Mathayo 7
7
Iweni Waangalifu Mnapokosoa Wengine
(Lk 6:37-38,41-42)
1Msiwahukumu wengine, ili Mungu asiwahukumu ninyi pia. 2Mtahukumiwa jinsi ile ile mnavyowahukumu wengine. Mungu atawatendea kama mnavyowatendea wengine.
3Kwa nini unaona vumbi iliyo katika jicho la rafiki yako, na hujali kipande cha mti kilicho katika jicho lako? 4Kwa nini unamwambia rafiki yako, ‘Ngoja nitoe vumbi lililo katika jicho lako wakati wewe mwenyewe bado una kipande cha mti katika jicho lako?’ 5Ewe mnafiki! Ondoa kwanza kipande cha mti katika jicho lako mwenyewe, ndipo utaweza kuona vizuri na kutoa vumbi katika jicho la rafiki yako.
6Msiwape mbwa kitu kitakatifu, watawageuka na kuwadhuru. Na msiwatupie nguruwe lulu zenu kwa kuwa watazikanyaga tu.
Mwombeni Mungu Kile Mnachohitaji
(Lk 11:9-13)
7Endeleeni kumwomba Mungu, naye atawapa, endeleeni kutafuta nanyi mtapata, endeleeni kubisha nanyi mtafunguliwa mlango. 8Ndiyo, yeyote anayeendelea kuomba atapokea. Yeyote anayeendelea kutafuta atapata. Na yeyote anayeendelea kubisha atafunguliwa mlango.
9Ni nani kati yenu aliye na mwana ambaye akimwomba mkate atampa jiwe? 10Au akimwomba samaki, atampa nyoka? Bila shaka hakuna! 11Ijapokuwa ninyi watu ni waovu, lakini bado mnajua kuwapa vitu vyema watoto wenu. Hakika Baba yenu wa mbinguni atawapa vitu vyema wale wamwombao.
Kanuni ya Muhimu Sana
12Watendee wengine kama ambavyo wewe ungetaka wao wakutendee. Hii ndiyo tafsiri ya torati#7:12 torati Au “Sheria ya Musa”. na mafundisho ya manabii.
Wachache tu Ndiyo Huiona Njia ya Uzima
(Lk 13:24)
13Unapaswa kuingia katika uzima wa kweli kupitia lango lililo jembamba. Kwa kuwa lango ni pana na njia inayoelekea katika uharibifu nayo ni pana na watu wengi wanaifuata njia hiyo. 14Lakini lango la kuelekea katika uzima wa kweli ni jembamba. Na njia iendayo huko ni ngumu kuifuata. Na ni watu wachache wanaoiona.
Kile Wanachokifanya watu Kinadhihirisha jinsi gani Walivyo
(Lk 6:43-44; 13:25-27)
15Mjihadhari na manabii wa uongo wanaokuja kwenu wakijifanya kondoo wasio na madhara ingawa ni watu hatari kama mbwa mwitu. 16Mtawatambua watu hawa kwa matendo yao. Mambo mazuri hayatoki kwa watu wabaya, kama ambavyo zabibu haitokani na miiba, na tini hazitokani na mbigiri. 17Vile vile, kila mti mzuri huzaa matunda mazuri na mti mbaya huzaa matunda mabaya. 18Mti mzuri hauwezi kuzaa matunda mabaya, na wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mazuri. 19Kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa kwenye moto. 20Mtawatambua manabii hawa wa uongo kwa matendo yao.
21Si kila aniitaye Bwana ataingia katika ufalme wa Mungu. Watakaoingia ni wale tu wafanyao yale ambayo Baba yangu wa mbinguni anataka. 22Siku ya mwisho wengi wataniiita Bwana. Watasema, ‘Bwana, kwa nguvu za jina lako tulihubiri. Na kwa nguvu za jina lako tulitoa mashetani na kufanya miujiza mingi.’ 23Ndipo nitawaambia waziwazi, ‘Ondokeni kwangu, ninyi waovu. Sikuwahi kuwajua.’
Aina Mbili za Watu
(Lk 6:47-49)
24Kila anayeyasikia mafundisho yangu na kuyatii ni kama mwenye hekima aliyejenga nyumba yake kwenye mwamba. 25Mvua kubwa iliponyesha na mafuriko yakaja, na upepo ukavuma sana, na kuipiga sana nyumba yake. Lakini, nyumba yake haikuanguka kwa sababu ilijengwa kwenye mwamba.
26Lakini kila anayeyasikia mafundisho yangu na asiyatii ni kama mjinga aliyejenga nyumba yake kwenye mchanga. 27Mvua kubwa iliponyesha na mafuriko kuja, na upepo ukavuma sana, nyumba yake ilianguka kwa kishindo kikuu.”
28Yesu alipomaliza kufundisha, watu walishangaa sana namna alivyokuwa akifundisha. 29Hakufundisha kama walimu wao wa sheria; alifundisha kwa mamlaka.#7:29 mamlaka Hakuhitaji mamlaka yoyote zaidi ya kwake. Kinyume chake waandishi daima waliwanukuu walimu wa kale wa Kiyahudi kama mamlaka ya mafundisho yao.
Selectat acum:
Mathayo 7: TKU
Evidențiere
Partajează
Copiază
Dorești să ai evidențierile salvate pe toate dispozitivele? Înscrie-te sau conectează-te
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International