1 Nyakati 21:14-30
1 Nyakati 21:14-30 NENO
Basi Mwenyezi Mungu akatuma tauni katika Israeli, na wanaume elfu sabini wa Israeli wakafa. Mungu akapeleka malaika kuangamiza Yerusalemu. Lakini malaika alipokuwa akifanya hivyo, Mwenyezi Mungu akaona na akahuzunika kwa sababu ya maafa, akamwambia yule malaika aliyekuwa anaangamiza watu, “Yatosha! Rudisha mkono wako.” Wakati huo malaika wa Mwenyezi Mungu alikuwa amesimama katika sakafu ya kupuria nafaka ya Arauna Myebusi. Daudi akayainua macho yake, akamwona huyo malaika wa Mwenyezi Mungu akiwa amesimama katikati ya mbingu na dunia, naye ameunyoosha upanga wake juu ya Yerusalemu tayari kuangamiza. Kisha Daudi na wazee, waliokuwa wamevaa gunia, wakaanguka kifudifudi. Daudi akamwambia Mungu, “Je, si mimi ndiye niliyeamuru watu wahesabiwe? Mimi ndiye niliyetenda dhambi na kukosa. Hawa ni kondoo tu. Wamefanya nini? Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, mkono wako na uwe juu yangu na jamaa yangu, lakini usiache tauni hii iendelee juu ya watu wako.” Kisha malaika wa Mwenyezi Mungu akamwamuru Gadi amwambie Daudi apande na kumjengea Mwenyezi Mungu madhabahu kwenye sakafu ya kupuria nafaka ya Arauna Myebusi. Kwa hiyo Daudi akakwea, akalitii lile neno ambalo Gadi alikuwa amelisema katika jina la Mwenyezi Mungu. Arauna alipokuwa akipura ngano, akageuka, akamwona yule malaika. Wanawe wanne waliokuwa pamoja naye wakajificha. Kisha Daudi akakaribia, Arauna alipotazama na kumwona, akaondoka kwenye uwanja wa kupuria nafaka akamsujudia Daudi, uso wake ukagusa chini. Daudi akamwambia Arauna, “Nipatie huu uwanja wako wa kupuria nafaka, niweze kujenga madhabahu ya Mwenyezi Mungu, ili tauni ipate kukomeshwa katika watu. Niuzie kwa bei yake kamili.” Arauna akamwambia Daudi, “Uchukue huo uwanja. Mfalme bwana wangu na afanye lolote analopenda. Tazama, nitatoa maksai kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, vifaa vya kupuria kuwa kuni, pamoja na ngano kwa ajili ya dhabihu ya nafaka. Natoa hivi vyote.” Lakini Mfalme Daudi akamjibu Arauna, “La hasha! Lakini ninasisitiza kwamba nitalipa bei yake kamili. Sitachukua kilicho chako kwa ajili ya Mwenyezi Mungu au kutoa sadaka ya kuteketezwa isiyonigharimu chochote.” Basi Daudi akamlipa Arauna shekeli mia sita za dhahabu kwa ajili ya ule uwanja. Kisha Daudi akamjengea Mwenyezi Mungu madhabahu mahali hapo, na kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Akamwita Mwenyezi Mungu naye Mwenyezi Mungu akajibu maombi yake kwa moto kutoka mbinguni juu ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa. Kisha Mwenyezi Mungu akanena na yule malaika, naye akarudisha upanga wake katika ala yake. Wakati huo, Daudi alipoona kwamba Mwenyezi Mungu amemjibu kule kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Arauna Myebusi, akatoa dhabihu huko. Maskani ya Mwenyezi Mungu ambayo Musa aliitengeneza kule jangwani, pamoja na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, kwa wakati huo vilikuwa viko mahali pa juu pa kuabudia huko Gibeoni. Lakini Daudi hakuthubutu kuisogelea ili kumuuliza Mungu, kwa sababu aliuogopa upanga wa yule malaika wa Mwenyezi Mungu.