Luka 21
21
Unabii kuhusu mambo yajayo
(Luka 21:1-38)
Sadaka ya mjane maskini
(Marko 12:41-44)
1Isa alipoinua macho yake, aliwaona matajiri wakiweka sadaka zao kwenye sanduku la hazina ya Hekalu. 2Akamwona pia mjane mmoja maskini akiweka humo sarafu mbili ndogo za shaba. 3Isa akasema, “Amin, nawaambia, huyu mjane maskini ameweka humo zaidi ya watu wengine wote. 4Hawa watu wengine wote wametoa sadaka kutokana na wingi wa mali yao. Lakini huyu mjane ametoa kutokana na umaskini wake vyote alivyokuwa navyo, hata kile alichohitaji ili kuishi.”
Kubomolewa kwa Hekalu kwatabiriwa
(Mathayo 24:1-2; Marko 13:1-2)
5Baadhi ya wanafunzi wake wakawa wanamwonesha jinsi Hekalu lilivyopambwa kwa mawe mazuri na kwa vitu vilivyotolewa kuwa sadaka kwa Mungu. Lakini Isa akawaambia, 6“Kuhusu haya mnayoyaona hapa, wakati utafika ambapo hakuna jiwe moja litakalobaki juu ya jingine, bali kila moja litabomolewa.”
Ishara za nyakati za mwisho
(Mathayo 24:3-14; Marko 13:3-13)
7Wakamuuliza, “Mwalimu, mambo haya yatatukia lini? Ni dalili gani itaonesha kwamba yanakaribia kutendeka?”
8Isa akawajibu, “Jihadharini msije mkadanganywa. Maana wengi watakuja kwa Jina langu, wakidai, ‘Mimi ndiye,’ na, ‘Wakati umekaribia.’ Msiwafuate. 9Lakini msikiapo habari za vita na machafuko, msiogope. Kwa maana hayo ni lazima yatokee kwanza, ila ule mwisho hautakuja wakati huo.”
10Kisha akawaambia: “Taifa litainuka dhidi ya taifa jingine, na ufalme mmoja dhidi ya ufalme mwingine. 11Kutakuwa na mitetemeko mikubwa ya ardhi, na njaa kali, na magonjwa ya kuambukiza katika sehemu mbalimbali. Pia kutakuwa na matukio ya kutisha na ishara kuu kutoka mbinguni.
12“Lakini kabla yote hayajatokea, watawakamata ninyi na kuwatesa. Watawatia mikononi mwa wakuu wa masinagogi na kuwafunga magerezani. Nanyi mtapelekwa mbele ya wafalme na watawala kwa ajili ya Jina langu. 13Hii itawapa nafasi ya kushuhudia. 14Lakini kusudieni mioyoni mwenu msisumbuke awali kuhusu mtakalosema mbele ya mashtaka. 15Kwa maana nitawapa maneno na hekima ambayo hakuna hata adui yenu mmoja atakayeweza kushindana nayo wala kuipinga. 16Mtasalitiwa hata na wazazi, ndugu, jamaa na rafiki zenu, na baadhi yenu watawaua. 17Mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya Jina langu. 18Lakini hapatakuwa na unywele mmoja wa kichwa chenu utakaoangamia. 19Kwa kuvumilia mtaokoa roho zenu.
Kuharibiwa kwa Yerusalemu kwatabiriwa
(Mathayo 24:15-21; Marko 13:14-19)
20“Mtakapoona mji wa Yerusalemu umezungukwa na majeshi, basi fahamuni kwamba kuharibiwa kwake kumekaribia. 21Wakati huo, wale walio Yudea wakimbilie milimani, walio mjini Yerusalemu watoke humo, nao wale walio mashambani wasiingie mjini. 22Kwa sababu huu utakuwa ni wakati wa adhabu ili kutimiza yote yaliyoandikwa. 23Ole wao wenye mimba na wale wanaonyonyesha watoto siku hizo! Kutakuwa na dhiki kuu katika nchi na ghadhabu juu ya hawa watu. 24Wataanguka kwa makali ya upanga, na wengine watachukuliwa kuwa mateka katika mataifa yote. Nao mji wa Yerusalemu utakanyagwa na watu wa Mataifa hadi muda wa hao watu wa Mataifa utimie.
Kuja kwa Mwana wa Adamu
(Mathayo 24:29-35; Marko 13:24-31)
25“Kutakuwa na ishara katika jua, mwezi na nyota. Hapa duniani, mataifa yatakuwa katika dhiki na fadhaa kutokana na ngurumo na misukosuko ya bahari. 26Watu watazimia roho kutokana na hofu kuu na kuyaona yale mambo yanayotokea duniani, kwa maana nguvu za angani zitatikisika. 27Wakati huo ndipo watakapomwona Mwana wa Adamu akija mawinguni pamoja na uweza na utukufu mkuu. 28Mambo haya yatakapoanza kutendeka, simameni na mkaviinue vichwa vyenu, kwa sababu ukombozi wenu umekaribia.”
Somo kuhusu mtini
(Mathayo 24:32-35; Marko 13:28-31)
29Akawaambia mfano huu: “Uangalieni mtini na miti mingine yote. 30Inapochipua majani, ninyi wenyewe mnaweza kuona na kutambua wenyewe ya kuwa wakati wa kiangazi umekaribia. 31Vivyo hivyo, mnapoyaona mambo haya yakitukia, mtambue kwamba ufalme wa Mungu umekaribia.
32“Amin, nawaambia, kizazi hiki hakitapita hadi mambo haya yote yawe yametimia. 33Mbingu na nchi zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.
Himizo la kukesha
34“Jihadharini mioyo yenu isije ikalemewa na anasa, ulevi na fadhaa za maisha haya, nayo siku ile ikawakuta ninyi bila kutazamia kama mtego unasavyo. 35Hivyo ndivyo siku hiyo itakavyowapata wanadamu wote wanaoishi katika uso wa dunia yote. 36Kesheni daima na mwombe ili mweze kuokoka na yale yote yatakayotokea na kusimama mbele ya Mwana wa Adamu.”
37Kila siku Isa alikuwa akifundisha Hekaluni, na jioni ilipofika, alienda zake kwenye Mlima wa Mizeituni na kukaa huko usiku kucha. 38Nao watu wote walikuja asubuhi na mapema Hekaluni ili kumsikiliza.
Pašlaik izvēlēts:
Luka 21: ONMM
Izceltais
Dalīties
Kopēt
Vai vēlies, lai tevis izceltie teksti tiktu saglabāti visās tavās ierīcēs? Reģistrējieties vai pierakstieties
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu™ ONMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Biblica® Open Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.