Mattayo MT. 27
27
1ILIPOKUWA assubuhi, makuhani wakuu wote na wazee wa watu wakafanya shauri juu ya Yesu, wapate kumfisha; 2wakamfunga, wakamchukua, wakampeleka kwa liwali Pontio Pilato.
3Ndipo Yuda, yule mwenye kumsaliti, alipoona ya kuwa amekwisha kuhukumiwa, akajuta, akawarudishia makuhani wakuu na wazee vile vipande thelathini vya fedha, 4akinena, Nalikosa nilipoisaliti damu isiyo na khatiya. Wakanena, Bassi, haya yatukhussu nini sisi? Tazama wewe hayo. 5Akavitupa vile vipande vya fedha katika patakatifu, akaondoka; akaenda, akajinyonga. 6Makuhani wakuu wakavitwaa vile vipande vya fedha, wakasema, Ni haramu kuviweka katika sanduku ya sadaka, kwa kuwa ni kima cha damu. 7Wakafanya shauri, wakavitumia kwa kununua konde la mfinyangi liwe mahali pa kuzikia wageni. 8Kwa hiyo konde lile linakwitwa konde la damu, hatta leo. 9Ndipo likatimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, akisema, Wakavitwaa vipande thelathini vya fedha, kima chake aliyetiwa kima, ambae watu miongoni mwa wana wa Israeli walimtia kima; 10wakavitumia kwa kununua konde la mfinyangi, kama Bwana alivyoniagiza.
11Yesu akasimama mbele ya liwali: liwali akamwuliza, akinena, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Yesu akamwambia, Wewe wanena. 12Aliposhitakiwa na makuhani wakuu na wazee, hakujibu hatta neno. 13Ndipo Pilato akamwambia, Husikii mambo mangapi wanayokushuhudia? 14Nae hakumjibu hatta kwa neno moja, hatta liwali akataajabu sana. 15Bassi wakati wa siku kuu liwali desturi yake huwafungulia makutano mfungwa mmoja waliyemtaka. 16Bassi walikuwa na mfungwa mashuhuri siku zile, jina lake Barabba. 17Bassi walipokutanika, Pilato akawaambia, Mnataka niwafungulie nani? Barabba, au Yesu aitwae Kristo? 18Kwa maana alijua ya kuwa wamemtoa kwa husuda. 19Na alipokuwa ameketi juu ya kiti cha hukumu, mkewe alimpelekea mjumbe, kumwambia, Usiwe na neno na yule mwenye haki: kwa sababu nimeteswa mengi leo katika udoto kwa ajili yake. 20Nao makuhani wakuu na wazee wakawashawishi makutano illi wamtake Barabba, na kumwangamiza Yesu. 21Lakini liwali akajibu, akawaambia, Mnataka niwafungulie nani katika hawo wawili? Wakasema, Barabba. 22Pilato akawaambia, Bassi, nimtendeni Yesu aitwae Kristo? Wakanena wote, Asulibiwe. 23Liwali akasema, Kwani? ubaya gani alioutenda? Wakazidi sana kupiga kelele, wakinena, Asulibiwe. 24Pilato alipoona ya kuwa hafai neno, bali ya kuwa inazidi kuwa ghasia, akatwaa maji, akanawa mikono yake mbele ya makutano, akasema, Mimi sina khatiya kwa khabari ya damu ya mtu huyu mwenye haki: tazameni hayo ninyi wenyewe. 25Watu wote wakajibu wakasema, Damu yake na iwe juu yetu, na juu ya watoto wetu. 26Ndipo akawafungulia Barabba: na alipokwisha kumpiga Yesu mijeledi, akamtoa apate kusulibiwa.
27Ndipo askari wa liwali wakamchukua Yesu ndani ya praitorio, wakamkusanyia kikosi kizima. 28Wakamvua nguo, wakamvika vazi jekundu. 29Wakasokota taji ya miiba, wakaiweka juu ya kichwa chake, na unyasi katika mkono wake wa kuume; wakapiga magoti mbele yake, wakamfanyizia dhihaka, wakinena, Salamu, Mfalme wa Wayahudi! 30Wakamtemea mate, wakautwaa ule unyasi, wakampiga kichwa. 31Walipokwisha kumfanyia dhihaka, wakalivua lile vazi, wakamvika nguo zake, wakamchukua kumsulibi.
