Mwanzo 1
1
Kuumbwa ulimwengu#1:1—2:4 Simulizi hili la kuumbwa ulimwengu lina umoja kamili wa kimaandishi. Aya za kwanza na za mwisho zinaliweka simulizi lote katika fremu ya jumla ambayo kila fungu la maneno lina mahali na maana yake katika simulizi lote: Kianzio (1:1) kinalingana na kimalizio (2:1). Tendo la kuumba linafanyika kwa “amri” au kutaka kwake Mungu likifuatiwa na tamko kwamba amri hiyo ilikamilika (1:3,6-7,14-15; rejea pia aya 30 n.k). Na Mungu anasemwa kwamba hatua zote aliziona kuwa njema (1:4,10,12,18,21,25; rejea aya 31). Mwa 1:2 inaonesha hali ilivyokuwa au mazingira ya mwanzo ya kuumbwa ulimwengu na inalingana na 2:2-3 ambamo Mwenyezi-Mungu anapumzika baada ya kumaliza kazi. Ndani ya fremu hii ni simulizi la kuumbwa ulimwengu kwa siku sita nalo limegawanywa katika sehemu mbili. Sehemu ya kwanza (1:3-10) Mwenyezi-Mungu anaumba vitu vya kimsingi vya ulimwengu wetu: anaumba wakati (1:3-5) na nafasi (1:6-10). Nafasi hiyo imewekewa mpaka wa wima: chini juu (aya 6-8) na mpaka wa usawa wa nchi (aya 9-10). Katika sehemu ya pili (1:11-31) Mwenyezi-Mungu anaumba pia katika ulimwengu huo ulio sasa na muundo, viumbe hai na mazingira ambayo yatavitegemeza. Kwanza mimea inaumbwa (1:11-13). Kisha jua na mwezi kama vyenye kusimamia mchana na usiku na pia kuongoza maisha na nyakati (1:14-19). Na tatu wanyama wanaumbwa (1:20-25) na mwishowe binadamu (1:26-28). Katika 1:31 Mungu anaona kila kitu alichofanya kuwa ni chema kabisa.
1Hapo mwanzo,#1:1 Hapo mwanzo: Maneno haya yanaweza kutafsiriwa pamoja na mtendaji, yaani Mungu, na kitendewa, yaani mbingu na dunia, kama: “Hapo mwanzo, Mungu alipoumba mbingu na dunia …” Mungu aliumba#1:1 Aliumba: Kiebrania “bara”. Katika A.K. neno hili ambalo ni kitenzi, Mungu ndiye mtendaji daima, na yahusu kitendo cha Kimungu ambacho daima matokeo yake ni kitu kipya na cha kuvutia. Neno lenyewe hutumika kusema juu ya kuumbwa kwa ulimwengu na binadamu (Mwa 1:27,51; Kumb 4:32; Isa 45:12), kuundwa kwa watu wa Israeli (Isa 43:1,15), kurekebishwa kwa Yerusalemu (Isa 65:18), urekebishwaji wa ndani wa mtu mwenye dhambi anayetubu na kusamehewa dhambi (Zab 51:10) na kuumbwa kutakakofanyika mwishoni mwa nyakati ambapo kutakuwa na mbingu mpya na nchi mpya (Isa 65:17; 66:22). mbingu na dunia.#1:1 Mbingu na dunia: Waebrania wa kale hawakuwa na neno moja ambalo lilitaja “ulimwengu”; badala yake kulikuwa na mtindo wa kuweza kutaja kitu kwa jumla yake yote kwa kutumia sehemu zake muhimu, k.m. “mbingu na dunia” yaani, ulimwengu. Rejea pia Mwa 14:22; Zab 124:8; Mat 28:18. 2Dunia ilikuwa bila umbo na tupu. Giza lilikuwa limefunika vilindi vya maji#1:2 Giza lilikuwa limefunika vilindi vya maji: Kulingana na fikira za watu wa kale huko Mashariki ya Kati, kabla ya kuumbwa ulimwengu kulikuwa na giza kila mahali na kitu kama maji yenye kutisha (Zab 104:6-9). Kwa hiyo, moja ya kitendo cha kwanza cha Muumba ni kutenganisha maji ya juu na ya chini, na hivyo kuweka kitu kama mstari wa kugawanya kile tunachokiona kama anga (aya 7). Taz Zab 18:15. Rejea pia Zab 24:2. na roho ya Mungu#1:2 Roho ya Mungu: Neno “roho” linatafsiri neno la Kiebrania “ruah”. Neno hilo la Kiebrania laweza pia kuwa na maana ya “upepo”, “pumzi”. Tena, maneno “ya Mungu” (“mungu” Kiebrania ni “elohim”) mara nyingine kama vile katika Mwa 23:6; 1Sam 14:15 na Yobu 1:16, hutumika kuelezea ukubwa. Kwa hiyo, wafafanuzi wengine wanafikiri maneno “roho ya Mungu ilikuwa ikitanda juu ya maji” yana maana ya “upepo mkubwa ulitanda juu ya maji”. ilikuwa ikitanda juu ya maji.
