia mfalme, “Nabii Nathani yuko hapa.” Kisha akaenda mbele ya mfalme na kumsujudia hadi uso wake ukagusa ardhi. Nathani akasema, “Je, bwana wangu mfalme, umetangaza kuwa Adoniya atakuwa mfalme baada yako na kwamba ataketi kwenye kiti chako cha ufalme? Leo ameshuka na kutoa dhabihu idadi kubwa ya ngʼombe, ndama walionona na kondoo. Amewaalika wana wote wa mfalme, jemadari wa jeshi na kuhani Abiathari. Sasa hivi, wanakula na kunywa pamoja naye wakisema, ‘Aishi maisha marefu, Mfalme Adoniya!’ Lakini mimi mtumishi wako, kuhani Sadoki, Benaya mwana wa Yehoyada na mtumishi wako Solomoni hakutualika. Je, hili ni jambo ambalo bwana wangu mfalme amelifanya pasipo kuwajulisha watumishi wake ili wapate kujua ni nani atakayeketi kwenye kiti cha ufalme cha bwana wangu mfalme baada yake?” Ndipo Mfalme Daudi akasema, “Mwite Bathsheba, aingie ndani.” Hivyo akaingia mbele ya mfalme na kusimama mbele yake. Ndipo mfalme akaapa: “Hakika kama BWANA aishivyo, ambaye ameniokoa kutoka kila taabu, hakika nitatekeleza leo kile nilichokuapia kwa BWANA, Mungu wa Israeli: Mwanao Solomoni atakuwa mfalme baada yangu, naye ataketi kwenye kiti changu cha ufalme baada yangu.” Kisha Bathsheba akasujudu akipiga magoti mbele ya mfalme uso wake ukigusa ardhi akasema, “Bwana wangu Mfalme Daudi na aishi milele!” Mfalme Daudi akasema, “Mwite kuhani Sadoki ndani, nabii Nathani na Benaya mwana wa Yehoyada.” Walipofika mbele ya mfalme, akawaambia: “Wachukueni watumishi wa bwana wenu pamoja nanyi na mkamkalishe mwanangu Solomoni juu ya nyumbu wangu mwenyewe mkamteremshe hadi Gihoni. Huko kuhani Sadoki na nabii Nathani wamtie mafuta awe mfalme juu ya Israeli. Pigeni tarumbeta na mpaze sauti, ‘Mfalme Solomoni aishi maisha marefu!’ Kisha mtapanda pamoja naye, atakuja na kuketi kwenye kiti changu cha ufalme na kutawala badala yangu. Nimemweka awe mtawala juu ya Israeli na Yuda.” Benaya mwana wa Yehoyada akamjibu mfalme, “Amen! BWANA, Mungu wa bwana wangu mfalme, na aseme vivyo hivyo. Kama vile BWANA alivyokuwa na bwana wangu mfalme, vivyo hivyo na awe na Solomoni kukifanya kiti chake cha utawala kuwa kikuu kuliko kile cha bwana wangu Mfalme Daudi!”