Luka 22

22
Yuda Akubali Kumsaliti Isa
(Mathayo 26:14-16; Marko 14:10-11)
1 Wakati huu Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, iitwayo Pasaka, ilikuwa imekaribia. 2 Viongozi wa makuhani na walimu wa Torati walikuwa wanatafuta njia ya kumuua Isa, kwa sababu waliwaogopa watu. 3 Shetani akamwingia Yuda, aliyeitwa Iskariote, mmoja wa wale Kumi na Wawili. 4 Yuda akaenda kwa viongozi wa makuhani na kwa maafisa wa walinzi wa Hekalu, akazungumza nao jinsi ambavyo angeweza kumsaliti Isa. 5 Wakafurahi na wakakubaliana kumpa fedha. 6Naye akakubali, akaanza kutafuta wakati uliofaa wa kumsaliti Isa kwao, wakati ambapo hakuna umati wa watu.
Maandalizi Ya Pasaka
(Mathayo 26:17-25; Marko 14:12-21; Yohana 13:21-30)
7 Basi ikawadia siku ya Mikate Isiyotiwa Chachu, siku ambayo mwana-kondoo wa Pasaka huchinjwa. 8 Hivyo Isa akawatuma Petro na Yohana, akisema, “Nendeni mkatuandalie chakula cha Pasaka ili tuweze kuila.”
9Wakamuuliza, “Unataka tukuandalie wapi?”
10Isa akawaambia, “Tazameni, mtakapokuwa mkiingia mjini, mtakutana na mwanaume amebeba mtungi wa maji. Mfuateni mpaka kwenye nyumba atakayoingia. 11Nanyi mwambieni mwenye nyumba, ‘Mwalimu anauliza: Kiko wapi chumba cha wageni, ambamo mimi na wanafunzi wangu tutakula Pasaka?’ 12Atawaonyesha chumba kikubwa ghorofani, kikiwa kimepambwa vizuri. Andaeni humo.”
13 Wakaenda, nao wakakuta kila kitu kama Isa alivyowaambia. Hivyo wakaiandaa Pasaka.
Kuanzishwa Kwa Chakula Cha Bwana Isa
(Mathayo 26:31-35; Marko 14:27-31; Yohana 13:36-38)
14 Wakati ulipowadia, Isa akaketi mezani pamoja na wale mitume wake. 15 Kisha akawaambia, “Nimetamani sana kuila Pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu. 16 Kwa maana, nawaambia, sitaila tena Pasaka mpaka itakapotimizwa katika Ufalme wa Mwenyezi Mungu.”
17Akiisha kukichukua kikombe, akashukuru, akasema, “Chukueni hiki mnywe wote. 18 Kwa maana nawaambia tangu sasa sitakunywa tena katika uzao wa mzabibu, hadi Ufalme wa Mwenyezi Mungu utakapokuja.”
19 Kisha akachukua mkate, akashukuru, akaumega, na kuwapa, akisema, “Huu ni mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.”
20 Vivyo hivyo baada ya kula, akakitwaa kikombe, akisema, “Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, imwagikayo kwa ajili yenu. 21 Lakini mkono wake huyo atakayenisaliti uko hapa mezani pamoja nami. 22 Mwana wa Adamu anaenda zake kama ilivyokusudiwa. Lakini ole wake mtu huyo amsalitiye.” 23 Wakaanza kuulizana wenyewe ni nani miongoni mwao angeweza kufanya jambo hilo.
Mabishano Kuhusu Ukuu
