Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Yohana 2:18-27

1 Yohana 2:18-27 NENO

Watoto wadogo, huu ni wakati wa mwisho! Kama mlivyosikia kwamba anayempinga Al-Masihi anakuja, hivyo basi wanaompinga Al-Masihi wengi wamekwisha kuja. Kutokana na hili twajua kwamba huu ni wakati wa mwisho. Walitoka kwetu, lakini hawakuwa wa kwetu hasa. Kwa maana kama wangekuwa wa kwetu, wangekaa pamoja nasi; lakini kutoka kwao kulionesha kwamba hakuna hata mmoja wao aliyekuwa wa kwetu. Lakini ninyi mmepakwa mafuta na yeye Aliye Mtakatifu, nanyi nyote mnaijua kweli. Siwaandikii kwa sababu hamuijui kweli, bali kwa sababu mnaijua, nanyi mnajua hakuna uongo unaotoka katika kweli. Je, mwongo ni nani? Mwongo ni mtu yule asemaye kwamba Isa si Al-Masihi. Mtu kama huyo ndiye anayempinga Al-Masihi, yaani yeye humkana Baba na Mwana. Hakuna yeyote amkanaye Mwana aliye na Baba. Yeyote anayemkubali Mwana anaye na Baba pia. Bali ninyi, hakikisheni kwamba lile mlilosikia tangu mwanzo linadumu ndani yenu. Kama lile mlilosikia tangu mwanzo linakaa ndani yenu, ninyi nanyi mtakaa ndani ya Mwana na ndani ya Baba. Hii ndiyo ahadi yake kwetu, yaani uzima wa milele. Nawaandikia mambo haya kuhusu wale watu ambao wanajaribu kuwapotosha. Bali ninyi, upako mlioupata kutoka kwake unadumu ndani yenu, wala ninyi hamna haja ya mtu yeyote kuwafundisha. Lakini kama vile upako wake unavyowafundisha kuhusu mambo yote nayo ni kweli wala si uongo, basi kama ulivyowafundisha kaeni ndani yake.