Yohana 6
6
Yesu Awalisha Watu Zaidi ya 5,000
(Mt 14:13-21; Mk 6:30-44; Lk 9:10-17)
1Baadaye, Yesu akavuka Ziwa Galilaya (ambalo pia linaitwa Ziwa Tiberia). 2Umati mkubwa wa watu ukamfuata kwa sababu waliona ishara za miujiza alizofanya kwa kuponya wagonjwa. 3Yesu akapanda mlimani na kukaa pale pamoja na wafuasi wake. 4Siku hizo sherehe ya Pasaka ya Wayahudi ilikuwa imekaribia.
5Yesu akainua macho yake na kuuona umati wa watu ukija kwake. Akamwambia Filipo, “Tunaweza kununua wapi mikate ya kuwatosha watu hawa wote?” 6Alimwuliza Filipo swali hili ili kumjaribu. Yesu alikwishajua kile alichopanga kufanya.
7Filipo akajibu, “Wote tunapaswa kufanya kazi kwa mwezi mmoja ili kununua mikate ya kutosha na kumpa kila mmoja aliyepo angalau kipande kidogo.”
8Mfuasi mwingine aliyekuwepo alikuwa Andrea, ndugu yake Simoni Petro. Andrea akasema, 9“Yupo hapa kijana mwenye mikate mitano ya shayiri na samaki wadogo wawili. Lakini hiyo haitoshi kwa umati huu wa watu.”
10Yesu akasema, “Mwambieni kila mtu akae chini.” Sehemu hiyo ilikuwa yenye nyasi nyingi, na wanaume wapatao 5,000 walikaa hapo. 11Yesu akaichukua ile mikate akamshukuru Mungu kwa ajili ya hiyo. Kisha akawapa watu waliokuwa wakisubiri kula. Alifanya vivyo hivyo kwa samaki. Akawapa watu kadiri walivyohitaji.
12Wote hao wakawa na chakula cha kutosha. Walipomaliza kula, Yesu akawaambia wafuasi wake, “Kusanyeni vipande vya samaki vilivyobaki na mikate ambayo haikuliwa. Msipoteze chochote.” 13Hivyo wakakusanya vipande vilivyobaki wakajaza vikapu 12 vikubwa vya mikate ya ngano iliyowabakia wale waliokula. Watu walikuwa wameanza kula wakiwa na vipande vitano tu vya mikate ya ngano.
14Watu waliiona ishara hii aliyoifanya Yesu na kusema, “Huyu atakuwa ndiye yule Nabii#6:14 Nabii Huenda walikuwa na maana nabii ambaye Mungu, alimwambia Musa ya kwamba atamtuma. Tazama Kum 18:15-19. anayekuja ulimwenguni!”
15Yesu akajua kwamba watu walipanga kuja kumchukua na kumfanya kuwa mfalme wao baada ya kuona muujiza alioufanya. Hivyo akaondoka na kwenda milimani peke yake.
Yesu Atembea Juu ya Maji
(Mt 14:22-27; Mk 6:45-52)
16Jioni ile wafuasi wake wakashuka kwenda ziwani. 17Ilikuwa giza sasa, wakati huo Yesu hakuwa pamoja na wafuasi wake. Wakapanda kwenye mashua na kuanza safari kuvuka ziwa kwenda Kapernaumu. 18Upepo ulikuwa unavuma kwa nguvu sana. Mawimbi ziwani yakawa makubwa. 19Wakaiendesha mashua kiasi cha kilomita tano au sita. Kisha wakamwona Yesu. Yeye alikuwa anatembea juu ya maji, akiifuata mashua. Nao wakaogopa. 20Lakini Yesu akawaambia, “Msiogope. Ni mimi.” 21Baada ya kusema hivyo, wakamkaribisha kwenye mashua. Kisha mashua ikafika ufukweni katika sehemu waliyotaka kwenda.
Watu Wamtafuta Yesu
22Siku iliyofuata watu wengi walikuwa wamekaa upande mwingine wa ziwa. Nao walijua kuwa Yesu hakwenda pamoja na wafuasi wake kwenye mashua. Kwani walifahamu kuwa wafuasi wake waliondoka na mashua peke yao. Walijua pia kuwa ile ilikuwa ni mashua pekee iliyokuwepo pale. 23Lakini baadaye mashua zingine kutoka Tiberia zilifika na kusimama karibu na mahali walipokula chakula jana yake. Hapo ni mahali pale walipokula mikate baada ya Yesu kushukuru. 24Watu wakaona kuwa Yesu na wafuasi wake hawakuwa hapo. Hivyo wakaingia katika mashua zao na kuelekea Kapernaumu kumtafuta Yesu.
