Yohana MT. 3
3
1PALIKUWA na mtu mmoja wa Mafarisayo, jina lake Nikodemo, mkuu wa Wayahudi; 2huyu alikuja kwa Yesu usiku, akamwambia, Rabbi, twajua ya kuwa u mwalimu, umetoka kwa Mungu; kwa maana hakuna mtu awezae kuzifanya ishara hizi uzifanyazo wewe, illa Mungu awe pamoja nae. 3Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa marra ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu. 4Nikodemo amwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mama yake marra ya pili akazaliwa? 5Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu. 6Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho. 7Usitaajahu kwa kuwa nilikuambia, Hamna buddi kuzaliwa marra ya pili. 8Upepo huenda utakako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na killa mtu aliyezaliwa kwa Roho. 9Nikodemo akajibu, akamwambia, Yawezaje kuwa haya? 10Yesu akajibu akamwambia, Je! Wewe u mwalimu katika Israeli, na haya huyafahamu? 11Amin, amin, nakuambia, Tulijualo twalisema, na tuliloliona twalishuhudu; na ushuhuda wetu hamwukubali. 12Ikiwa nimewaambia mambo ya duniani, nanyi hamwa, mini, mtaaminije, niwaambiapo mambo ya mbinguni? 13Na hapana mtu aliyepanda mbinguni, illa yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, Mwana wa Adamu alioko mbinguni. 14Na kama Musa alivyomwinua nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana buddi kuinuliwa: 15illi asipotee mtu aliye yole amwaminiye, bali awe na uzima wa milele.
16Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hatta akampeleka Mwana wake wa pekee, illi mtu aliye yote amwaminiye asipotee, bali apate uzima wa milele. 17Maana Mungu hakumpeleka Mwana wake ulimwenguni auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe nae. 18Amwaminiye hahukumiwi; asiyemwamini amekwisha kuhukumiwa, kwa maana hakuliamini jina la Mwana wa pekee wa Mungu. 19Na hii ndiyo hukumu, ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, watu wakapenda giza zaidi ya nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. 20Maana killa atendae manyonge huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasikemewe; 21hali aitendae kweli huja kwenye nuru, matendo yake yaonekane ya kuwa yametendwa katika Mungu.
22Baada ya haya Yesu na wanafunzi wake walikwenda hatta inchi ya Kiyahudi; akashinda huko pamoja nao, akibatiza. 23Yohana nae alikuwa akibatiza huko Ainon, karibu na Salim, kwa sababu palikuwa na maji tele; watu wakamwendea wakabatizwa. 24Maana Yohana alikuwa hajatiwa gerezani. 25Bassi palitokea mashindano ya wanafunzi wa Yohana na Wayahudi katika khabari ya utakaso. 26Wakamwendea Yohana, wakamwambia, Rabbi, yeye aliyekuwa pamoja nawe ngʼambu ya Yardani, uliyemshuhudia wewe, huyu nae anabatiza, na watu wote wanamwendea. 27Yohana akajibu, akasema, Hawezi mtu kupokea neno lo lote isipokuwa amepewa kutoka mbinguni. 28Ninyi wenyewe mwanishuhudia ya kwamba nalisema, Mimi siye Kristo, bali nimetumwa mbele yake. 29Aliye nae bibi arusi ndiye bwana arusi; lakini rafiki yake bwana arusi anaesimama na kumsikia, aifurahia sana sauti yake bwana arusi: bassi hii furaha yangu imetimia. 30Yeye hana buddi kuzidi, bali mimi kupungua. 31Ajae kutoka juu huyu yu juu ya yote: aliye wa dunia, asili yake ni ya dunia, na anena mambo ya dunia: yeye ajae kutoka mbinguni yu juu ya yote. 32Aliyoyaona na kuyasikia ndiyo anayoshuhudia, wala hapana anaeukubali ushuhuda wake. 33Aliyeukubali ushuhuda wake ametia muhuri yake kwamba Mungu ni kweli. 34Kwa kuwa yeye aliyetumwa na Mungu huyanena maneno ya Mungu: kwa sababu Mungu hampi Roho kwa kupima. 35Baba ampenda Mwana, amempa vyote mikononi mwake. 36Amwaminiye Mwana ana uzima wa milele; na asiyemtii Mwana hataona uzima, hali ghadhabu ya Mungu inamkalia.
Nu geselecteerd:
Yohana MT. 3: SWZZB1921
Markering
Deel
Kopiëren
Wil je jouw markerkingen op al je apparaten opslaan? Meld je aan of log in
Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.