3Mungu akasema,#1:3 Mungu akasema: Maneno haya ambayo yanafungamana na kukamilika kwa yale aliyosema Mungu, yaani “ikawa hivyo” (aya 7,9,11, n.k.), yanatilia mkazo uwezo na nguvu kuu ya Mungu na neno lake. Amri ya Mungu inatekelezwa mara moja na tukio linalofuata amri yake ni la namna iliyo sawa kabisa na jinsi alivyotamka Mungu (rejea Zab 33:6-9; 148:5; Isa 48:13; 55:10-11; Ebr 11:3). “Mwanga uwe”, mwanga ukawa. 4Mungu akauona mwanga kuwa ni mwema. Kisha Mungu akautenganisha mwanga na giza,#1:4 Simulizi hili la kuumbwa ulimwengu linasisitiza na kutilia mkazo kwamba kazi aliyoifanya Mungu Muumba ni njema (aya 4,10,12,18,21,25,31). Hapa inasisitizwa kwamba kila kilichoumbwa ni “chema” kwa sababu kimetoka kwa Mungu na ni sawa na matakwa yake. Wazo hili ni tofauti kabisa na mawazo ya watu wasiomjua Mungu wa kweli ambao walifikiri kwamba vitu vilivyoumbwa viliumbwa kutokana na ujeuri wa miungu na kwamba ulimwengu upo bila mpango au malengo maalumu, tena ni mabaya. 5mwanga akauita “Mchana” na giza akaliita “Usiku.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi;#1:5 Ikawa jioni, ikawa asubuhi: Neno kwa neno “kutwa, kucha”. Msemo huu unamaanisha kwamba siku moja ilikamilika. Taz Zab 104:19. siku ya kwanza.
6Mungu akasema, “Anga#1:6-8 Anga: Neno la Kiebrania lililotafsiriwa hapa kwa “anga” lina maana ya kitu kilichotandazwa kama bati. Kwa hiyo wazo la ulimwengu kwa watu wa kale lilikuwa la sehemu tatu: Mbingu, Dunia na chini ya dunia. “Dunia” au nchi ilifikiriwa kuwa NA sura au uso ulio sawasawa; Mbingu ilifikiriwa kuwa kama kitu kilicho kama bati kilichotanda (anga) taz Yobu 37:18, juu ya anga hilo kulikuwa na hazina kuu ya maji au bahari ya juu ambamo hutoka mvua (rejea Mwa 7:11; Zab 148:4; Isa 40:22); Chini ya dunia (nchi) kulikuwa na bahari kuu ambamo kulitokea chemchemi zilizolowanisha nchi (taz Mwa 1:2; Zab 104:5-6; 136:6). liwe katikati ya maji, liyatenge maji sehemu mbili.” 7Mungu akalifanya anga, akayatenga maji yaliyo juu ya anga na yale yaliyo chini ya anga hilo. Ikawa hivyo. 8Mungu akaliita anga “Mbingu.” Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya pili.
