Mwanzo 4

4
Kaini na Abeli#4:1-16 Simulizi hili linaendeleza kisa kilichoanzwa hapo nyuma katika sura iliyotangulia. Uasi wa binadamu dhidi ya Mungu (Mwa 3:6) hauwezi kuwa tukio la pekee la kupita tu. Kutokana na uasi huo unafuata mwenendo wa dhambi na uhalifu. Taz Yer 9:3 maelezo.
1Adamu akalala na Hawa mkewe, naye akapata mimba, akamzaa Kaini.#4:1 Kaini: Jina “Kaini” linatamkika kama kitenzi cha Kiebrania chenye maana ya “nimepata”. Hawa akasema, “Nimepata mtoto wa kiume kwa msaada wa Mwenyezi-Mungu!” 2Halafu akamzaa Abeli nduguye. Abeli alikuwa mfugaji kondoo na Kaini alikuwa mkulima.#4:2 Hapa tunapewa kazi mbili zinazotofautiana: mkulima na mfugaji. Inafahamika kwamba kulikuwa na mzozo kati ya wakulima na wafugaji (rejea Amu 6:3-6). Hata hivyo uhasama wa Kaini dhidi ya nduguye Abeli haukuwa kwa vile Abeli alikuwa mfugaji, bali kutokana na kukubaliwa na kukataliwa kwa matambiko yao kwa Mwenyezi-Mungu (rejea aya ya 5). 3Baada ya muda fulani, Kaini alimtolea Mwenyezi-Mungu sadaka kutokana na mazao ya shambani, 4naye Abeli akamtolea Mungu sadaka ya wazawa wa kwanza wa kondoo wake na nyama nono. Mwenyezi-Mungu akapendezwa na Abeli na tambiko yake, 5lakini hakupendezwa na Kaini wala na tambiko yake. Basi, Kaini akakasirika sana na uso wake ukakunjamana.#4:4-5 Kisa hiki hakioneshi kwa nini tambiko moja ilikubaliwa na nyingine kukataliwa. Katika Ebr 11:4 mwandishi wa barua hiyo anasema kwamba ni kwa sababu ya imani kwamba tambiko ya Abeli ilikubaliwa. 6Mwenyezi-Mungu akamwambia Kaini, “Kwa nini umekasirika, na kwa nini uso wako umekunjamana? 7Je, ukitenda vyema hutakubaliwa? Na usipotenda vyema, basi, dhambi inakuvizia mlangoni; inakutamani, lakini unapaswa kuishinda.”#4:7 Lakini unapaswa kuishinda: Kwa mara nyingine simulizi hili la Biblia linaonesha uwezekano wa binadamu kuchagua kwa hiari yake na kwa kuwajibika jambo jema au baya (taz Mwa 2:17 maelezo na pia Kumb 30:15-20). Msomaji anaweza kuona uhusiano uliopo kati ya onyo la Mwenyezi-Mungu kwa Kaini hapa na amri aliyowapa binadamu wa kwanza (Mwa 2:16-17). Kadiri ya simulizi lililotangulia, agizo la Mungu lilivunjwa kwa kutotii; kadiri ya simulizi hili, inahusu kosa la jinai. Kama vile katika kosa la hapo awali na katika kisa hiki, baada ya dhambi Mwenyezi-Mungu anawakabili wote kwa swali (Mwa 3:9 na 4:9), kisha adhabu (3:14-19; 4:11-12) na kufuata kitendo cha ishara cha huruma kutoka kwa Mwenyezi-Mungu ambacho kwa namna moja au nyingine kinapunguza uzito wa hizo adhabu (Mwa 3:21 na 4:15). Hayo ni mambo yanayoonekana kutokana na muundo wa maandishi.
8Baadaye, Kaini akamwambia Abeli nduguye, “Twende nje shambani.”#4:8 Twende nje shambani: Tafsiri kulingana na hati nyingine za kale. Maneno haya hayamo katika makala ya Kiebrania. Basi, walipokuwa shambani, Kaini akamvamia Abeli nduguye, akamuua. 9Mwenyezi-Mungu akamwuliza Kaini, “Ndugu yako Abeli yuko wapi?”#4:9 Ndugu yako Abeli yuko wapi?: Katika swali hili kuna uhusiano sambamba na swali katika Mwa 3:9. Katika visa hivyo viwili wanaoulizwa wanajaribu kuficha kuwajibika kwao kwa namna moja au nyingine. Kaini akamjibu, “Mimi sijui! Je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” 10Mwenyezi-Mungu akasema, “Umefanya nini?#4:10 Umefanya nini?: Linganisha swali hili na lile la Mwa 3:13. Damu ya ndugu yako yanililia#4:10 Damu ya ndugu yako yanililia: Taz Zab 9:12 maelezo. Uuaji wa mtu bila sababu za kutosha ni jinai na kitendo hicho kinapatilizwa. Rejea Eze 24:7-8. kutoka udongoni. 11Sasa wewe umelaaniwa! Hutailima tena ardhi yenye rutuba ambayo kama kinywa imeipokea damu ya nduguyo uliyemuua. 12Ukiilima ardhi haitakupatia tena mazao yake. Utakuwa mtu wa kutangatanga, asiye na makao maalumu duniani.”