24 Pia yakazuka mabishano katikati ya wanafunzi kwamba ni nani aliyeonekana kuwa mkuu kuliko wote miongoni mwao. 25Isa akawaambia, “Wafalme na watu wa Mataifa huwatawala watu kwa nguvu. Nao wenye mamlaka juu yao hujiita ‘Wafadhili.’ 26 Lakini ninyi msifanane nao. Bali yeye aliye mkuu kuliko wote miongoni mwenu, inampasa kuwa kama yeye aliye mdogo wa wote, naye atawalaye na awe kama yeye ahudumuye. 27 Kwani ni nani aliye mkuu? Ni yule aketiye mezani au ni yule ahudumuye? Si ni yule aliyekaa mezani? Lakini mimi niko miongoni mwenu kama yule ahudumuye. 28 Ninyi mmekuwa pamoja nami katika majaribu yangu. 29 Nami kama Baba#22:29 Jina Baba linaonyesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. yangu alivyonipa ufalme, kadhalika mimi nami ninawapa ninyi, 30ili mpate kula na kunywa mezani pangu katika karamu ya ufalme wangu, na kukaa katika viti vya enzi, mkihukumu makabila kumi na mawili ya Israeli.”
Isa Atabiri Kuwa Petro Atamkana
31 Isa akasema, “Simoni, Simoni, sikiliza, Shetani ameomba kuwapepeta ninyi wote kama ngano. 32 Lakini nimekuombea wewe Simoni ili imani yako isishindwe, nawe ukiisha kunirudia, uwaimarishe ndugu zako.”
33 Petro akajibu, “Bwana Isa, niko tayari kwenda pamoja nawe gerezani na hata kifoni.”
34 Isa akamjibu, “Ninakuambia Petro, kabla jogoo hajawika usiku wa leo, utakana mara tatu kwamba hunijui mimi.”
Mfuko, Mkoba Na Upanga
35 Kisha Isa akawauliza, “Nilipowatuma bila mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu chochote?”
Wakajibu, “La, hatukupungukiwa na kitu chochote.”
36Akawaambia, “Lakini sasa, aliye na mfuko na auchukue, na aliye na mkoba vivyo hivyo. Naye asiye na upanga, auze joho lake anunue mmoja. 37 Kwa sababu, nawaambia, andiko hili lazima litimizwe juu yangu, kwamba, ‘Alihesabiwa pamoja na wakosaji’; kwa kweli yaliyoandikwa kunihusu mimi hayana budi kutimizwa.”
38Wanafunzi wake wakamwambia, “Bwana Isa, tazama hapa kuna panga mbili.”
Akawajibu, “Inatosha.”
Isa Aomba Kwenye Mlima Wa Mizeituni
(Mathayo 26:36-46; Marko 14:32-42)
39 Isa akatoka, akaenda kwenye Mlima wa Mizeituni kama ilivyokuwa kawaida yake, nao wanafunzi wake wakamfuata. 40 Walipofika huko, akawaambia wanafunzi wake, “Ombeni, msije mkaingia majaribuni.” 41 Akajitenga nao kama umbali wa kutupa jiwe, akapiga magoti, akaomba 42 akisema, “Baba, kama ni mapenzi yako, niondolee kikombe hiki. Lakini si kama nipendavyo, bali mapenzi yako yatendeke.” 43 Malaika kutoka mbinguni akamtokea, akamtia nguvu. 44 Naye akiwa katika maumivu makuu, akaomba kwa bidii, nalo jasho lake likawa kama matone ya damu yakidondoka ardhini.
45Baada ya kuomba, akawarudia wanafunzi wake akawakuta wamelala, wakiwa wamechoka kutokana na huzuni. 46 Naye akawauliza, “Mbona mmelala? Amkeni, mwombe ili msije mkaingia majaribuni.”
Isa Akamatwa
(Mathayo 26:47-56; Marko 14:43-50; Yohana 18:3-11)
47 Isa alipokuwa bado anazungumza, umati mkubwa wa watu ukaja. Uliongozwa na Yuda, ambaye alikuwa mmoja wa wale wanafunzi Kumi na Wawili. Akamkaribia Isa ili ambusu. 48Lakini Isa akamwambia, “Yuda, je, unamsaliti Mwana wa Adamu kwa busu?”
49Wafuasi wa Isa walipoona yale yaliyokuwa yanakaribia kutokea, wakasema, “Bwana Isa, tuwakatekate kwa panga zetu?” 50 Mmoja wao akampiga mtumishi wa kuhani mkuu kwa upanga, akamkata sikio la kuume.