Yesu, Mkate wa Uzima
25Watu wakamwona Yesu akiwa upande mwingine wa ziwa. Wakamwuliza, “Mwalimu, ulifika huku lini?”
26Akawajibu, “Kwa nini mnanitafuta? Ni kwa sababu mliona ishara na miujiza iliyotendeka? Ukweli ni kwamba, mnanitafuta kwa vile mlikula ile mikate mkashiba. 27Lakini chakula cha kidunia kinaharibika na hakidumu. Ninyi msifanye kazi ili kupata chakula cha aina hiyo kinachoharibika. Isipokuwa fanyeni kazi ili mpate chakula kinachodumu na kinachowapa uzima wa milele. Mwana wa Adamu atawapa hicho chakula. Yeye ndiye pekee aliyethibitishwa na Mungu Baba kuwapa.”
28Watu wakamwuliza Yesu, “Mungu anatutaka tufanye nini?”
29Yesu akajibu, “Kazi anayoitaka Mungu muifanye ni hii: kumwamini yule aliyemtuma.”
30Hivyo watu wakamwuliza, “Ni ishara gani utakayotufanyia? Ili nasi tutakapokuona unafanya ishara basi tukuamini? Je! utafanya nini? 31Baba zetu walipewa mana kula jangwani. Kama Maandiko yanavyosema, ‘Aliwapa mkate wa kula kutoka mbinguni.’”#Zab 78:24
32Yesu akasema, “Naweza kuwahakikishia kwamba Musa siye aliyewapa watu wenu mkate kutoka mbinguni. Bali Baba yangu huwapa ninyi mkate halisi unaotoka mbinguni. 33Mkate wa Mungu ni ule unaoshuka kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima.”
34Watu wakasema, “Bwana, kuanzia sasa na kuendelea tupe mkate wa aina hiyo.”
35Kisha Yesu akasema, “Mimi ndiye mkate unaoleta uzima. Hakuna anayekuja kwangu atakayehisi njaa. Hakuna anayeniamini atakayepata kiu kamwe. 36Nilikwisha kuwaambia mapema kuwa mmeona kile ambacho naweza kufanya,#6:36 kile ambacho naweza kufanya Au “mimi ninachoweza kufanya”, ambayo ipo katika nakala nyingi za Kiyunani, lakini haipo katika nakala mbili kati ya zile bora zaidi. lakini bado hamuniamini. 37Vyote anavyonipa Baba vitakuja kwangu hata hivyo yeyote Yule atakayekuja kwangu sitamkataa kabisa. Nami kwa hakika daima nitawapokea. 38Nilishuka kutoka mbinguni kuja kufanya yale Mungu anayopenda, siyo ninayoyapenda mimi. 39Nami sitampoteza hata mmoja wa wale alionipa Mungu. Bali nataka nimfufue katika siku ya mwisho. Haya ndiyo Baba yangu anayoyataka. 40Kila anayemtazama Mwana na kumwamini anao uzima wa milele. Nami nitamfufua katika siku ya mwisho. Hayo ndiyo anayoyataka Baba yangu.”
41Baadhi ya Wayahudi walianza kumlalamikia Yesu kwa vile alisema, “Mimi ni mkate unaoshuka kutoka mbinguni.” 42Wakasema, “Huyu ni Yesu. Tunawajua baba na mama yake. Yeye ni mtoto wa Yusufu. Anawezaje kusema, ‘Nilishuka kutoka mbinguni’?”
43Lakini Yesu akawaambia, “Acheni kunung'unika miongoni mwenu. 44Baba ndiye aliyenituma, na ndiye anayewaleta watu kwangu. Nami nitawafufua siku ya mwisho. Hakuna mtu anayeweza kuja kwangu asipoletwa na Baba yangu. 45Hii iliandikwa katika vitabu vya manabii: ‘Mungu atawafundisha wote.’#Isa 54:13 Watu humsikiliza Baba na hujifunza kutoka kwake. Hao ndiyo wanaokuja kwangu. 46Sina maana kwamba yupo yeyote aliyemwona Baba. Yule pekee aliyekwisha kumwona Baba ni yule aliyetoka kwa Mungu. Huyo amemwona Baba.
