1 Samueli 27
27
Daudi miongoni mwa Wafilisti
1Daudi akajisemea moyoni, “Siku moja, Shauli ataniangamiza. Jambo jema kwangu ni kukimbilia katika nchi ya Wafilisti. Shauli atakata tamaa kunitafuta ndani ya mipaka ya nchi ya Israeli, nami nitakuwa salama kutoka mikononi mwake.” 2Hivyo, mara moja Daudi na watu wake 600 wakaenda kwa Akishi mwana wa Maoki, mfalme wa Gathi. 3Daudi na watu wake pamoja na jamaa yake wakaishi na Akishi huko Gathi. Daudi alikuwa na wake wawili: Ahinoamu kutoka Yezreeli na Abigaili mjane wa Nabali kutoka mji wa Karmeli. 4Shauli aliposikia kwamba Daudi amekimbilia Gathi, hakumfuata tena.
5Siku moja, Daudi akamwambia Akishi, “Kama nimepata kibali mbele yako nakuomba unipe mji mmoja nchini mwako ili uwe mahali pangu pa kuishi. Hakuna haja kwangu kuishi nawe katika mji huu wa kifalme.” 6Siku hiyo, Akishi akampa mji wa Siklagi. Hivyo, tangu siku hiyo mji wa Siklagi umekuwa mali ya wafalme wa Yuda.
7Daudi aliishi katika nchi ya Wafilisti kwa muda wa mwaka mmoja na miezi minne. 8Katika muda huo, Daudi na watu wake waliwashambulia Wageshuri, Wagirizi na Waamaleki, ambao walikuwa wenyeji wa nchi hiyo tangu zamani. Aliwashambulia katika nchi yao mpaka Shuri, mpakani na Misri. 9Daudi aliipiga nchi hiyo asimwache hai mtu yeyote, awe mwanamume au mwanamke, akateka kondoo, ng'ombe, punda, ngamia na mavazi; kisha akarudi na kufika kwa Akishi. 10Akishi alipomwuliza, “Leo mashambulizi yako yalikuwa dhidi ya nani?” Daudi alimwambia, “Dhidi ya Negebu ya Yuda” au “Dhidi ya Negebu ya Wayerameeli” au “Dhidi ya Negebu ya Wakeni.” 11Daudi hakumwacha mtu yeyote hai awe mwanamume au mwanamke ili aletwe Gathi; alifikiri moyoni: “Wanaweza wakaeleza juu yetu na kusema, ‘Daudi alifanya kitendo hiki na kile.’” Hivyo ndivyo Daudi alivyozoea kutenda wakati wote alipoishi katika nchi ya Wafilisti. 12Kwa hiyo, Akishi alimsadiki Daudi, akifikiri, “Wananchi wenzake Waisraeli hawampendi kabisa; kwa hiyo, atanitumikia maisha yake yote.”
Currently Selected:
1 Samueli 27: BHN
Highlight
Share
Copy
Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in
Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.