Yohana 1

1
Neno Alifanyika Mwili
1 Hapo mwanzo alikuwako Neno, huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. 2 Tangu mwanzo huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu.
3 Vitu vyote viliumbwa kwa yeye, wala pasipo yeye hakuna chochote kilichoumbwa ambacho kimeumbwa. 4 Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima na huo uzima ulikuwa nuru ya watu. 5 Nuru hung’aa gizani nalo giza halikuishinda.
6 Alikuja mtu mmoja aliyetumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yahya. 7 Alikuja kama shahidi apate kuishuhudia hiyo nuru, ili kwa kupitia kwake watu wote waweze kuamini. 8 Yeye mwenyewe hakuwa ile nuru, bali alikuja kuishuhudia hiyo nuru. 9 Kwamba nuru halisi, imwangaziayo kila mtu ilikuwa inakuja ulimwenguni.
10 Huyo Neno alikuwako ulimwenguni na ingawa ulimwengu uliumbwa kupitia kwake, haukumtambua. 11 Alikuja kwa walio wake, lakini wao hawakumpokea. 12 Bali wote waliompokea, aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake. 13 Hawa ndio wasiozaliwa kwa damu, wala kwa mapenzi ya mwili au kwa mapenzi ya mtu, bali kwa mapenzi ya Mungu.
14 Neno alifanyika mwili, akakaa miongoni mwetu, nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba,#1:14 Jina Baba linaonyesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. amejaa neema na kweli.
15 Yahya alishuhudia habari zake, akapaza sauti, akisema, “Huyu ndiye yule niliyewaambia kwamba, ‘Yeye ajaye baada yangu ni mkuu kuniliko mimi, kwa kuwa alikuwepo kabla yangu.’ ” 16 Kutokana na ukamilifu wake, sisi sote tumepokea neema juu ya neema. 17 Kwa kuwa sheria ilitolewa kwa mkono wa Musa, lakini neema na kweli imekuja kupitia Isa Al-Masihi. 18Hakuna mtu yeyote aliyemwona Mungu wakati wowote, ila ni Mungu Mwana pekee, aliye kifuani mwa Baba ndiye ambaye amemdhihirisha.
Ushuhuda Wa Yahya
(Mathayo 3:1-12; Marko 1:1-8; Luka 3:1-18)
19 Huu ndio ushuhuda wa Yahya wakati Wayahudi walipowatuma makuhani na Walawi kutoka Yerusalemu kumuuliza, “Wewe ni nani?” 20 Yahya alikiri waziwazi pasipo kuficha akasema, “Mimi si Al-Masihi.”
21 Wakamuuliza, “Wewe ni nani basi? Je, wewe ni Ilya?”
Yeye akajibu, “Hapana, mimi siye.”
“Je, wewe ni yule Nabii?”
Akajibu, “Hapana.”
22Ndipo wakasema, “Basi tuambie wewe ni nani ili tupate jibu la kuwapelekea wale waliotutuma. Wewe wasemaje juu yako mwenyewe?”
23 Akawajibu kwa maneno ya nabii Isaya, akisema, “Mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani, ‘Yanyoosheni mapito ya Mwenyezi Mungu.’ ”
24Basi walikuwa wametumwa watu kutoka kwa Mafarisayo,#1:24 Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli. 25 wakamuuliza, “Kama wewe si Al-Masihi, wala si Ilya na wala si yule Nabii, kwa nini basi unabatiza?#1:25 Ubatizo ni ishara ya kuungama dhambi na kusamehewa na Mwenyezi Mungu, na kuweka nadhiri ya kubadilisha mienendo ya awali.
26 Yahya akawajibu, “Mimi ninabatiza kwa maji,#1:26 Hapa tafsiri zingine zinasema ndani ya maji. lakini katikati yenu yupo mtu msiyemjua. 27 Yeye ajaye baada yangu, sistahili hata kufungua kamba za viatu vyake.”
28 Mambo haya yote yalitukia huko Bethania, ng’ambo ya Mto Yordani, mahali Yahya alipokuwa akibatiza.
Isa Mwana-Kondoo Wa Mungu
