Luka MT. 20
20
1IKAWA siku moja, alipokuwa akiwafundisha watu hekaluni na kuikhubiri Injili, makuhani wakuu na waandishi, na pamoja nao wazee, wakamtokea ghafula, 2wakasema nae, wakinena, Kwa mamlaka gani unatenda haya? Na ni nani aliyekupa mamlaka hii? 3Akajibu, akawaambia, Nami nitawauliza ninyi neno moja, kaniambieni. 4Ubatizo wa Yohana, ulitoka mbinguni au kwa wana Adamu? 5Wakasemezana wao kwa wao, wakinena, Kama tukisema, Toka mbinguni, atasema, Mbona hamkumwamini bassi? 6Bali tukisema, Kwa wana Adamu, watu wote watatupiga mawe: kwa sababu wamesadiki ya kuwa Yohana ni nabii. 7Wakajibu kwamba, Hatujui atokako. 8Yesu akawaambia, Wala mimi siwaambii ninyi ni kwa mamlaka gani ninatenda haya.
9Akaanza kuwaambia watu mfano huu: Mtu alipanda mizabibu, akapangisha wakulima, akaenda inchi nyingine kwa muda wa siku nyingi. 10Na wakati wa mavuno akatuma mtumishi kwa wale wakulima illi wampe baadhi ya matunda ya mizabibu, wakulima wakampiga, wakamtoa hana kitu. 11Akaongeza akampeleka mtumishi mwingine, wakampiga huyu wakamfedhehesha, wakamtoa hana kitu. 12Akaongeza akampeleka wa tatu, wakamtia jeraha, wakamfukuza. 13Yule Bwana wa mizabibu akasema, Nifanyeje? Nitampeleka mwana wangu, mpendwa wangu, labuda wakimwona yeye watamheshimu. 14Lakini wale wakulima, walipomwona, wakafanya shauri wao kwa wao, wakinena, Huyu ndiye mrithi; na tumwue bassi, urithi upate kuwa wetu. 15Wakamtupa nje ya shamba la mizabibu wakamwua. Bassi yule bwana wa shamba la mizabibu atawatendani? 16Atakuja na kuwaangamiza wale wakulima, na lile shamba la mizabibu atawapa wengine. 17Waliposikia wakasema, Mungu na apishe mbali. Akawakazia macho, akasema, Maana yake nini, bassi, neno hili lililoandikwa,
Jiwe walilolikataa waashi
Hili limekuwa jiwe kuu la pembeni?
18Killa mtu aangukae juu ya jiwe hilo atavunjikavunjika, nae ambae litamwangukia litamsagasaga.
19Makuhani wakuu na waandishi wakatafuta kumkamata saa hiyo hiyo, wakawaogopa watu: maana walitambua ya kuwa ule mfano amewanena wao.
20Wakamvizia wakatuma wapelelezi, nao wakajifanya kuwa wenye haki, illi wamnase kwa neno lake, kusudi wamtie katika enzi na mamlaka ya liwali. 21Wakamwuliza, wakinena, Mwalimu, twajua ya kuwa wanena yaliyo kweli na kuyafundisha, wala hujali cheo cha mtu, bali katika kweli waifundisha njia ya Mungu: 22Je! ni halali kumpa Kaisari kodi au sivyo? 23Lakini akatambua ujanja wao, akawaambia, 24Nionyesheni dinari: ina sura ya nani? ina anwaui ya nani? Wakasema, ya Kaisari. 25Akawaambia, Bassi, mpeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na Mungu yaliyo ya Mungu. 26Wala hawakuweza kumshika kwa neno lake mbele ya watu: wakastaajabia jawabu lake, wakanyamaza.
27Kiisha baadhi ya Masadukayo wakamwendea, watu wanenao ya kwamba hakuna kiyama: wakamwuliza, wakinena, 28Mwalimu, Musa alituandikia ya kama ndugu ya mtu akifa, nae ana mke, na mtu huyo akifa hana mtoto, ni lazima ndugu yake amtwae yule mke, akampatie ndugu yake mzao. 29Bassi, palikuwa na ndugu saba: wa kwanza akatwaa mke akafa, hana mtoto, 30wa pili akamtwaa yule mke, akafa nae, hana mtoto. 31Hatta wa tatu akamtwaa, na kadhalika hawa saba hawakuacha watoto, wakafa. 32Mwisho wa hawo wote yule mwanamke akafa nae. 33Bassi katika kiyama, atakuwa mke wa nani katika hawo? maana wale saba walikuwa nae. 34Yesu akajibu akawaambia, Wana wa ulimwengu huu huoa, na kuozwa, 35bali wao watakaohesabiwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na ufufuo wa wafu, hawaoi wala hawaozwi, 36kwa kuwa hawawezi kufa tena, maana huwa sawasawa na malaika; tena ni wana wa Mungu kwa kuwa wana wa ule ufufuo. 37Walakini ya kuwa wafu wafufuka, Musa nae alionyesha katika sura ya Kijiti, hapo amtajapo Bwana kuwa ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaak, na Mungu wa Yakobo. 38Bassi, yeye siye Muugu wa wafu, bali Mungu wa wahayi, maana wote ni wahayi kwake. 39Baadhi ya waandishi wakajibu wakasema, Mwalimu, umesema vema. 40Wala hakuthubutu mtu kumwuliza neno baada ya haya. 41Akawaambia, Kwa maana gani hunena ya kwamba Kristo yu mwana wa Daud? 42Na Daud mwenyewe asema katika chuo cha Zaburi,
Bwana alimwambia Bwana wangu,
Keti mkono wangu wa kuume,
43Hatta niwafanyapo adui zako kuwa chini ya miguu yako.
44Daud, bassi, amwita Bwana, na amekuwaje Mwana wake? 45Hatta watu wote walipokuwa wakimsikiliza, akawaambia wanafunzi wake, 46Jihadharini na waandishi wapendao kutembea wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa masokoni, na kuketi mbele katika sunagogi, na mahali palipo mbele katika karamu. 47Wanakula nyumba za wajane: na kwa unafiki husali sala ndefu. Hawo watapokea hukumu iliyo kubwa zaidi.
Valgt i Øjeblikket:
Luka MT. 20: SWZZB1921
Markering
Del
Kopiér
Vil du have dine markeringer gemt på tværs af alle dine enheder? Tilmeld dig eller log ind
Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.