Luka 15

15
Furaha Mbinguni
(Mt 18:12-14)
1Watoza ushuru na wenye dhambi wengi waliendelea kuja kumsikiliza Yesu. 2Hivyo Mafarisayo na walimu wa sheria wakaanza kulalamika wakisema, “Mtazameni mtu huyu#15:2 mtu huyu Yaani, Yesu. Adui zake walikuwa wanakwepa kutamka jina lake. huwakaribisha wenye dhambi na hata kula pamoja nao!”
3Hivyo Yesu akawaambia mfano huu, 4“Chukulia mmoja wenu ana kondoo mia, lakini mmoja akapotea. Utafanya nini? Utawaacha wale tisini na tisa na kwenda kumtafuta yule mmoja aliyepotea mpaka umpate. 5Na ukishampata, utafurahi sana. Utambeba mabegani mwako 6mpaka nyumbani. Kisha utakwenda kwa majirani na rafiki zako na utawaambia, ‘Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimempata kondoo wangu aliyepotea!’ 7Katika namna hiyo hiyo ninawaambia, kunakuwa na furaha zaidi mbinguni kwa sababu ya mtu anayeacha dhambi zake. Kuna furaha zaidi kwa ajili ya mtu mmoja anayeacha dhambi kuliko watu wema tisini na tisa ambao hudhani hawahitaji kubadilika.
8Fikiria kuhusu mwanamke mwenye sarafu kumi za fedha,#15:8 sarafu kumi za fedha Kila sarafu, Sarafu ya Kiyunani iliyoitwa drachma ilikuwa na thamani ya ujira au mshahara wa siku moja. lakini akapoteza sarafu moja kati ya hizo. Atawasha taa na kuifagia nyumba. Ataitafuta sarafu kwa bidii mpaka aione. 9Na akiiona, atawaita rafiki na jirani zake na kuwaaambia, ‘Furahini pamoja nami, kwa sababu nimeipata sarafu niliyoipoteza!’ 10Katika namna hiyo hiyo, ni furaha kwa malaika wa Mungu, mwenye dhambi mmoja anapotubu.”
Simulizi Kuhusu Mwana Mpotevu
11Kisha Yesu akasema, “Alikuwepo mtu mmoja aliyekuwa na wana wawili. 12Mwana mdogo alimwambia baba yake, ‘Baba, nipe sehemu ya mali ninayotarajia kurithi baadaye.’ Hivyo baba yake akagawa utajiri wake kwa wanawe wawili.
13Baada ya siku chache yule mdogo akauza mali zake, akachukua pesa zake na akaondoka. Akasafiri mbali katika nchi nyingine. Huko alipoteza pesa zake zote katika starehe na anasa. 14Baada ya kutumia vyote alivyokuwa navyo, kukatokea njaa kali katika nchi ile yote. Akawa na njaa na mhitaji wa pesa. 15Hivyo alikwenda kutafuta kazi kwa mwenyeji mmoja wa nchi ile, naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe. 16Alikuwa anasikia njaa kiasi kwamba alikuwa anatamani kula chakula walichokula nguruwe. Lakini hakuna mtu aliyempa chakula.
17Alipotambua namna alivyokuwa mjinga, akafikiri moyoni mwake na kusema, ‘Wafanyakazi wote wa baba yangu wana chakula kingi. Lakini niko hapa kama niliyekufa kwa sababu sina chakula. 18Nitaondoka na kurudi kwa baba yangu. Nitamwambia hivi: Baba, nimemtenda Mungu dhambi na nimekukosea wewe. 19Sistahili kuitwa mwanao tena. Lakini niruhusu niwe kama mmoja wa wafanyakazi wako.’ 20Hivyo akaondoka na kurudi kwa baba yake.
Alipokuwa mbali na nyumbani kwao, baba yake alimwona, akamwonea huruma. Akamkimbilia, akamkumbatia na kumbusu sana. 21Mwanaye akasema, ‘Baba, nimemtenda Mungu dhambi na nimekukosea wewe; sistahili kuitwa mwanao tena.’
22Lakini baba akawaambia watumishi wake, ‘Fanyeni haraka, leteni vazi maalumu, mvikeni. Pia, mvisheni viatu vizuri na pete kwenye kidole chake. 23Na leteni ndama aliyenona, mchinjeni ili tule na kusherehekea. 24Kwa sababu mwanangu alikuwa amekufa, lakini sasa yuko hai tena! Alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana.’ Wakaanza kusherehekea.
25Mwanaye mkubwa alikuwa shambani. Alipoikaribia nyumba, alisikia sauti za muziki na kucheza. 26Akaita mmoja wa watumishi na akamwuliza, ‘Kuna nini?’ 27Mtumishi akasema, ‘Mdogo wako amerudi, na baba yako amechinja ndama aliyenona. Anafurahi kwa sababu amempata mwanaye akiwa salama na mzima.’
28Mwana mkubwa alikasirika na hakutaka kwenda kwenye sherehe. Hivyo baba yake akatoka nje kumsihi. 29Lakini alimwambia baba yake, ‘Tazama, miaka yote hii nimekutumikia kama mtumishi, kamwe sijaacha kukutii! Lakini hujawahi kunipa hata mbuzi mdogo ili nisherehekee pamoja na rafiki zangu. 30Lakini alipokuja huyu mwanao aliyepoteza mali zako kwa makahaba, umemchinjia ndama aliyenona!’
31Baba yake akamwambia, ‘Mwanangu, daima umekuwa pamoja nami, na vyote nilivyo navyo ni vyako. 32Lakini tulipaswa kusherehekea. Mdogo wako alikuwa amekufa, lakini sasa ni hai tena. Alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana.’”

ទើបបានជ្រើសរើសហើយ៖

Luka 15: TKU

គំនូស​ចំណាំ

ចែក​រំលែក

ចម្លង

None

ចង់ឱ្យគំនូសពណ៌ដែលបានរក្សាទុករបស់អ្នក មាននៅលើគ្រប់ឧបករណ៍ទាំងអស់មែនទេ? ចុះឈ្មោះប្រើ ឬចុះឈ្មោះចូល