29 Siku iliyofuata, Yahya alimwona Isa akimjia akasema, “Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu! 30 Huyu ndiye yule niliyewaambia kwamba, ‘Mtu anakuja baada yangu ambaye ni mkuu kuniliko mimi, kwa kuwa alikuwepo kabla yangu.’ 31 Mimi mwenyewe sikumfahamu, lakini sababu ya kuja nikibatiza kwa maji ni ili yeye apate kufunuliwa kwa Israeli.”
32 Kisha Yahya akatoa ushuhuda huu: “Nilimwona Roho akishuka kutoka mbinguni kama hua, akakaa juu yake. 33 Mimi nisingemtambua, lakini yeye aliyenituma nibatize kwa maji alikuwa ameniambia, ‘Yule mtu utakayemwona Roho akimshukia na kukaa juu yake, huyo ndiye atakayebatiza kwa Roho wa Mwenyezi Mungu.’ 34 Mimi mwenyewe nimeona jambo hili na ninashuhudia kuwa huyu ndiye Mwana wa Mungu.#1:34 Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yn 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili.
Wanafunzi Wa Kwanza Wa Isa
35 Siku iliyofuata, Yahya alikuwa huko tena pamoja na wanafunzi wake wawili. 36 Alipomwona Isa akipita, akasema, “Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu!”
37Wale wanafunzi wawili walipomsikia Yahya akisema haya, wakamfuata Isa. 38 Isa akageuka, akawaona wakimfuata akawauliza, “Mnataka nini?”
Wakamwambia, “Mwalimu, unaishi wapi?”
39Isa akawajibu, “Njooni, nanyi mtapaona!”
Hivyo wakaenda na kupaona mahali alipokuwa anaishi, wakakaa naye siku ile, kwa kuwa ilikuwa yapata saa kumi.
40 Andrea nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa wale wawili waliosikia yale Yahya aliyokuwa amesema, naye ndiye alimfuata Isa. 41 Kitu cha kwanza Andrea alichofanya ni kumtafuta Simoni nduguye na kumwambia, “Tumemwona Masiya” (yaani, Al-Masihi). 42 Naye akamleta kwa Isa.
Isa akamwangalia na kusema, “Wewe ni Simoni mwana wa Yohana. Utaitwa Kefa” (ambalo limetafsiriwa Petro#1:42 Petro kwa Kiyunani au Kefa kwa Kiaramu; maana yake ni Kipande cha mwamba.).
Isa Awaita Filipo Na Nathanaeli
43 Siku iliyofuata Isa aliamua kwenda Galilaya. Akamkuta Filipo, akamwambia, “Nifuate.”
44 Basi Filipo alikuwa mwenyeji wa Bethsaida, mji alikotoka Andrea na Petro. 45 Filipo naye akamkuta Nathanaeli na kumwambia, “Tumemwona yeye ambaye Musa aliandika habari zake katika Torati na ambaye pia manabii waliandika kumhusu, yaani, Isa Al-Nasiri, mwana wa Yusufu.#1:45 Yusufu hakuwa baba mzazi wa Isa, bali alikuwa baba mlezi.
46 Nathanaeli akauliza, “Nasiri! Je, kitu chochote chema chaweza kutoka Nasiri?” Filipo akamwambia, “Njoo uone.”
47 Isa alipomwona Nathanaeli anakaribia, akanena habari zake akasema, “Tazama huyu ni Mwisraeli kweli kweli, hana hila ndani yake.”
48Nathanaeli akamuuliza, “Umenifahamuje?”
Isa akamjibu, “Nilikuona ulipokuwa bado uko chini ya mtini, kabla hata Filipo hajakuita.”
49 Nathanaeli akamwambia, “Mwalimu, wewe ni Mwana wa Mungu! Wewe ni Mfalme wa Israeli!”
50Isa akamwambia, “Unaamini kwa kuwa nilikuambia nilikuona ulipokuwa bado uko chini ya mtini? Basi utaona mambo makuu zaidi kuliko hilo.” 51 Ndipo akawaambia, “Amin, amin nawaambia, ninyi mtaona mbingu ikifunguka na malaika wa Mungu wakipanda na kushuka juu ya Mwana wa Adamu.”

選択箇所:

Yohana 1: NMM

ハイライト

シェア

コピー

None

すべてのデバイスで、ハイライト箇所を保存したいですか? サインアップまたはサインインしてください。