Yohana MT. 14

14
1MSIFADHAIKE mioyo yenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi. 2Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambieni; nashika njia kwenda kuwaandalia mahali. 3Bassi nikishika njia kwenda kuwaandalia mahali, nitakuja tena, niwakaribisheni kwangu; illi nilipo mimi, nanyi mwepo. 4Na mimi niendako, mwaijua njia. 5Tomaso akamwambia, Bwana, hatujui uendako; twaijuaje njia? 6Yesu akamwambia, Ndimi niliye njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba bila kwa mimi. 7Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba; tangu sasa mnamjua, tena mmemwona. 8Filipo akamwambia, Bwana, tuonyeshe Baba, yatutosha. 9Yesu akamwambia, Nimekuwa pamoja nanyi siku hizi zote wala hukunijua, Filipo? Aliyeniona mimi, amemwona Baba; wasemaje wewe, Tuonyeshe Baba? 10Huamini ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba ndani yangu? Maneno niwaambiayo mimi, sisemi kwa shauri langu tu; lakini Baba akaae ndani yangu huzifanya kazi zake. 11Niaminini ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba ndani yangu; la! hamwamini hivyo, niaminini kwa sababu ya kazi zenyewe. 12Amin, amin, nawaambieni, Aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi na yeye atazifanya; atafanya na kubwa kuliko hizi, kwa kuwa nashika njia kwenda kwa Baba. 13Na mkiomba lo lote kwa jina langu, hili nitalifanya, Baba atukuzwe ndani ya Mwana. 14Mkiomba neno kwa jina langu, hili nitalifanya. 15Mkinipenda mtazishika amri zangu. 16Na mimi nitamwomba Baba, nae atawapa Mfariji mwingine, akaae nanyi hatta milele, 17Roho ya kweli; ambae ulimwengu hauwezi kumkubali, kwa kuwa haumwoni wala haumjui: bali ninyi mnamjua; maana anakaa kwenu, nae atakuwa ndani yenu. 18Sitawaacha ninyi yatima; naja kwenu. 19Bado kidogo na ulimwengu haunioni tena; bali ninyi mnaniona; kwa sababu mimi ni hayi, ninyi nanyi mtakuwa hayi. 20Katika siku ile mtajua ninyi, ya kuwa mimi ni ndani ya Baba yangu, na ninyi ndani yangu, na mimi ndani yenu. 21Aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendae; nae anipendae atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda, na kujidhihirisha kwake. 22Yuda akamwambia (siye Iskariote), Bwana, imekuwaje, ya kwamba wataka kujidhihirisha kwetu, wala si kwa ulimwengu? 23Yesu akajibu akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake. 24Asiyenipenda, hayashiki maneno yangu; na neno mnalolisikia silo langu, bali lake Baba aliyenipeleka. 25Haya nimewaambia, nikikaa kwenu. 26Lakini Mfariji, Roho Mtakatifu, ambae Baba atampeleka kwa jina langu, yeye atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia. 27Amani nawaachieni; amani yangu nawatolea; si kama ulimwengu utoavyo, mimi nawatolea. Msifadhaike moyo wenu, wala msiwe na woga. 28Mlisikia ya kwamba mimi naliwaambia, Nakwenda zangu, tena naja kwenu. Kama mngalinipenda, mngalifurahi, kwa sababu nashika njia kwenda kwa Baba: kwa maana Baba ni mkuu kuliko mimi. 29Na sasa nimewaambieni kabla haijawa, kusudi iwapo, mwamini. 30Sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana mkuu wa ulimwengu anakuja, wala hana kitu kwangu: 31lakini ulimwengu ujue ya kuwa nampenda Baba; na, kama Baba alivyoniamuru, ndivyo nifanyavyo. Ondokeni, tufoke huku.

Currently Selected:

Yohana MT. 14: SWZZB1921

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in