Yohana 1

1
Utangulizi
(Yohana 1:1-18)
Neno alifanyika mwili
1Hapo mwanzo alikuwako Neno, naye huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. 2Tangu mwanzo huyo Neno alikuwa pamoja na Mungu.
3Vitu vyote viliumbwa kupitia kwake, na hakuna chochote kilichoumbwa ambacho kimeumbwa pasipo yeye. 4Ndani yake kulikuwa na uzima, nao huo uzima ulikuwa nuru ya watu. 5Nuru hung’aa gizani nalo giza halikuishinda.
6Alikuja mtu mmoja aliyetumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yahya. 7Alikuja kama shahidi apate kuishuhudia hiyo nuru, ili kupitia kwake watu wote waweze kuamini. 8Yeye mwenyewe hakuwa ile nuru, bali alikuja kuishuhudia hiyo nuru.
9Nuru halisi inayomwangazia kila mtu ilikuwa inakuja ulimwenguni. 10Huyo Neno alikuwako ulimwenguni, na ingawa ulimwengu uliumbwa kupitia kwake, haukumtambua. 11Alikuja kwa walio wake, lakini wao hawakumpokea. 12Bali wote waliompokea, yaani wale walioliamini jina lake, aliwapa uwezo wa kufanyika wana wa Mungu. 13Hawa hawakuzaliwa kwa damu, wala kwa mapenzi ya mwili au kwa mapenzi ya mtu, bali wamezaliwa kwa mapenzi ya Mungu.
14Neno alifanyika mwili, akakaa miongoni mwetu, nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba#1:14 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu., amejaa neema na kweli.
15Yahya alishuhudia habari zake, akapaza sauti, akisema, “Huyu ndiye yule niliyewaambia kwamba, ‘Yeye ajaye baada yangu ni mkuu kuliko mimi, kwa kuwa alikuwa kabla yangu.’ ” 16Kutokana na ukamilifu wake, sisi sote tumepokea neema juu ya neema. 17Kwa kuwa sheria ilitolewa kwa mkono wa Musa, lakini neema na kweli zimekuja kupitia Isa Al-Masihi. 18Hakuna mtu yeyote aliyemwona Mungu wakati wowote, ila ni Mungu Mwana pekee, aliye kifuani mwa Baba, ndiye ambaye amemdhihirisha.
Huduma ya Isa kabla ya kurudi Galilaya
(Yohana 1:19–4:54)
Ushuhuda wa Yahya
(Mathayo 3:1-12; Marko 1:1-8; Luka 3:1-18)
19Huu ndio ushuhuda wa Yahya wakati viongozi wa Wayahudi waliwatuma makuhani na Walawi kutoka Yerusalemu kumuuliza, “Wewe ni nani?” 20Yahya alikiri waziwazi pasipo kuficha, akasema, “Mimi si Al-Masihi#1:20 Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta..”
21Wakamuuliza, “Wewe ni nani, basi? Je, wewe ni Ilya?”
Yeye akajibu, “Hapana, mimi siye.”
“Je, wewe ni yule Nabii?”
Akajibu, “Hapana.”
22Ndipo wakasema, “Basi tuambie wewe ni nani ili tupate jibu la kuwapelekea wale waliotutuma. Wewe wasemaje juu yako mwenyewe?”
23Akawajibu kwa maneno ya nabii Isaya, akisema, “Mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani, ‘Yanyoosheni mapito ya Mwenyezi Mungu.’ ”
24Basi walikuwa wametumwa watu kutoka kwa Mafarisayo#1:24 Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli., 25wakamuuliza, “Kama wewe si Al-Masihi, wala si Ilya na wala si yule Nabii, kwa nini basi unabatiza#1:25 Ubatizo ni ishara ya kuungama dhambi na kusamehewa na Mwenyezi Mungu, na kuweka nadhiri ya kubadilisha mienendo ya awali.?”
26Yahya akawajibu, “Mimi ninabatiza kwa maji#1:26 au ndani ya maji, lakini kati yenu yupo mtu msiyemjua. 27Yeye anakuja baada yangu, nami sistahili hata kufungua kamba za viatu vyake.”
28Mambo haya yote yalitukia huko Bethania, ng’ambo ya Yordani, mahali Yahya alipokuwa akibatiza.
Mwana-Kondoo wa Mwenyezi Mungu
