Nilitazama, nikaona dhoruba kubwa ikitoka kaskazini: wingu kubwa sana likiwa na miali ya radi, likizungukwa na mwanga mkali. Katikati ya huo moto kulikuwa kama chuma inavyong’aa ndani ya moto. Ndani ya ule moto kulikuwa na mfano wa viumbe wanne wenye uhai. Kuonekana kwao walikuwa na umbo la mwanadamu, lakini kila mmoja alikuwa na nyuso nne na mabawa manne. Miguu yao ilikuwa imenyooka; nyayo za miguu yao zilikuwa kama kwato za miguu ya ndama, nazo zilimetameta kama shaba iliyosuguliwa. Chini ya mabawa yao katika pande zao nne walikuwa na mikono ya mwanadamu. Wote wanne walikuwa na nyuso na mabawa, nayo mabawa yao yaligusana. Kila mmoja alienda kuelekea mbele moja kwa moja; hawakugeuka walipotembea.