47Hakika nawaambieni kila anayeamini anao uzima wa milele. 48Maana mimi ni mkate unaoleta uzima. 49Baba zenu walikula mana waliyopewa na Mungu kule jangwani, lakini haikuwazuia kufa. 50Hapa upo mkate unaotoka mbinguni. Yeyote anayekula mkate huu hatakufa kamwe. 51Mimi ni mkate ulio hai ulioshuka kutoka mbinguni. Yeyote atakayeula mkate huu ataishi milele. Mkate huu ni mwili wangu. Nitautoa mwili wangu ili watu wa ulimwengu huu waweze kupata uzima.”
52Kisha Wayahudi hawa wakaanza kubishana wao kwa wao. Wakasema, “Yawezekanaje mtu huyu akatupa mwili wake tuule?”
53Yesu akasema, “Mniamini ninaposema kwamba mnapaswa kuula mwili wa Mwana wa Adamu, na mnapaswa kuinywa damu yake. Msipofanya hivyo, hamtakuwa na uzima wa kweli. 54Wale wanaoula mwili wangu na kuinywa damu yangu wanao uzima wa milele. Nitawafufua siku ya mwisho. 55Mwili wangu ni chakula halisi, na damu yangu ni kinywaji halisi. 56Wale waulao#6:56 waulao Kukaa kula Maana yake, “kutafuna kwa kelele” au “kutafuna kwa nguvu”. Ni neno la kufurahia kula, kunywa na ushirika baada ya mlo mkuu. Sehemu hii ya mlo pia ilijulikana kama “meza ya pili”. mwili wangu na kuinywa damu yangu wanaishi ndani yangu, nami naishi ndani yao.
57Baba alinituma. Yeye anaishi, nami naishi kwa sababu yake. Hivyo kila anayenila mimi ataishi kwa sababu yangu. 58Mimi siyo kama ule mkate walioula baba zenu. Wao waliula mkate huo, lakini bado walikufa baadaye. Mimi ni mkate uliotoka mbinguni. Yeyote atakayeula mkate huu ataishi milele.”
59Yesu aliyasema haya yote alipokuwa akifundisha kwenye Sinagogi katika mji wa Kapernaumu.
Wafuasi Wengi Wamwacha Yesu
60Wafuasi wa Yesu waliposikia haya, wengi wao wakasema, “Fundisho hili ni gumu sana. Nani awezaye kulipokea?”
61Yesu alikwishatambua kuwa wafuasi wake walikuwa wanalalamika juu ya hili. Hivyo akasema, “Je! fundisho hili ni tatizo kwenu? 62Ikiwa ni hivyo mtafikiri nini mtakapomwona Mwana wa Adamu akipanda kurudi kule alikotoka? 63Roho ndiye anayeleta uzima. Sio mwili. Lakini maneno niliyowaambia yanatoka kwa Roho, hivyo yanaleta uzima.” 64Lakini baadhi yenu hamuamini. (Yesu aliwafahamu wale ambao hawakuamini. Alijua haya tangu mwanzo. Na alimjua yule ambaye angemsaliti kwa adui zake.) 65Yesu akasema, “Ndiyo maana nilisema, ‘Hayupo hata mmoja ambaye anaweza kuja kwangu pasipo kusaidiwa na baba.’”
66Baada ya Yesu kusema mambo hayo, wafuasi wake wengi wakamkimbia na wakaacha kumfuata.
67Yesu akawauliza wale mitume kumi na wawili, “Nanyi pia mnataka kuondoka?”
68Simoni Petro akamjibu, “Bwana, tutaenda wapi? Wewe unayo maneno yanayoleta uzima wa milele. 69Sisi tunakuamini wewe. Tunafahamu kwamba wewe ndiye Yule Mtakatifu atokaye kwa Mungu.”
70Kisha Yesu akajibu, “Niliwachagua nyote kumi na wawili. Lakini mmoja wenu ni Ibilisi.” 71Alikuwa anazungumza juu ya Yuda, mwana wa Simoni Iskariote. Yuda alikuwa miongoni mwa mitume kumi na wawili, lakini baadaye angemkabidhi Yesu kwa adui zake.
ទើបបានជ្រើសរើសហើយ៖
Yohana 6: TKU
គំនូសចំណាំ
ចែករំលែក
ចម្លង
ចង់ឱ្យគំនូសពណ៌ដែលបានរក្សាទុករបស់អ្នក មាននៅលើគ្រប់ឧបករណ៍ទាំងអស់មែនទេ? ចុះឈ្មោះប្រើ ឬចុះឈ្មោះចូល
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International