1 Wakorintho 14:2-15
1 Wakorintho 14:2-15 NEN
Kwa maana mtu yeyote anayesema kwa lugha, hasemi na wanadamu bali anasema na Mungu. Kwa kuwa hakuna mtu yeyote anayemwelewa, kwani anasema mambo ya siri kwa roho. Lakini anayetoa unabii anasema na watu akiwajenga, kuwatia moyo na kuwafariji. Anenaye kwa lugha hujijenga mwenyewe, bali atoaye unabii hulijenga kanisa. Ningependa kila mmoja wenu anene kwa lugha lakini ningependa zaidi nyote mtoe unabii. Kwa kuwa yeye atoaye unabii ni mkuu kuliko anenaye kwa lugha, isipokuwa atafsiri, ili kanisa lipate kujengwa. Sasa ndugu zangu, kama nikija kwenu nikasema kwa lugha mpya nitawafaidia nini kama sikuwaletea ufunuo au neno la maarifa au unabii au mafundisho? Hata vitu visivyo na uhai vitoapo sauti, kama vile filimbi au kinubi, mtu atajuaje ni wimbo gani unaoimbwa kusipokuwa na tofauti ya upigaji? Tena kama tarumbeta haitoi sauti inayoeleweka, ni nani atakayejiandaa kwa ajili ya vita? Vivyo hivyo na ninyi, kama mkinena maneno yasiyoeleweka katika akili, mtu atajuaje mnalosema? Kwa maana mtakuwa mnasema hewani tu. Bila shaka ziko sauti nyingi ulimwenguni, wala hakuna isiyo na maana. Basi kama sielewi maana ya hiyo sauti, nitakuwa mgeni kwa yule msemaji, naye atakuwa mgeni kwangu. Vivyo hivyo na ninyi. Kwa kuwa mnatamani kuwa na karama za rohoni, jitahidini kuzidi sana katika karama kwa ajili ya kulijenga kanisa. Kwa sababu hii, yeye anenaye kwa lugha na aombe kwamba apate kutafsiri kile anachonena. Kwa maana nikiomba kwa lugha, roho yangu inaomba, lakini akili yangu haina matunda. Nifanyeje basi? Nitaomba kwa roho, na pia nitaomba kwa akili yangu. Nitaimba kwa roho na nitaimba kwa akili yangu pia.