Mwanzo 5
5
Kutoka Adamu hadi Nuhu
(1 Nyakati 1:1-4)
1Hii ni orodha iliyoandikwa ya vizazi vya Adamu.
Mungu alipomuumba mwanadamu, alimfanya kwa sura ya Mungu. 2Aliwaumba mwanaume na mwanamke, akawabariki. Walipokwisha kuumbwa, akawaita “Binadamu.”
3Adamu alipokuwa ameishi miaka mia moja na thelathini, alimzaa mwana aliyekuwa na sura yake, mwenye kufanana naye. Akamwita jina Sethi. 4Baada ya Sethi kuzaliwa, Adamu aliishi miaka mia nane, akawa na watoto wengine wa kiume na wa kike. 5Adamu aliishi jumla ya miaka mia tisa na thelathini, ndipo akafa.
6Sethi alipokuwa ameishi miaka mia moja na tano, akamzaa Enoshi. 7Baada ya kumzaa Enoshi, Sethi aliishi miaka mia nane na saba (807), akawa na watoto wengine wa kiume na wa kike. 8Sethi aliishi jumla ya miaka mia tisa na kumi na mbili (912), ndipo akafa.
9Enoshi alipokuwa ameishi miaka tisini, akamzaa Kenani. 10Baada ya kumzaa Kenani, Enoshi aliishi miaka mia nane na kumi na tano (815), naye alikuwa na watoto wengine wa kiume na wa kike. 11Enoshi aliishi jumla ya miaka mia tisa na tano (905), ndipo akafa.
12Kenani alipokuwa ameishi miaka sabini, akamzaa Mahalaleli. 13Baada ya kumzaa Mahalaleli, Kenani aliishi miaka mia nane na arobaini, akawa na watoto wengine wa kiume na wa kike. 14Kenani aliishi jumla ya miaka mia tisa na kumi, ndipo akafa.
15Mahalaleli alipokuwa ameishi miaka sitini na tano, akamzaa Yaredi. 16Baada ya kumzaa Yaredi, Mahalaleli aliishi miaka mia nane na thelathini, akawa na watoto wengine wa kiume na wa kike. 17Mahalaleli aliishi jumla ya miaka mia nane tisini na tano (895), ndipo akafa.
18Yaredi alipokuwa ameishi miaka mia moja na sitini na mbili (162), akamzaa Idrisi. 19Baada ya kumzaa Idrisi, Yaredi aliishi miaka mia nane, naye akawa na watoto wengine wa kiume na wa kike. 20Yaredi aliishi jumla ya miaka mia tisa na sitini na mbili (962), ndipo akafa.
21Idrisi alipokuwa ameishi miaka sitini na tano, akamzaa Methusela. 22Baada ya kumzaa Methusela, Idrisi alitembea na Mungu miaka mia tatu, na akawa na watoto wengine wa kiume na wa kike. 23Idrisi aliishi jumla ya miaka mia tatu sitini na tano (365). 24Idrisi akatembea na Mungu, kisha akatoweka, kwa sababu Mungu alimchukua.
25Methusela alipokuwa ameishi miaka mia moja na themanini na saba (187), akamzaa Lameki. 26Baada ya kumzaa Lameki, Methusela aliishi miaka mia saba na themanini na mbili (782), akawa na watoto wengine wa kiume na wa kike. 27Methusela aliishi jumla ya miaka mia tisa sitini na tisa (969), ndipo akafa.
28Lameki alipokuwa ameishi miaka mia moja na themanini na mbili (182), alimzaa mwana. 29Akamwita jina Nuhu. Naye akasema, “Huyu ndiye atakayetufariji katika kazi ngumu ya mikono yetu yenye maumivu makali yaliyosababishwa na ardhi iliyolaaniwa na Mwenyezi Mungu.” 30Baada ya Nuhu kuzaliwa, Lameki aliishi miaka mia tano na tisini na tano (595), akawa na watoto wengine wa kiume na wa kike. 31Lameki aliishi jumla ya miaka mia saba sabini na saba (777), ndipo akafa.
32Baada ya Nuhu kuishi miaka mia tano, aliwazaa Shemu, Hamu, na Yafethi.
Biblica® Toleo Wazi Neno: Maandiko Matakatifu™ ONMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Biblica® Open Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.