9Mungu akasema, “Maji yaliyo chini ya mbingu na yakusanyike mahali pamoja, nchi kavu itokee.” Ikawa hivyo. 10Mungu akapaita mahali pakavu “Nchi” na kusanyiko la maji akaliita “Bahari.” Mungu akaona kuwa ni vyema.
11Kisha Mungu akasema, “Nchi na ioteshe#1:11 Nchi na ioteshe: Kadiri ya simulizi hili, Mungu anajalia baadhi ya viumbe kipaji cha rutuba ambayo kwayo vinaendelea na kukamilisha kazi ya Muumba. Na, kulingana na A.K. kuwa na rutuba ni baraka inayotoka kwa Mungu mwenyewe. Taz Mwa 1:28 maelezo. mimea: mimea izaayo mbegu, na miti izaayo matunda yenye mbegu.” Ikawa hivyo. 12Basi, nchi ikaotesha mimea izaayo mbegu kwa jinsi yake, na miti izaayo matunda yenye mbegu kwa jinsi yake. Mungu akaona kuwa ni vyema. 13Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya tatu.
14Mungu akasema, “Mianga na iweko angani, itenge mchana na usiku, ioneshe nyakati, majira, siku na miaka,#1:14 Ioneshe nyakati, majira, siku na miaka: Hapa yahusu hasa majira au nyakati za kidini zilizohusika. Rejea Zab 81:3. 15na ing'ae angani na kuiangazia dunia.” Ikawa hivyo. 16Basi, Mungu akafanya mianga miwili mikubwa; ule mkubwa utawale mchana na ule mdogo utawale usiku; akafanya na nyota pia.#1:14-18 Mungu akafanya mianga miwili mikubwa …na nyota pia: Katika dini za Mashariki ya Kati ya Kale sayari na nyota ziliabudiwa kama miungu. Hapa zinawekwa kama viumbe vyenye kumtumikia Mungu na wala sio kama nguvu za pekee zilizofichika wala vitu vya kuabudiwa (rejea Kumb 4:19). Rejea pia Zab 8:3; Yer 31:35. 17Mungu akaiweka mianga hiyo angani iiangazie dunia, 18ipate kutawala mchana na usiku, na kuutenga mwanga na giza. Mungu akaona kuwa ni vyema. 19Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya nne.
20Mungu akasema, “Maji na yatoe makundi ya viumbe hai na ndege waruke angani.” 21Basi, Mungu akaumba wanyama wakubwa sana wa baharini#1:21 Wanyama wakubwa sana wa baharini: Hawa wanatajwa ili kuonesha kwamba hata wao walikuwa wameumbwa na Mungu na wamo chini ya uwezo wake. Hapa inadhihirika kabisa mojawapo ya tofauti za kimsingi kati ya simulizi la Biblia na simulizi moja maarufu la hadithi za Babuloni. Kulingana na hadithi za Babuloni kuumbwa kwa ulimwengu kulitanguliwa na kutokea kwa miungu mbalimbali na ushindi wa mungu Marduki ambaye alimshinda mnyama mkubwa sana wa baharini. Jamii nyingi hata za Kiafrika zina hadithi zao kuhusu chimbuko la ulimwengu lakini hadithi hizo zote ni tofauti sana na simulizi la Biblia ambapo kila kitu kumeumbwa na Mwenyezi-Mungu ambaye ndiye peke yake Mungu na vyote viko chini ya maongozi yake. na aina zote za viumbe vyote hai viendavyo na kujaa majini; akaumba na aina zote za ndege wote. Mungu akaona kuwa ni vyema. 22Mungu akavibariki, akasema, “Zaeni, muongezeke, muyajaze maji ya bahari; nao ndege waongezeke katika nchi.” 23Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya tano.
