YouVersion Logo
Search Icon

Mwanzo 13

13
Abramu na Lutu watengana
1Hivyo Abramu akakwea kutoka Misri kwenda Negebu, na mkewe na kila kitu alichokuwa nacho; pia Lutu akaenda pamoja naye. 2Wakati huo Abramu alikuwa tajiri sana wa mifugo, fedha na dhahabu.
3Kutoka Negebu, akasafiri sehemu mbalimbali hadi akafika Betheli, mahali ambapo mwanzoni alipiga hema lake kati ya Betheli na Ai, 4pale alipokuwa amejenga madhabahu ya kwanza. Huko Abramu akaliitia jina la Mwenyezi Mungu.
5Basi Lutu, aliyekuwa anafuatana na Abramu, alikuwa pia na mifugo na mahema. 6Lakini nchi haikuwatosha kukaa pamoja kwa ajili ya wingi wa mali yao. 7Ukazuka ugomvi kati ya wafugaji wa wanyama wa Abramu na wale wa Lutu. Wakati huo, Wakanaani na Waperizi pia waliishi katika nchi hiyo.
8Hivyo Abramu akamwambia Lutu, “Pasiwe na ugomvi wowote kati yangu na wewe, wala kati ya wachungaji wangu na wako, kwa kuwa sisi ni ndugu. 9Je, nchi yote haiko mbele yako? Tutengane. Ukielekea kushoto, nitaenda kulia; ukielekea kulia, mimi nitaenda kushoto.”
10Lutu akatazama, akaona lile bonde lote la Yordani kuwa lilikuwa na maji tele, kama bustani ya Mwenyezi Mungu, kama nchi ya Misri, kuelekea Soari. (Hii ilikuwa kabla Mwenyezi Mungu hajaharibu Sodoma na Gomora.) 11Hivyo Lutu akajichagulia bonde lote la Yordani, akaelekea upande wa mashariki. Watu hao wawili wakatengana. 12Abramu aliishi nchi ya Kanaani, naye Lutu akaishi miongoni mwa miji ya lile bonde na kupiga mahema yake karibu na Sodoma. 13Basi watu wa Sodoma walikuwa waovu, wakitenda dhambi nyingi dhidi ya Mwenyezi Mungu.
14Baada ya Lutu kuondoka, Mwenyezi Mungu akamwambia Abramu, “Ukiwa hapo ulipo, inua macho yako utazame kaskazini na kusini, mashariki na magharibi. 15Nchi yote unayoiona nitakupa wewe na uzao wako hata milele. 16Nitaufanya uzao wako uwe mwingi kama mavumbi ya nchi, hivyo ikiwa kuna yeyote awezaye kuhesabu mavumbi, basi uzao wako utahesabika. 17Ondoka, tembea katika marefu na mapana ya nchi, kwa maana ninakupa wewe.”
18Basi Abramu akaondoa mahema yake, akaenda kuishi karibu na mialoni ya Mamre huko Hebroni. Naye akamjengea Mwenyezi Mungu madhabahu huko.

Currently Selected:

Mwanzo 13: ONMM

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in