Mwanzo 9
9
Mwenyezi Mungu aweka agano na Nuhu
1Ndipo Mungu akawabariki Nuhu na wanawe, akiwaambia, “Zaeni, mkaongezeke kwa idadi, na mkaijaze tena dunia. 2Wanyama wote wa nchi, na ndege wote wa angani, na kila kiumbe kinachotambaa juu ya ardhi, na samaki wote wa baharini wamekabidhiwa mikononi mwenu, nao watawaogopa na kuwahofu. 3Kila kitu chenye uhai kiendacho kitakuwa chakula chenu. Kama vile nilivyowapa mimea mbalimbali, sasa nawapa kila kitu.
4“Lakini kamwe msile nyama ambayo bado ina damu, kwa maana damu ni uhai. 5Hakika damu ya uhai wenu nitaidai. Nitaidai kutoka kwa kila mnyama. Kutoka kwa kila mwanadamu pia nitaidai kwa ajili ya uhai wa binadamu mwenzake.
6“Yeyote amwagaye damu ya mwanadamu,
damu yake itamwagwa na mwanadamu;
kwa kuwa katika mfano wa Mungu,
Mungu alimuumba mwanadamu.
7Bali ninyi, zaeni mwongezeke kwa idadi; zidini duniani na kuijaza.”
8Ndipo Mungu akamwambia Nuhu na wanawe pamoja naye: 9“Sasa mimi ninaweka agano langu nanyi, pamoja na uzao wenu baada yenu, 10pia na kila kiumbe hai kilichokuwa pamoja nanyi: ndege, mifugo, na wanyama pori wote, wale wote waliotoka katika safina pamoja nanyi: kila kiumbe hai duniani. 11Ninaweka agano nanyi: Kamwe uhai hautafutwa tena kwa gharika; kamwe hakutakuwa tena gharika ya kuangamiza dunia.”
12Mungu akasema, “Hii ni ishara ya agano ninalofanya kati yangu na ninyi na kila kiumbe hai kilicho pamoja nanyi, agano kwa vizazi vyote vijavyo: 13Nimeweka upinde wangu wa mvua mawinguni, nao utakuwa ishara ya agano nifanyalo kati yangu na dunia. 14Wakati wowote ninapotanda mawingu juu ya dunia na upinde wa mvua ukatokea mawinguni, 15nitakumbuka agano langu kati yangu na ninyi na viumbe vyote vilivyo hai vya kila aina. Kamwe maji hayatakuwa tena gharika ya kuangamiza uhai wote. 16Wakati wowote upinde wa mvua unapotokea mawinguni, nitauona na kukumbuka agano la milele kati ya Mungu na viumbe vyote vilivyo hai vya kila aina duniani.”
17Hivyo Mungu akamwambia Nuhu, “Hii ndiyo ishara ya agano ambalo nimelifanya kati yangu na viumbe vyote vilivyo hai duniani.”
Wana wa Nuhu
18Wana wa Nuhu waliotoka ndani ya safina walikuwa: Shemu, na Hamu, na Yafethi. (Hamu ndiye alikuwa baba wa Kanaani.) 19Hao walikuwa wana watatu wa Nuhu, na kutokana nao watu walienea katika dunia.
20Nuhu akawa mkulima, akawa mtu wa kwanza kupanda mizabibu. 21Alipokunywa huo mvinyo wake, akalewa na akalala uchi kwenye hema lake. 22Hamu, baba wa Kanaani, akauona uchi wa baba yake na kuwaeleza ndugu zake wawili waliokuwa nje. 23Lakini Shemu na Yafethi wakachukua nguo, wakaitanda mabegani mwao wote wawili, kisha wakaenda kinyumenyume, wakaufunika uchi wa baba yao. Nyuso zao zilielekea upande mwingine ili wasiuone uchi wa baba yao.
24Nuhu alipolevuka na kujua lile mwanawe mdogo alilomtendea, 25akasema,
“Alaaniwe Kanaani!
Atakuwa mtumwa wa chini kabisa
kwa ndugu zake.”
26Pia akasema,
“Atukuzwe Mwenyezi Mungu, Mungu wa Shemu!
Kanaani na awe mtumwa wa Shemu.
27Mungu na apanue mipaka ya Yafethi;
Yafethi na aishi katika mahema ya Shemu,
na Kanaani na awe mtumwa wake.”
28Baada ya gharika, Nuhu aliishi miaka mia tatu na hamsini. 29Nuhu aliishi jumla ya miaka mia tisa na hamsini, ndipo akafa.
Markert nå:
Mwanzo 9: ONMM
Marker
Del
Kopier
Vil du ha høydepunktene lagret på alle enhetene dine? Registrer deg eller logg på
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu™ ONMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Biblica® Open Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.