Luka 11
11
Yesu Afundisha Kuhusu Maombi
(Mt 6:9-15)
1Siku moja Yesu alitoka akaenda mahali fulani kuomba. Alipomaliza, mmoja wa wafuasi wake akamwambia, “Yohana aliwafundisha wafuasi wake namna ya kuomba. Bwana, tufundishe nasi pia.”
2Yesu akawaambia wafuasi wake, “Hivi ndivyo mnapaswa kuomba:
‘Baba yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe daima.
Tunaomba Ufalme wako uje.
3Utupe chakula tunachohitaji kila siku.
4Utusamehe dhambi zetu,
kama tunavyomsamehe kila mtu anayetukosea.
Na usiruhusu tukajaribiwa.’”
Mwombeni Mungu Kile Mnachohitaji
(Mt 7:7-11)
5-6Kisha Yesu akawaambia, “Chukulia mmoja wenu angekwenda kwa rafiki yake usiku na kumwambia, ‘Rafiki yangu aliyekuja mjini amekuja kunitembelea. Lakini sina chakula cha kumpa ili ale. Tafadhali nipe mikate mitatu.’ 7Rafiki yako ndani ya nyumba akajibu, ‘Nenda zako! Usinisumbue! Mlango umefungwa. Mimi na watoto wangu tumeshapanda kitandani kulala. Siwezi kuamka ili nikupe kitu chochote kwa sasa.’ 8Ninawaambia, urafiki unaweza usimfanye aamke akupe kitu chochote. Lakini hakika ataamka ili akupe unachohitaji ikiwa utaendelea kumwomba. 9Hivyo ninawaambia, Endeleeni kuomba na Mungu atawapa. Endeleeni kutafuta na mtapata. Endeleeni kubisha milangoni, na milango itafunguliwa kwa ajili yenu. 10Ndiyo, kila atakayeendelea kuomba atapokea. Kila atakayeendelea kutafuta atapata. Na kila atakayeendelea kubisha mlangoni, mlango utafunguliwa kwa ajili yake. 11Je! kuna mmoja wenu aliye na mwana? Utafanya nini ikiwa mwanao atakuomba samaki? Je! kuna baba yeyote anayeweza kumpa nyoka? 12Au akiomba yai, utampa nge? Hakika hakuna baba wa namna hivyo. 13Ikiwa ninyi waovu mnajua namna ya kuwapa watoto wenu vitu vizuri. Vivyo hivo, hakika Baba yenu aliye mbinguni anajua namna ya kuwapa Roho Mtakatifu wale wanao mwomba?”
Nguvu ya Yesu Inatoka kwa Mungu
(Mt 12:22-30; Mk 3:20-27)
14Wakati mmoja Yesu alikuwa akitoa pepo aliyemfanya mtu ashindwe kuzungumza. Ikawa, pepo alipotoka, yule mtu akaanza kuongea, umati wa watu walishangaa. 15Lakini baadhi ya watu walisema, “Anatumia nguvu za Shetani kuwatoa pepo. Shetani#11:15 Shetani Jina la Mwovu lenye maana “Adui”. Kwa maana ya kawaida, “Beelzebuli” kwa Kiyunani (mwovu). Pia katika mstari wa 18,19. ni mtawala wa pepo wachafu.”
16Baadhi ya watu wengine waliokuwa pale walitaka kumjaribu Yesu, walimwomba afanye muujiza kama ishara kutoka kwa Mungu. 17Lakini alijua walichokuwa wanafikiria, hivyo akawaambia, “Kila ufalme unaopigana wenyewe huteketezwa; na familia yenye magomvi husambaratika. 18Hivyo, ikiwa Shetani anapigana yeye mwenyewe, ufalme wake utasimamaje? Ninawauliza hivi kwa kuwa mnasema kwamba ninatoa pepo kwa kutumia nguvu za Shetani. 19Lakini ikiwa ninatoa pepo kwa kutumia nguvu za Shetani, watu wenu wanatumia nguvu gani wanapotoa pepo? Hivyo watu wenu wenyewe watathibitisha kuwa ninyi ni waovu. 20Lakini, ninatumia nguvu za Mungu kutoa pepo. Hii inaonesha kuwa Ufalme wa Mungu umekuja kwenu sasa.
21Mwenye nguvu aliye na silaha nyingi anapoilinda nyumba yake, vitu vilivyomo ndani ya nyumba yake huwa salama. 22Lakini chukulia kuwa mwenye nguvu zaidi kuliko yeye akimshambulia na kumshinda, yule mwenye nguvu zaidi humnyang'anya silaha zake zote alizokuwa akizitegemea kuilinda nyumba yake. Ndipo mwenye nguvu zaidi atavitumia vitu vya yule mtu wa kwanza kadri anavyotaka.
23Mtu yeyote asiye pamoja nami, yuko kinyume nami. Na mtu yeyote asiyefanya kazi pamoja nami anafanya kinyume nami.
