Yohana 11
11
Kifo cha Lazaro
1Alikuwepo mtu aliyekuwa mgonjwa aliyeitwa Lazaro. Huyo aliishi katika mji wa Bethania, mahali ambapo Mariamu na dada yake Martha waliishi. 2(Mariamu ni mwanamke yule aliyempaka Bwana manukato na kumpangusa miguu kwa nywele zake.) Ndugu wa Mariamu alikuwa Lazaro, ambaye sasa alikuwa mgonjwa. 3Kwa hiyo Mariamu na Martha walimtuma mtu kwa Yesu kumwambia, “Bwana, rafiki yako mpendwa Lazaro ni mgonjwa.”
4Yesu aliposikia hayo alisema, “ugonjwa huu sio wa kifo. Isipokuwa, ugonjwa huu ni kwa ajili ya utukufu wa Mungu. Hili limetokea ili kuleta utukufu kwa Mwana wa Mungu.” 5Yesu aliwapenda Martha, na dada yake na Lazaro. 6Hivyo aliposikia kwamba Lazaro ni mgonjwa, akabaki alipokuwa kwa siku mbili zaidi, 7kisha akawaambia wafuasi wake, “Inatupasa kurudi tena Uyahudi.”
8Wakamjibu, “Lakini Mwalimu, ni muda mfupi tu uliopita viongozi wa Wayahudi pale walijitahidi kukuua kwa mawe. Sasa unataka kwenda huko tena?”
9Yesu akajibu, “Yako masaa kumi na mawili ya mchana katika siku. Yeyote anayetembea mchana hatajikwaa na kuanguka kwani anamulikiwa na nuru ya ulimwengu huu. 10Lakini yeyote anayetembea usiku atajikwaa kwa sababu hana nuru#11:10 nuru Hana chanzo cha nuru. inayomwongoza.”
11Kisha Yesu akasema, “Rafiki yetu Lazaro sasa amelala, lakini nitakwenda ili nimwamshe.”
12Wafuasi wake wakajibu, “Lakini, Bwana, kama amelala ataweza kupona.” 13Walifikiri kwamba Yesu alikuwa na maana kwamba Lazaro alikuwa amelala usingizi, lakini Yeye alikuwa na maana kuwa amefariki.
14Kisha hapo Yesu akasema wazi wazi, “Lazaro amekufa. 15Na ninafurahi sikuwepo hapo. Ninafurahi kwa ajili yenu kwa sababu sasa mtaniamini mimi. Twendeni kwake sasa.”
16Ndipo Tomaso, pia aliyeitwa “Pacha”, akawaambia wafuasi wengine, “Nasi pia tutaenda kule kufa pamoja na Yesu.”
Yesu Akiwa Bethania
17Yesu akaenda Bethania na huko akakuta Lazaro amekufa na kuwa kaburini kwa siku nne. 18Mji wa Bethania ulikuwa kama kilomita tatu#11:18 kilomita tatu Kwa maana ya kawaida, “stadia 15” ambazo ni kama umbali wa kilomita tatu hivi. kutoka Yerusalemu. 19Wayahudi wengi wakaja ili kuwaona Martha na Mariamu. Walikuja ili kuwafariji kwa ajili ya msiba wa kaka yao, Lazaro.
20Martha aliposikia kuwa Yesu alikuwa anakuja, alikwenda kumpokea. Lakini Mariamu alibaki nyumbani. 21Martha akamwambia Yesu, “Bwana, kama ungalikuwepo hapa, ndugu yangu asingelikufa. 22Lakini najua kwamba hata sasa Mungu atakupa chochote utakachomwomba.”
23Yesu akasema, “Kaka yako atafufuka na kuwa hai tena.”
24Martha akajibu, “Ninajua kuwa atafufuka tena wakati wa ufufuo siku ya mwisho.”
25Yesu akamwambia, “Mimi ndiye huo ufufuo. Mimi ndiye uzima. Kila anayeniamini atakuwa na uzima, hata kama atakufa. 26Kila atakayeniamini hatakufa kiroho hata kama atakufa kimwili. Je! Martha, unaliamini jambo hili?”
27Martha akajibu, “Ndiyo Bwana naliamini. Nakuamini kwamba wewe ni Masihi, Mwana wa Mungu. Ndiwe unayekuja ulimwenguni.”
Yesu Alia
28Baada ya Martha kusema maneno haya, alirejea kwa Mariamu dada yake. Aliongea naye peke yake na kusema, “Mwalimu yupo hapa. Anakutafuta.” 29Mariamu aliposikia hivyo, aliinuka na kwenda haraka kwa Yesu. 30Yesu hakuwa amefika kijijini. Alikuwa bado yupo pale pale Martha alipomkuta. 31Wayahudi waliokuwepo nyumbani hapo wakimfariji Mariamu walimwona akiinuka na kuondoka ghafla. Walifikiri alikuwa anaenda kaburini kuomboleza. Hivyo wakamfuata. 32Mariamu alienda pale Yesu alipokuwa. Naye baada ya kumwona, aliinama miguuni pake Yesu na kusema, “Bwana, kama ungekuwa hapa, kaka yangu asingekufa.”