24Mungu akasema, “Nchi na itoe aina zote za viumbe hai, wanyama wa kufugwa, viumbe vitambaavyo na wanyama wa porini wa kila aina.” Ikawa hivyo. 25Basi, Mungu akafanya aina zote za wanyama wa porini, wanyama wa kufugwa, na viumbe vitambaavyo. Mungu akaona kuwa ni vyema.
26Kisha Mungu akasema, “Tumfanye mtu kwa mfano wetu,#1:26 Kwa mfano wetu: Huu wingi unaotumika hapa na ambao umetamkwa na Mungu aliye peke yake Mungu umewahi kufafanuliwa kwa namna mbalimbali. Lakini miongoni mwa fafanuzi zote, inaonekana kwamba hapa, kwa namna ya pekee kabisa, maneno hayo ya wingi yanaashiria makusudi na maamuzi ya pekee ya Mungu Muumba katika wakati wa kumuumba binadamu. Kati ya kazi zote za Mungu ni kazi hii ya kuumba binadamu ndio peke yake inayotanguliwa na matumizi ya wingi na yana kusudi rasmi la Mungu la kutenda kitu hicho. Ingawa wasomaji wataharakisha kuona hapa uwezekano wa kutaja nafsi tatu za Mungu, ni lazima kukumbuka kwamba fundisho kuhusu nafsi tatu za Mungu ni fundisho lililokamilishwa katika A.J. na kwamba habari hiyo mpya juu ya Uungu haikujulikana moja kwa moja kwa waandishi wa A.K. kwa sura yetu; atawale samaki wa baharini, ndege wa angani, wanyama wa kufugwa, dunia yote na viumbe vyote vitambaavyo.” 27Basi, Mungu akaumba mtu#1:27 Mtu: Kiebrania ni “adam” na hapa yahusu binadamu. Katika sehemu nyingine neno hili linatumika kama jina, yaani “Adamu” (rejea Mwa 4:25). kwa mfano wake; naam, kwa mfano wake Mungu alimuumba.#1:27 Kwa mfano wake; naam, kwa mfano wake Mungu alimuumba: Binadamu sio tu viumbe vya pekee vya Mungu (taz Mwa 2:7 maelezo) ila wamepewa hali ambayo inawawezesha kuwa katika uhusiano wa kibinafsi na Mungu na kuweza kutekeleza, kama wawakilishi wake, utawala juu ya ulimwengu aliouumba Mungu (taz aya 28). Rejea Mwa 5:1; 9:6; 1Kor 11:7; Yak 3:9. Aliwaumba mwanamume na mwanamke.#1:27 Mwanamume na mwanamke: Maneno haya katika makala hii yanaonesha dhahiri kwamba hali ya uhusiano wa kijinsia kati ya ya mume na mke ni hali iliyowekwa kwa matakwa ya Mungu. Rejea Mat 19:4; Marko 10:6. 28Mungu akawabariki na kuwaambia, “Zaeni muongezeke, mkaijaze nchi na kuimiliki; muwatawale samaki wa baharini, ndege wa angani, na kila kiumbe hai kitembeacho duniani.”#1:28 Katika A.K. baraka za Mungu, mara nyingi, zinaonekana kuhusikana zaidi na rutuba. Rejea Mwa 17:16,20; 22:17; 28:12,24; 28:3. Taz pia Mwa 49:22,26; Zab 128.
29Kisha Mungu akasema, “Tazama, nawapeni kila mmea duniani uzaao mbegu, na kila mti uzaao matunda yenye mbegu; mbegu zao au matunda yao yatakuwa chakula chenu. 30Nao wanyama wote duniani, ndege wote wa angani, viumbe vyote vitambaavyo, naam, kila kiumbe chenye uhai, chakula chao kitakuwa majani yote ya mimea.” Ikawa hivyo. 31Mungu akaona kila kitu alichokifanya kuwa ni chema kabisa. Ikawa jioni, ikawa asubuhi; siku ya sita.
Currently Selected:
Mwanzo 1: BHNTLK
Označeno
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993
The Bible Society of Kenya 1993