Hatari ya Kuwa Mtupu
(Mt 12:43-45)
24Mtu anapotokwa na roho chafu, roho hiyo husafiri sehemu zilizo kavu, ikitafuta mahali ili ipumzike. Lakini hukosa mahali pa kupumzika. Hivyo husema, ‘Nitarudi kwenye nyumba nilikotoka.’ 25Inaporudi hukuta nyumba imesafishwa na kupangwa vizuri. 26Ndipo roho hiyo chafu huenda ikachukua roho wengine saba, walio waovu kuliko yenyewe. Na kwa pamoja roho zote hizo huingia na kuishi ndani ya mtu huyo, na mtu huyo hupata matatizo mengi kuliko ya kwanza.”
Watu Wanaobarikiwa na Mungu
27Yesu alipokuwa akisema mambo haya, mwanamke mmoja katika kundi la watu akapaza sauti akamwambia “Amebarikiwa na Mungu mwanamke aliyekuzaa na kukunyonyesha!”
28Lakini Yesu akasema, “Wamebarikiwa zaidi wanaosikia na kuyatii mafundisho ya Mungu.”
Baadhi ya Watu Wawa na Mashaka na Mamlaka ya Yesu
(Mt 12:38-42; Mk 8:12)
29Baada ya kundi la watu kuongezeka na kumzunguka, Yesu alisema, “Ninyi watu mnaoishi sasa ni waovu. Mnaomba muujiza kama ishara kutoka kwa Mungu. Lakini hakuna muujiza utakaofanyika ili kuwathibitishia jambo lolote. Ishara pekee mtakayopata ni kile kilichompata Yona.#11:29 Yona Nabii katika Agano la Kale. Baada ya siku tatu akiwa katika tumbo la samaki, alitoka akiwa hai. Kisha alikwenda katika mji uliojaa uovu, mji wa Ninawi ili kuwapa watu maonyo ya Mungu. 30Yona alikuwa ishara kwa watu walioishi katika mji wa Ninawi. Ni sawasawa na Mwana wa Adamu atakavyokuwa ishara kwa watu wa wakati huu.
31Siku ya hukumu, ninyi watu mnaoishi sasa, mtalinganishwa na Malkia wa Kusini,#11:31 Malkia wa Kusini Au “Malkia wa Sheba.” Alisafiri kama maili 1,000 (kilomita 1,600) ili kujifunza hekima ya Mungu kutoka kwa Sulemani. Tazama 1 Fal 10:1-13. naye pia, atakuwa shahidi atakayeonyesha namna mlivyo waovu. Kwa nini ninasema haya? Kwa sababu alisafiri kutoka mbali, mbali sana ili ayasikilize mafundisho yenye hekima ya Suleimani. Na ninawaambia mkuu#11:31 mkuu Kwa maana ya kawaida, “mtu mkuu zaidi”. Pia katika mstari wa 32. kuliko Suleimani yupo hapa, lakini hamnisikilizi!
32Siku ya hukumu, ninyi watu mnaoishi sasa mtafananishwa pia na watu wa Ninawi, nao watakuwa mashahidi watakaoonyesha makosa yenu. Ninasema hivi kwa sababu Yona alipowahubiri, walibadili mioyo na maisha yao. Na sasa mnamsikia mtu aliye mkuu kuliko Yona, Lakini hamtaki kubadilika!
Iweni Mwanga kwa Ajili ya Ulimwengu
(Mt 5:15; 6:22-23)
33Hakuna mtu anayechukua taa na kuiweka mahali palipofichika au kuifunika. Badala yake huiweka mahali palipo wazi, ili wanaoingia ndani waweze kuiona nuru yake. 34Namna unavyowatazama watu inaonesha kwa hakika jinsi ulivyo. Unapowatazama watu katika hali isiyo ya ubinafsi, inaonesha wazi kuwa umejaa nuru. Lakini unapowatazama watu katika namna ya uchoyo, ni wazi kuwa umejaa giza.#11:34 Kwa maana ya kawaida, “Taa ya mwili ni jicho lako. Unapowatazama watu bila kuwa na kinyongo, mwili wako wote unakuwa umejaa nuru. Lakini ikiwa jicho lako ni la uovu, mwili wako una giza.” 35Hivyo iweni waangalifu ili nuru iliyo ndani yenu usiwe giza! 36Ikiwa umejaa nuru na hakuna sehemu yenye giza ndani yako, basi utang'aa, kama nuru ya kwenye taa.”
Yesu Awakosoa Viongozi wa Kidini
(Mt 23:1-36; Mk 12:38-40; Lk 20:45-47)
37Baada ya Yesu kumaliza kuzungumza, Farisayo mmoja alimwalika Yesu kula pamoja naye. Hivyo Yesu alikwenda na kuketi sehemu ya kulia chakula. 38Lakini Farisayo alishangaa alipoona Yesu hakunawa#11:38 hakunawa Hakunawa kwa maana ya kuwa kunawa mikono au kuoga mwili wote ilikuwa desturi ya dini ya Kiyahudi na Mafarisayo waliipa desturi hii umuhimu mkubwa. mikono yake kwanza kabla ya kuanza kula. 39Bwana akamwambia, “Usafi mnaoufanya ninyi Mafarisayo ni kama kusafisha kikombe au sahani kwa nje tu. Lakini ndani yenu mna nini? Mnataka kuwadanganya na kuwaumiza watu tu. 40Ninyi ni wajinga! Aliyeumba kilicho nje ndiye aliumba kilicho ndani. 41Hivyo, jalini vilivyo ndani. Wapeni vitu wenye uhitaji. Ndipo mtakuwa wasafi kikamilifu.