51Lakini Isa akasema, “Acheni!” Akaligusa lile sikio la yule mtu na kumponya.
52 Kisha Isa akawaambia wale viongozi wa makuhani, maafisa wa walinzi wa Hekalu, pamoja na wazee waliokuwa wamekuja kumkamata, “Mmekuja na panga na marungu, kana kwamba mimi ni mnyang’anyi? 53 Siku kwa siku nilikuwa pamoja nanyi Hekaluni lakini hamkunikamata. Lakini hii ni saa yenu, wakati giza linatawala!”
Petro Amkana Isa
(Mathayo 26:57-75; Marko 14:53-72; Yohana 18:12-27)
54 Kisha wakamkamata Isa, wakamchukua, wakaenda naye mpaka nyumbani kwa kuhani mkuu. Lakini Petro akafuata kwa mbali. 55 Walipokwisha kuwasha moto katikati ya ua na kuketi pamoja, Petro naye akaketi pamoja nao. 56Mtumishi mmoja wa kike akamwona kwa mwanga wa moto akiwa ameketi pale. Akamtazama sana, akasema, “Huyu mtu pia alikuwa pamoja na Isa!”
57Lakini Petro akakana, akasema, “Ewe mwanamke, hata simjui!”
58 Baadaye kidogo, mtu mwingine alimwona Petro akasema, “Wewe pia ni mmoja wao!” Petro akajibu, “Wewe mtu, mimi sio mmoja wao!”
59 Baada ya muda wa kama saa moja hivi, mtu mwingine akazidi kusisitiza, “Kwa hakika huyu mtu naye alikuwa pamoja na Isa, kwa maana yeye pia ni Mgalilaya.”
60Petro akajibu, “Wewe mtu, mimi sijui unalosema!” Wakati huo huo, akiwa bado anazungumza, jogoo akawika. 61 Naye Bwana Isa akageuka, akamtazama Petro. Ndipo Petro akakumbuka lile neno ambalo Bwana Isa alimwambia: “Kabla jogoo hajawika leo, utanikana mara tatu.” 62Naye akaenda nje, akalia kwa majonzi.
Walinzi Wamdhihaki Isa Na Kumpiga
(Mathayo 26:67-68; Marko 14:65)
63 Watu waliokuwa wanamlinda Isa wakaanza kumdhihaki na kumpiga. 64Wakamfunga kitambaa machoni na kumuuliza, “Tabiri! Tuambie ni nani aliyekupiga?” 65 Wakaendelea kumtukana kwa matusi mengi.
Isa Apelekwa Mbele Ya Baraza
(Mathayo 26:59-66; Marko 14:55-64; Yohana 18:28-38)
66 Kulipopambazuka, baraza la wazee wa watu,#22:66 Baraza la wazee hapa ina maana ya Sanhedrin ambalo lilikuwa ndilo Baraza la juu kabisa la utawala wa Kiyahudi, lililoundwa na wazee 70 pamoja na kuhani mkuu. yaani viongozi wa makuhani na walimu wa Torati, wakakutana pamoja, naye Isa akaletwa mbele yao. 67 Wakamwambia, “Kama wewe ndiwe Al-Masihi, tuambie.”
Isa akawajibu, “Hata nikiwaambia hamtaamini. 68 Nami nikiwauliza swali, hamtanijibu. 69 Lakini kuanzia sasa, Mwana wa Adamu ataketi mkono wa kuume wa Mungu Mwenye Nguvu.”
70 Wote wakauliza, “Wewe basi ndiwe Mwana wa Mungu?#22:70 Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yn 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili.
Yeye akawajibu, “Ninyi mwasema kwamba mimi ndiye.”
71 Kisha wakasema, “Tuna haja gani tena ya ushahidi zaidi? Tumesikia wenyewe kutoka kinywani mwake.”

Markert nå:

Luka 22: NMM

Marker

Del

Kopier

None

Vil du ha høydepunktene lagret på alle enhetene dine? Registrer deg eller logg på