13Kaini akamwambia Mwenyezi-Mungu, “Adhabu yangu ni kubwa mno; siwezi kuistahimili.#4:13 Kaini haoneshi majuto; anaona tu kwamba kosa lake la jinai linamtenga na Mungu na binadamu na kunung'unika kwamba mazingira yake yanamsababisha kutokuwa na usalama na ulinzi. 14Leo umenifukuza kutoka ardhi yenye rutuba na mbali nawe. Basi, nitakuwa mtu wa kutangatanga, asiye na makao maalumu duniani, na yeyote atakayeniona ataniua.” 15Lakini Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Sivyo! Atakayekuua wewe Kaini atalipizwa mara saba.”#4:15 Mara saba: Taz maelezo ya 4:23-24. Basi, Mwenyezi-Mungu akamtia Kaini alama ya tahadhari, ili yeyote atakayemwona asimuue.#4:15 Katika aya hii haisemwi hiyo ishara au alama ni ya namna gani. Lakini ni dhahiri kwamba alama hiyo ilimweka huyo mhalifu chini ya ulinzi wa Mungu na kuyakinga maisha yake. Rejea Eze 9:4-5. Taz pia Mwa 3:21 maelezo. 16Kisha Kaini akaondoka mbele ya Mwenyezi-Mungu, akawa anaishi katika nchi ya Nodi,#4:16 Nodi: Mahali au eneo lisilojulikana. Baadhi ya wafafanuzi wa Maandiko Matakatifu wanadhani jina hili linatumika kama mfano wa kugusia juu ya maisha ya kutangatanga (neno “Nad” Kiebrania lina maana ya “mwenye kutangatanga”). upande wa mashariki wa Edeni.
Wazawa wa Kaini#4:17-24 Orodha hii ya nasaba ina umuhimu wake hapa kwa vile ina shabaha ya kuunganisha asili ya binadamu (Mwa 1-11) na historia ya mababu wa Waisraeli (Mwa 12-50). Kwa mtindo huo inakuwa dhahiri kwamba Mungu alipojidhihirisha kwa Abrahamu na baadaye kwa taifa la Israeli ilikuwa ni mpango wake wa wokovu ambao utayahusu mataifa yote. Rejea Mwa 12:3; 26:4; 28:14.
17Kaini akalala na mkewe, naye akapata mimba, akamzaa Henoki. Kaini akajenga mji akauita kwa jina la Henoki mwanawe. 18Henoki akamzaa Iradi, naye Iradi akamzaa Mehuyaeli; Mehuyaeli akamzaa Methushaeli, naye Methushaeli akamzaa Lameki.#4:18 Sehemu ya kwanza ya nasaba hii ina vizazi saba, kuanzia Adamu mpaka Lameki. Idadi hiyo saba bila shaka inatumiwa kama mfano kwa vile huko Palestina na kwa jumla katika Mashariki ya Kati ya Kale idadi saba huwakilisha ukamilifu na utimilifu. Taz maelezo ya Mwa 4:23-24 na Zab 79:12. 19Lameki alioa wanawake wawili, mmoja aliitwa Ada na mwingine Sila. 20Ada alimzaa Yabali ambaye alikuwa baba yao wafugaji waishio mahemani. 21Ndugu yake alikuwa Yubali; huyo alikuwa baba yao wanamuziki wote wapigao zeze na filimbi. 22Sila naye alimzaa Tubal-kaini, ambaye alikuwa mhunzi wa vyombo vyote vya shaba na chuma. Dada yake Tubal-kaini alikuwa Naama.
23Lameki akawaambia wake zake,
“Ada na Sila sikieni sauti yangu!
Sikilizeni nisemayo enyi wake za Lameki.
Mimi niliua mtu kwa kunijeruhi,
naam, nilimuua kijana kwa kuniumiza.
24Ikiwa Kaini atalipizwa mara saba,
kweli Lameki atalipizwa mara sabini na saba.”#4:23-24 Shairi hili la Lameki linaonesha majivuno na ukatili wa mtu ambaye anakabili kitu kidogo alichokosewa kwa kulipiza kisasi bila mpaka. Maneno “mara sabini na saba” hutafsiriwa pengine kama: saba mara kumi na moja. Kwa matumizi zaidi ya tarakimu hiyo taz 4:18. Rejea pia Mat 18:21-22.
Sethi na Enoshi
25Adamu akalala tena na Hawa mkewe, naye akazaa mtoto wa kiume, akamwita Sethi akisema, “Mungu amenijalia mtoto mahali pa Abeli aliyeuawa na Kaini.” 26Sethi#4:26 Sethi: Jina hili Kiebrania linatamkika kama neno lenye maana ya “nimejaliwa”. naye alipata mtoto wa kiume, akamwita Enoshi.#4:26 Enoshi: Jina hili katika Kiebrania lina maana ya “mtu”. Hapo ndipo watu walipoanza kumwomba Mwenyezi-Mungu#4:26 Mwenyezi-Mungu: Taz maelezo ya 2:4. Hapa tunadokezewa kwamba jina hilo la Mwenyezi-Mungu lilikuwa la kale, kabla ya Mose. Taz pia maelezo ya Kut 3:13; 3:14; na 6:3. kwa jina lake.

選択箇所:

Mwanzo 4: BHNTLK

ハイライト

シェア

コピー

None

すべてのデバイスで、ハイライト箇所を保存したいですか? サインアップまたはサインインしてください。