42Lakini, ole wenu ninyi Mafarisayo! Mnampa Mungu sehemu ya kumi ya vyakula mnavyopata, hata mnanaa, na hata kila mmea mdogo katika bustani#11:42 Mnampa … bustani Kwa maana ya kawaida, “Mnatoa zaka za mnanaa, mchicha na kila aina ya mboga za majani.” Sheria ya Musa iliwataka Waisraeli kushirikiana chakula kwa kutenga sehemu ya kumi ya mazao na mifugo yao kwa ajili ya Mungu (tazama Law 27:30-32; Kum 26:12). Hii haikujumuisha mazao madogo ya bustani kama yaliyotajwa hapa. Hivyo Mafarisayo hawa walikuwa wanatoa zaidi ya inavyotakiwa ili kuhakikisha kuwa hawavunji sheria. zenu. Lakini mnapuuzia kuwatendea haki wengine na kumpenda Mungu. Haya ni mambo mnayotakiwa kufanya. Na endeleeni kufanya mambo hayo mengine.
43Ole wenu ninyi Mafarisayo, kwa sababu mnapenda kupata viti vya heshima katika masinagogi. Na mnapenda kusalimiwa na watu kwa kuheshimiwa sehemu za masoko. 44Ole wenu, kwa kuwa mnafanana na makaburi ya zamani yasiyoonekana, ambayo watu hupita juu yake na kuyakanyaga bila kuyatambua.”
45Mmoja wa wanasheria akamwambia Yesu, “Mwalimu, unaposema mambo haya kuhusu Mafarisayo unatukosoa hata sisi pia.”
46Yesu akamjibu, “Ole wenu, enyi wanasheria! Mnatunga sheria kali ambazo ni vigumu watu kuzitii.#11:46 Mnatunga sheria kali … watu kuzitii Kwa maana ya kawaida, “Mnawatwisha watu mizigo wasiyoweza kuibeba.” Mnawalazimisha wengine kuzitii sheria zenu. Lakini ninyi wenyewe hamthubutu hata kujaribu kufuata mojawapo ya sheria hizo. 47Ole wenu kwa kuwa mnajenga makaburi ya manabii. Lakini hawa ni manabii wale wale ambao mababu zenu waliwaua. 48Na sasa mnawaonesha watu wote kwamba mnakubaliana na mambo ambayo baba zenu walifanya. Waliwaua manabii, nanyi mnasherehekea mauaji hayo kwa kujenga makaburi ya manabii! 49Hii ndiyo sababu ambayo kwa Hekima yake Mungu alisema, ‘Nitawatuma manabii na mitume#11:49 manabii na mitume Watu waliochaguliwa na Mungu kuhubiri Habari Njema ulimwenguni. kwao. Baadhi ya manabii na mitume wangu watauawa na watu waovu. Wengine watateswa sana.’
50Hivyo ninyi watu mnaoishi sasa mtaadhibiwa kwa sababu ya vifo vya manabii wote waliouawa tangu mwanzo wa ulimwengu. 51Mtachukuliwa wenye hatia kutokana na vifo hivyo vyote, tangu kuuawa kwa Habili mpaka kuuawa kwa nabii Zakaria,#11:51 Habili … Zakaria Katika Agano la Kale la Kiebrania, hawa ni watu wa kwanza na wa mwisho kuuawa. Tazama Mwa 4:8-11 na 2 Nya 24:20-25. aliyeuawa kati ya madhabahu na Hekalu. Ndiyo ninawaambia, kizazi hiki kitaadhibiwa kwa sababu yao wote.
52Ole wenu, ninyi wanasheria, mmechukua ufunguo wa kujifunza kuhusu Mungu. Ninyi wenyewe hamtaki kujifunza na mmewazuia wengine wasijifunze pia.”
53Yesu alipotoka humo, walimu wa sheria na Mafarisayo walianza kumpinga sana. Walianza kumjaribu ili awajibu maswali kuhusu mambo mengi, 54ili Yesu akisema jambo isivyo sahihi waweze kupata sababu ya kumkosoa.
ទើបបានជ្រើសរើសហើយ៖
Luka 11: TKU
គំនូសចំណាំ
ចែករំលែក
ចម្លង
ចង់ឱ្យគំនូសពណ៌ដែលបានរក្សាទុករបស់អ្នក មាននៅលើគ្រប់ឧបករណ៍ទាំងអស់មែនទេ? ចុះឈ្មោះប្រើ ឬចុះឈ្មោះចូល
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International