Luka 17

17
Kujaribiwa ili kutenda dhambi
(Mathayo 18:6-7, 21-22; Marko 9:42)
1Isa akawaambia wanafunzi wake, “Mambo yanayosababisha watu watende dhambi hayana budi kutukia. Lakini ole wake mtu yule anayeyasababisha. 2Ingekuwa heri kama mtu huyo angefungiwa jiwe la kusagia shingoni na kutoswa baharini, kuliko kumsababisha mmoja wa hawa wadogo kutenda dhambi. 3Kwa hiyo, jilindeni.
“Ndugu yako akikukosea, mwonye; naye akitubu, msamehe. 4Akikukosea mara saba kwa siku moja, na mara saba kwa siku moja akaja kwako akisema, ‘Ninatubu,’ msamehe.”
Imani
5Mitume wake wakamwambia Bwana, “Tuongezee imani.”
6Bwana akawajibu, “Kama mngekuwa na imani ndogo kama punje ya haradali, mngeweza kuuambia mti huu wa mkuyu, ‘Ng’oka ukaote baharini,’ nao ungewatii.
Wajibu wa mtumishi
7“Ikiwa mmoja wenu ana mtumishi anayelima shambani au anayechunga kondoo, je, mtumishi huyo arudipo atamwambia, ‘Karibu hapa keti ule chakula’? 8Je, badala yake, hatamwambia, ‘Niandalie chakula, nile, jifunge unitumikie ninapokula na kunywa; baadaye unaweza kula na kunywa’? 9Je, huyo mtu atamshukuru mtumishi huyo kwa kutimiza yale aliyoamriwa? 10Vivyo hivyo nanyi mkishafanya mliyoagizwa, semeni, ‘Sisi tu watumishi tusiostahili; tumefanya tu yale tuliyopaswa kufanya.’ ”
Isa atakasa watu kumi wenye ukoma
11Isa alipokuwa njiani akienda Yerusalemu, alipitia mpakani mwa Samaria na Galilaya. 12Alipokuwa akiingia kwenye kijiji kimoja, watu kumi waliokuwa na ukoma wakakutana naye. Wakasimama mbali, 13wakapaza sauti, wakasema, “Isa, Bwana, tuhurumie!”
14Alipowaona akawaambia, “Nendeni mkajioneshe kwa makuhani.” Nao walipokuwa njiani wakienda, wakatakasika.
15Mmoja wao alipoona kwamba amepona, akarudi kwa Isa, akimsifu Mungu kwa sauti kuu. 16Akajitupa miguuni mwa Isa akamshukuru. Yeye alikuwa Msamaria.
17Isa akauliza, “Je, hawakutakaswa wote kumi? Wako wapi wale wengine tisa? 18Hakuna hata mmoja aliyeonekana kurudi ili kumshukuru Mungu isipokuwa huyu mgeni?” 19Isa akamwambia, “Inuka na uende zako, imani yako imekuponya.”
Kuja kwa Ufalme wa Mwenyezi Mungu
(Mathayo 24:23-28, 37-41)
20Isa alipoulizwa na Mafarisayo#17:20 Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli. ufalme wa Mungu utakuja lini, yeye akawajibu, “Ufalme wa Mungu hauji kwa kuchunguza kwa bidii, 21wala watu hawatasema, ‘Huu hapa,’ au ‘Ule kule,’ kwa maana ufalme wa Mungu umo ndani yenu.”
22Kisha Isa akawaambia wanafunzi wake, “Wakati utafika ambapo mtatamani kuiona moja ya siku ya Mwana wa Adamu, lakini hamtaiona. 23Watu watawaambia, ‘Yule kule!’ au, ‘Huyu hapa!’ Msiwakimbilie. 24Kwa maana kama vile radi imulikavyo katika anga kuanzia mwisho mmoja hadi mwingine, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu katika siku yake. 25Lakini kwanza itampasa kuteseka katika mambo mengi na kukataliwa na kizazi hiki.
26“Kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika siku za Mwana wa Adamu. 27Watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, hadi siku ile Nuhu alipoingia katika safina. Ndipo gharika ikaja na kuwaangamiza wote.
28“Ndivyo ilivyokuwa katika siku za Lutu: Watu walikuwa wakila na kunywa, wakinunua na kuuza, wakilima na kujenga. 29Lakini siku ile Lutu alipoondoka Sodoma, ikanyesha mvua ya moto na kiberiti kutoka mbinguni ukawaangamiza wote.
30“Hivyo ndivyo itakavyokuwa siku ile Mwana wa Adamu atakapofunuliwa. 31Siku hiyo, mtu yeyote aliye juu ya dari ya nyumba yake, hata vitu vyake vikiwa ndani ya hiyo nyumba, asishuke kuvichukua. Vivyo hivyo mtu aliye shambani asirudi nyumbani kuchukua chochote. 32Mkumbukeni mke wa Lutu! 33Mtu yeyote anayejaribu kuyaokoa maisha yake atayapoteza, na yeyote atakayeyapoteza maisha yake atayaokoa. 34Nawaambia, usiku huo watu wawili watakuwa wamelala kitanda kimoja; naye mmoja atatwaliwa na mwingine ataachwa. 35Wanawake wawili watakuwa wanasaga nafaka pamoja; naye mmoja atatwaliwa na mwingine ataachwa. [ 36Wanaume wawili watakuwa wanafanya kazi pamoja shambani; mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.]#17:36 Maandiko mengine ya kale hayana maneno haya.
37Kisha wakamuuliza, “Haya yatatukia wapi Bwana Isa?”
Akawaambia, “Pale ulipo mzoga, huko ndiko tai watakapokusanyika.”

वर्तमान में चयनित:

Luka 17: ONMM

हाइलाइट

शेयर

कॉपी

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in