32Hatta walipokuwa wakitoka humo, wakakutana na mtu Mkurene, jina lake Simon; huyu wakamtumikisha auchukue msalaba wake. 33Walipofika mahali paitwapo Golgotha, maana yake, Mahali pa kichwa, 34wakampa kunywa siki iliyochanganyika na safura; nae alipoonja hakutaka kunywa. 35Walipokwisha kumsulibi, wakagawa nguo zake, wakipiga kura: illi litimie neno lililonenwa na nabii. Waligawa nguo zangu kati yao, na juu ya vazi langu walipiga kura. 36Wakaketi, wakamwangalia huko. 37Wakaweka juu ya kichwa chake mshitaka wake, ulioandikwa, HUYU NI YESU, MFALME WA WAYAHUDI. 38Ndipo wanyangʼanyi wawili wakasulibiwa pamoja nae, mmoja mkono wake wa kuume, na mmoja mkono wake wa kushoto. 39Nao waliokuwa wakipita njiani wakamtukana, wakitikisatikisa vichwa vyao, 40wakinena, Ewe ulivunjae hekalu na kuijenga kwa siku tatu, jiponye nafsi yako; ukiwa Mwana wa Mungu, shuka msalahani. 41Kadhalika ua wale makuhani wakuu wakimdhihaki pamoja na waandishi na wazee, wakinena, 42Aliponya watu wengine, hawezi kujiponya nafsi yake. Akiwa mfalme wa Israeli, na ashuke sasa msalabani, naswi tutamwamini. 43Amemtegemea Mungu; na amwokoe sasa, kamii akimtaka; kwa maana alisema, Mimi ni Mwana wa Mungu. 44Vilevile wa ayangʼanyi nao waliosulibiwa pamoja nae walimshutumu.
45Tangu saa sita palikuwa giza juu ya inchi yote hatta saa tissa. 46Na kama saa tissa, Yesu akapaaza sauti yake kwa nguvu akinena, Eli, Eli, lama sabakhthani? maana yake, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? 47Baadhi yao waliosimama huko, waliposikia, wakanena, Huyu anamwita Elia. 48Marra mmoja wao akaenda mbio, akatwaa sifongo, akaijaza siki, akaitia juu ya unyasi, akamnywesha. 49Wale wengine walinena, Acha; na tuone kwamba Elia anakuja kumponya. 50Nae Yesu akiisha kupaaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake. 51Na tazama pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hatta chini: inchi ikatetema; miamba ikapasuka; 52makaburi yakafunuka; ikafufuka miili mingi ya watakatifu waliolala; 53nao wakiisha kutoka makaburini, baada ya kufufuka kwake, wakaingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi. 54Bassi yule akida, nao walio pamoja nae wakimwangalia Yesu, walipoliona tetemeko la inchi na mambo yaliyofanyika, wakaogopa sana, wakinena, Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu. 55Na palikuwa na wanawake wengi huko wakitazama kwa mbali, hawo ndio waliomfuata Yesu toka Galilaya, na kumtumikia. 56Miongoni mwao alikuwamo Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo na Yose, na mama yao wana wa Zebedayo.
57Ilipokuwa jioni akafika mtu tajiri wa Arimathaya, jina lake Yusuf, nae mwenyewe alikuwa mwanafunzi wa Yesu; 58mtu huyu alimwendea Pilato, akauomba mwili wa Yesu. Pilato akaamuru apewe mwili wake. 59Yusuf akautwaa mwili, akauzinga katika kitambaa cha kitani safi, 60akanweka katika kaburi lake jipya, alilolikata mwambani; akafingirisha jiwe kubwa hatta mlango wa kaburi, akaenda zake. 61Walikuwako hapo Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili, wameketi kulielekea kaburi.
62Hatta siku ya pili, ndiyo iliyo baada ya Maandalio, makuhani wakuu na Mafarisayo wakamkusanyikia Pilato, 63wakinena, Bwana, tumekumbuka kwamba yule mjanja alisema, alipokuwa hayi bado, Baada ya siku tatu nitafufuka. 64Bassi amuru kaburi lilindwe sana hatta siku ya tatu; wasije wanafunzi wake usiku wakamwiba, wakawaambia watu, Amefufuka katika wafu: na kosa la mwisho litapita lile la kwanza. 65Pilato akawaambia, Mna askari: enendeni kalilindeni sana kadiri mjuavyo. 66Wakenda zao, wakalilinda sana kaburi, wakilitia lile jiwe muhuri, pamoja na wale askari walinzi.
Aktuálne označené:
Mattayo MT. 27: SWZZB1921
Zvýraznenie
Zdieľať
Kopírovať
Chceš mať svoje zvýraznenia uložené vo všetkých zariadeniach? Zaregistruj sa alebo sa prihlás
Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.