33Ndipo Yesu alipomwona Mariamu na watu waliokuwa pamoja naye wakilia, akahuzunika na kusikitika sana. 34Akawauliza, “Mmemweka wapi?”
Wakasema, “Bwana, njoo uone.”
35Yesu akalia na kutoa machozi.
36Na Wayahudi wakasema, “Angalia! Alikuwa anampenda sana Lazaro!”
37Lakini wengine wao wakasema, “Yesu aliyeyaponya macho ya yule mtu asiyeona kwa nini hakumsaidia Lazaro na kumzuia asife?”
Yesu Amfufua Lazaro Kutoka Mautini
38Akiwa bado ana uchungu na kusikitika sana, Yesu akaenda kaburini. Kaburi lenyewe lilikuwa ni pango lenye jiwe kubwa lililofunika pa kuingilia. 39Yesu akasema, “Lisogezeni pembeni hilo jiwe.”
Martha akasema, “Lakini, Bwana, ni siku nne#11:39 siku nne Nyakati hizo Wayahudi wengi waliamini kuwa mtu akifa roho yake ilibaki pamoja na mwili kwa siku tatu. sasa tangu Lazaro alipofariki. Kutakuwa na harufu mbaya.” Martha alikuwa ni dada wa marehemu.
40Kisha Yesu akamwambia Martha, “Unakumbuka jinsi nilivyokuambia? Je! sikukuambia kwamba kama ukiamini, ungeuona utukufu wa Mungu?”
41Kwa hiyo wakalisogeza lile jiwe kutoka kwenye sehemu ya kuingilia. Kisha Yesu akatazama juu na kusema, “Baba, Nakushukuru kwa kuwa ulinisikia. 42Najua kuwa siku zote unanisikia. Lakini nimeyasema mambo haya kwa ajili ya watu walioko hapa. Nataka kwamba waweze kuamini kuwa ni wewe uliyenituma.” 43Baada ya Yesu kusema hivi akaita kwa sauti kubwa, “Lazaro, toka nje!” 44Yule mtu aliyekuwa amekufa akatoka nje, mikono na miguu yake ilikuwa imefungwa sanda. Uso wake ulikuwa umefunikwa kwa kitambaa.
Yesu akawaambia watu, “Mfungueni hizo sanda na kumwacha aende.”
Mpango wa Kumwua Yesu
(Mt 26:1-5; Mk 14:1-2; Lk 22:1-2)
45Walikuwepo Wayahudi wengi waliokuja kumtembelea Mariamu. Hawa walipoona aliyotenda Yesu, wengi wao wakamwamini. 46Lakini baadhi yao wakaenda kwa Mafarisayo na kuwapa habari ya mambo aliyofanya Yesu. 47Kisha viongozi wa makuhani na Mafarisayo wakaitisha kikao cha baraza kuu. Wakasema, “Tutafanyaje? Mtu huyu anafanya ishara nyingi sana. 48Tukimwacha aendelee kufanya hivi, kila mtu atamwamini. Ndipo Warumi watakuja na kulichukua Hekalu na Taifa letu pia.”
49Mmoja wa watu wale alikuwa ni Kayafa. Yeye alikuwa kuhani mkuu kwa mwaka ule. Akasema, “Ninyi hamjui lo lote! 50Ni bora mtu mmoja akafa kwa ajili ya watu wengine badala ya taifa zima kuangamia. Ninyi bado hamjalitambua hili.”
51Kayafa hakufikiri hivi peke yake. Hakika kama kuhani mkuu kwa mwaka ule, alikuwa akitabiri kwamba Yesu angekufa kwa ajili ya Wayahudi. 52Kweli, angekufa kwa ajili ya Wayahudi. Lakini pia angekufa kwa ajili ya watoto wa Mungu waliotawanyika ulimwenguni pote. Angekufa ili awakusanye na kuwaweka katika kundi moja.
53Siku ile viongozi wa Wayahudi wakaanza kupanga jinsi ya kumuua Yesu. 54Hivyo Yesu akaacha kusafiri wazi wazi katikati ya Wayahudi. Akaelekea katika mji ulioitwa Efraimu uliokuwa kwenye eneo karibu na jangwa. Akakaa huko pamoja na wafuasi wake.
55Wakati huo Sikukuu ya Pasaka ya Wayahudi ilikaribia. Watu wengi kutoka katika nchi yote ya Uyahudi wakaenda Yerusalemu siku chache kabla. Walienda kujitakasa tayari kwa ajili ya sikukuu hiyo. 56Watu wakamtafuta Yesu. Nao walisimama katika maeneo ya Hekalu na kuulizana, “Je! naye atakuja kwenye sikukuu? Unafikirije wewe?” 57Lakini viongozi wa makuhani na Mafarisayo walitoa agizo maalumu kuhusu Yesu. Walisema kuwa mtu yeyote anayejua mahali alipo Yesu awaambie ili waweze kumkamata.
ទើបបានជ្រើសរើសហើយ៖
Yohana 11: TKU
គំនូសចំណាំ
ចែករំលែក
ចម្លង
ចង់ឱ្យគំនូសពណ៌ដែលបានរក្សាទុករបស់អ្នក មាននៅលើគ្រប់ឧបករណ៍ទាំងអស់មែនទេ? ចុះឈ្មោះប្រើ ឬចុះឈ្មោះចូល
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International