29Siku iliyofuata, Yahya alimwona Isa akimjia, akasema, “Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu! 30Huyu ndiye yule niliyewaambia kwamba, ‘Mtu anakuja baada yangu ambaye ni mkuu kuliko mimi, kwa kuwa alikuwa kabla yangu.’ 31Mimi mwenyewe sikumfahamu, lakini sababu ya kuja nikibatiza kwa maji ni ili yeye apate kufunuliwa kwa Israeli.”
32Kisha Yahya akatoa ushuhuda huu: “Nilimwona Roho Mtakatifu wa Mungu akishuka kutoka mbinguni kama hua, akakaa juu yake. 33Mimi nisingemtambua, lakini yeye aliyenituma nibatize kwa maji alikuwa ameniambia, ‘Yule mtu utakayemwona Roho Mtakatifu wa Mungu akimshukia na kukaa juu yake, huyo ndiye atakayebatiza kwa Roho wa Mungu.’ 34Mimi mwenyewe nimeona jambo hili na ninashuhudia kuwa huyu ndiye Mwana wa Mungu#1:34 Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yohana 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili..”
Wanafunzi wa kwanza wa Isa
(Mathayo 4:18-22; Marko 1:16-20; Luka 5:1-11)
35Siku iliyofuata, Yahya alikuwa huko tena pamoja na wanafunzi wake wawili. 36Alipomwona Isa akipita, akasema, “Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu!”
37Wale wanafunzi wawili walipomsikia Yahya akisema haya, wakamfuata Isa. 38Isa akageuka, akawaona wakimfuata, akawauliza, “Mnataka nini?”
Wakamwambia, “Mwalimu, unaishi wapi?”
39Isa akawajibu, “Njooni, nanyi mtapaona!”
Hivyo wakaenda na kupaona mahali alipokuwa anaishi, wakakaa naye siku ile, kwa kuwa ilikuwa yapata saa kumi.
40Andrea, nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa wale wawili waliosikia yale Yahya alisema na kumfuata Isa. 41Kitu cha kwanza Andrea alichofanya ni kumtafuta Simoni nduguye na kumwambia, “Tumemwona Masihi” (yaani Al-Masihi). 42Naye akamleta kwa Isa.
Isa akamwangalia na kusema, “Wewe ni Simoni mwana wa Yohana. Utaitwa Kefa” (ambalo limetafsiriwa Petro#1:42 Petro kwa Kiyunani au Kefa kwa Kiaramu; maana yake Kipande cha mwamba.).
43Siku iliyofuata Isa aliamua kwenda Galilaya. Akamkuta Filipo, akamwambia, “Nifuate.”
44Filipo alikuwa raia wa Bethsaida, mji walikotoka Andrea na Petro. 45Filipo naye akamkuta Nathanaeli na kumwambia, “Tumemwona yeye ambaye Musa aliandika habari zake katika Torati, na ambaye pia manabii waliandika kumhusu, yaani Isa Al-Nasiri, mwana wa Yusufu#1:45 Yusufu hakuwa baba mzazi wa Isa, bali alikuwa baba mlezi..”
46Nathanaeli akauliza, “Nasiri! Je, kitu chochote chema chaweza kutoka Nasiri?”
Filipo akamwambia, “Njoo uone.”
47Isa alipomwona Nathanaeli anakaribia, akanena habari zake, akasema, “Tazama huyu ni Mwisraeli kweli kweli; hana hila ndani yake.”
48Nathanaeli akamuuliza, “Umenifahamuje?”
Isa akamjibu, “Nilikuona ulipokuwa bado uko chini ya mtini, kabla hata Filipo hajakuita.”
49Nathanaeli akamwambia, “Mwalimu, wewe ni Mwana wa Mungu! Wewe ni Mfalme wa Israeli!”
50Isa akamwambia, “Unaamini kwa kuwa nilikuambia nilikuona ulipokuwa bado uko chini ya mtini? Basi utaona mambo makuu kuliko hilo.” 51Ndipo akawaambia, “Amin, amin nawaambia, ninyi mtaona mbingu ikifunguka na malaika wa Mungu wakipanda na kushuka juu ya Mwana wa Adamu.”

Valgt i Øjeblikket:

Yohana 1: ONMM

Markering

Del

Kopiér

None

Vil du have dine markeringer gemt på tværs af alle dine enheder? Tilmeld dig eller log ind