YouVersion Logo
Search Icon

Luka 16

16
Mfano wa msimamizi mjanja
1Isa akawaambia wanafunzi wake, “Palikuwa na tajiri mmoja na msimamizi wake. Huyo msimamizi alishitakiwa kwake kwamba alikuwa akitapanya mali ya tajiri yake. 2Hivyo huyo tajiri akamwita na kumuuliza, ‘Ni mambo gani haya ninayoyasikia kukuhusu? Toa taarifa ya usimamizi wako, kwa sababu huwezi kuendelea kuwa msimamizi.’
3“Yule msimamizi akawaza moyoni mwake, ‘Nitafanya nini sasa? Bwana wangu ananiondoa katika kazi yangu. Sina nguvu za kulima, nami ninaona aibu kuombaomba. 4Najua nitakalofanya ili nikiachishwa kazi yangu hapa, watu wanikaribishe nyumbani mwao.’
5“Kwa hiyo akawaita wadeni wote wa bwana wake, mmoja mmoja. Akamuuliza wa kwanza, ‘Deni lako kwa bwana wangu ni kiasi gani?’
6“Akajibu, ‘Vipimo mia moja#16:6 ni kama lita elfu nne vya mafuta ya mizeituni.’
“Msimamizi akamwambia, ‘Chukua hati ya deni lako, ibadilishe upesi, uandike vipimo hamsini.’
7“Kisha akamuuliza wa pili, ‘Wewe deni lako ni kiasi gani?’
“Akajibu, ‘Vipimo elfu moja#16:7 ni kama magunia mia moja vya ngano.’
“Yule msimamizi akamwambia, ‘Chukua hati yako, uandike vipimo mia nane!’
8“Yule bwana akamsifu yule msimamizi dhalimu kwa jinsi alivyotumia ujanja. Kwa maana watu wa dunia hii wana ujanja zaidi wanapojishughulisha na mambo ya dunia kuliko watu wa nuru. 9Nawaambia, tumieni mali ya dunia kujipatia rafiki, ili itakapokwisha, mkaribishwe katika makao ya milele.
10“Yeyote aliye mwaminifu katika mambo madogo, pia ni mwaminifu katika mambo makubwa. Na yeyote asiye mwaminifu katika mambo madogo pia si mwaminifu katika mambo makubwa. 11Ikiwa hamkuwa waaminifu katika mali ya kidunia, ni nani atakayewaaminia mali ya kweli? 12Nanyi kama hamkuwa waaminifu na mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewapa iliyo yenu wenyewe?
13“Hakuna mtumishi awezaye kuwatumikia mabwana wawili. Kwa kuwa atamchukia huyu na kumpenda yule mwingine, au atashikamana sana na huyu na kumdharau yule mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu pamoja na Mali#16:13 au Utajiri; yaani Mamoni kwa Kiaramu au Mamona kwa Kiyunani.”
14Mafarisayo, waliokuwa wapenda fedha, waliyasikia hayo yote na wakamcheka kwa dharau. 15Isa akawaambia, “Ninyi mnajionesha kuwa wenye haki mbele za wanadamu, lakini Mungu anaijua mioyo yenu. Kwa maana vile vitu ambavyo wanadamu wanavithamini sana, kwa Mungu ni machukizo.
Torati na Ufalme wa Mwenyezi Mungu
16“Torati na Manabii vilihubiriwa hadi kuja kwa Yahya. Tangu wakati huo Injili ya ufalme wa Mungu inahubiriwa, na kila mmoja hujiingiza kwa nguvu. 17Lakini ni rahisi zaidi mbingu na dunia kupita kuliko hata herufi moja kuondoka katika Torati.
18“Mtu yeyote amwachaye mkewe na kumwoa mwanamke mwingine anazini, naye mwanaume amwoaye mwanamke aliyetalikiwa anazini.
Tajiri na Lazaro
19“Palikuwa na mtu mmoja tajiri aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, ambaye aliishi kwa anasa kila siku. 20Hapo penye mlango wake aliishi maskini mmoja, jina lake Lazaro, mwenye vidonda mwili mzima. 21Huyo Lazaro alitamani kujishibisha kwa makombo yaliyoanguka kutoka mezani kwa yule tajiri. Hata mbwa walikuwa wakija na kuramba vidonda vyake.
22“Wakati ukafika yule maskini akafa, nao malaika wakamchukua akae pamoja na Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa na akazikwa. 23Kule Kuzimu#16:23 Kuzimu kwa Kiyunani ni Hades, yaani mahali pa wafu. alipokuwa akiteseka, alitazama juu, akamwona Ibrahimu kwa mbali, naye Lazaro alikuwa kifuani mwake. 24Hivyo yule tajiri akamwita, ‘Baba Ibrahimu, nihurumie na umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake ndani ya maji aupoze ulimi wangu, kwa sababu nina maumivu makuu kwenye moto huu.’
25“Lakini Ibrahimu akamjibu, ‘Mwanangu, kumbuka kwamba wakati wa uhai wako ulipata mambo mazuri, lakini Lazaro alipata mambo mabaya. Lakini sasa anafarijiwa hapa na wewe uko katika maumivu makuu. 26Zaidi ya hayo, kati yetu na ninyi huko kumewekwa shimo kubwa, ili wale wanaotaka kutoka huku kuja huko wasiweze, wala mtu yeyote asiweze kuvuka kutoka huko kuja kwetu.’
27“Akasema, ‘Basi, nakuomba, umtume Lazaro aende nyumbani mwa baba yangu, 28maana ninao ndugu watano. Awaonye, ili wasije nao wakafika mahali hapa pa mateso.’
29“Ibrahimu akamjibu, ‘Ndugu zako wana Maandiko ya Musa na Manabii, wawasikilize hao.’
30“Yule tajiri akasema, ‘Hapana, baba Ibrahimu, lakini mtu kutoka kwa wafu akiwaendea, watatubu.’
31“Ibrahimu akamwambia, ‘Kama wasipowasikiliza Musa na Manabii, hawataweza kushawishika hata kama mtu akifufuka kutoka kwa wafu.’ ”

Currently Selected:

Luka 16: NENO

Highlight

Share

Copy

None

Want to have your highlights saved across all your devices? Sign up or sign in