1 Nyakati 15:1-16
1 Nyakati 15:1-16 NENO
Baada ya Daudi kujijengea nyumba zake katika Mji wa Daudi, akatengeneza sehemu kwa ajili ya Sanduku la Mungu, na akasimamisha hema kwa ajili yake. Kisha Daudi akasema, “Hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kulibeba Sanduku la Mungu isipokuwa Walawi peke yao, kwa sababu Mwenyezi Mungu aliwachagua kulibeba Sanduku la Mwenyezi Mungu na kuhudumu mbele zake milele.” Daudi akawakusanya Israeli wote huko Yerusalemu ili kulipandisha Sanduku la Mwenyezi Mungu na kulileta hadi kwenye sehemu aliyokuwa ametengeneza kwa ajili yake. Kisha Daudi akawakusanya wazao wa Haruni na Walawi: Kutoka wazao wa Kohathi, Urieli kiongozi na ndugu zake mia moja na ishirini. Kutoka wazao wa Merari, Asaya kiongozi na ndugu zake mia mbili na ishirini. Kutoka wazao wa Gershoni, Yoeli kiongozi na ndugu zake mia moja na thelathini. Kutoka wazao wa Elisafani, Shemaya kiongozi na ndugu zake mia mbili. Kutoka wazao wa Hebroni, Elieli kiongozi na ndugu zake themanini. Kutoka wazao wa Uzieli, Aminadabu kiongozi na ndugu zake mia moja na kumi na wawili (112). Kisha Daudi akawaita makuhani Sadoki na Abiathari, pamoja na Walawi Urieli, Asaya, Yoeli, Shemaya, Elieli na Aminadabu. Akawaambia, “Ninyi ndio viongozi wa jamaa za Walawi. Ninyi pamoja na Walawi wenzenu inawapasa mjitakase na kulipandisha Sanduku la Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, hadi mahali pale nimetengeneza kwa ajili yake. Ilikuwa ni kwa sababu hii, ninyi Walawi, hamkulipandisha Sanduku la Mwenyezi Mungu mara ya kwanza, hata ikasababisha Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, kuwaka hasira dhidi yetu. Hatukumuuliza jinsi ya kufanya ili tupate kulileta jinsi alivyoagiza.” Kwa hiyo makuhani pamoja na Walawi wakajitakasa ili kulipandisha Sanduku la Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli. Nao Walawi wakalichukua Sanduku la Mungu mabegani mwao wakitumia mipiko, kama vile Musa alivyoamuru sawasawa na neno la Mwenyezi Mungu. Daudi akawaambia viongozi wa Walawi wawateue ndugu zao waimbaji ili waimbe nyimbo za shangwe, wakiwa na vyombo vya uimbaji: zeze, vinubi na matoazi.