Mathayo 2
2
Wenye Hekima Waja Kumwona Yesu
1Yesu alizaliwa katika mji wa Bethlehemu ya Uyahudi wakati Herode alipokuwa mfalme. Baada ya Yesu kuzaliwa, baadhi ya wenye hekima kutoka mashariki walikuja Yerusalemu. 2Walipofika wakawauliza watu, “Yuko wapi mtoto aliyezaliwa ili awe Mfalme wa Wayahudi? Tuliiona nyota ilipochomoza na kutuonesha kuwa amezaliwa. Nasi tumekuja ili tumwabudu.”
3Mfalme Herode aliposikia haya, yeye pamoja na watu wote wakaao Yerusalemu walikasirika sana. 4Herode aliitisha mkutano wa wakuu wote wa makuhani wa Kiyahudi na walimu wa sheria. Akawauliza ni wapi ambapo Masihi angezaliwa. 5Wakamjibu, “Ni katika mji wa Bethlehemu ya Yuda kama ambavyo nabii aliandika:
6‘Bethlehemu, katika nchi ya Yuda,
wewe ni wa muhimu miongoni mwa watawala wa Yuda.
Ndiyo, mtawala atakayewaongoza
watu wangu Israeli, atatoka kwako.’”#Mik 5:2
7Kisha Herode akawaita na kufanya mkutano wa siri na wenye hekima kutoka mashariki. Akaelewa kwa usahihi wakati walipoiona nyota. 8Kisha akawaruhusu waende Bethlehemu. Akawaambia, “Nendeni mkamtafute mtoto kwa makini na mtakapompata mrudi na kunipa taarifa mahali alipo, ili nami pia niende kumwabudu.”
9Wenye hekima walipomsikiliza mfalme, waliondoka. Waliiona tena ile nyota waliyoiona hapo mwanzo na wakaifuata. Nyota ile iliwaongoza mpaka mahali alipokuwa mtoto na kusimama juu ya sehemu hiyo. 10Wenye hekima walipoona kuwa nyota ile imesimama, walifurahi na kushangilia kwa furaha.
11Wenye hekima hao kisha waliingia katika nyumba alimokuwamo mtoto Yesu pamoja na Mariamu mama yake. Walisujudu na kumwabudu mtoto. Kisha wakafungua masanduku yenye zawadi walizomletea mtoto. Wakampa hazina za dhahabu, uvumba na manemane. 12Lakini Mungu aliwaonya wenye hekima hao katika ndoto kuwa wasirudi tena kwa Herode. Hivyo kwa kutii walirudi nchini kwao kwa kupitia njia nyingine.
Yesu Apelekwa Uhamishoni Misri
13Baada ya wenye hekima kuondoka, malaika wa Bwana akamjia Yusufu katika ndoto na kumwambia, “Damka! Mchukue mtoto pamoja na mama yake ukimbilie Misri kwa sababu Herode amedhamiria kumwua mtoto na sasa atatuma watu kumtafuta. Na mkae Misri mpaka nitakapowaambia mrudi.”
14Hivyo Yusufu alidamka na kutoka kwenda Misri akiwa na mtoto na mama yake. Nao waliondoka usiku. 15Yusufu na familia yake walikaa huko Misri mpaka Herode alipofariki. Hili lilitukia ili maneno yaliyosemwa na nabii yatimie: “Nilimwita mwanangu atoke Misri.”#Hos 11:1
Herode Aua Watoto wa Kiume Katika Mji wa Bethlehemu
16Herode alipoona kuwa wenye hekima wamemfanya aonekane mjinga, alikasirika sana. Hivyo akatoa amri ya kuua watoto wote wa kiume wenye umri wa miaka miwili au chini ya miaka hiyo katika mji wa Bethlehemu na vitongoji vyake. Herode alifahamu kutoka kwa wenye hekima kwamba walikuwa wameiona nyota miaka miwili kabla. 17Hili likatimiza yale yaliyosemwa na Mungu kupitia nabii Yeremia aliposema:
18“Sauti imesikika Rama,
sauti ya kilio na huzuni kuu.
Raheli akiwalilia watoto wake,
na amekataa kufarijiwa
kwa sababu watoto wake hawapo tena.”#Yer 31:15
Yusufu na Familia Yake Warudi Kutoka Misri
19Wakati Yusufu na familia yake wakiwa Misri, Herode alifariki. Malaika wa Bwana akamjia Yusufu katika ndoto 20na akamwambia, “Damka! Mchukue mtoto na mama yake urudi Israeli, kwani waliojaribu kumwua mtoto wamekwisha kufa.”
21Hivyo Yusufu alidamka na kumchukua mtoto Yesu na mama yake na kurudi Israeli. 22Lakini Yusufu aliposikia kuwa Arkelao alikuwa mfalme wa Yuda baada ya baba yake kufa, aliogopa kwenda huko. Lakini baada ya kuonywa na Mungu katika ndoto, Yusufu aliondoka pamoja na familia yake akaenda sehemu za Galilaya. 23Alikwenda katika mji wa Nazareti na kukaa huko. Hii ilitokea ili kutimiza maneno yale yaliyosemwa na manabii. Mungu alisema Masihi angeitwa Mnazareti.#2:23 Mnazareti Mtu anayetoka katika mji wa Nazareti. Jina hili linafanana na neno la Kiebrania linalomaanisha “tawi”. Hivyo inawezekana Mathayo anamaanisha ahadi ya “tawi” la ukoo wa Daudi. Tazama Isa 11:1; Yer 23:5; 33:15; Zek 3:8; 6:12.
Valgt i Øjeblikket:
Mathayo 2: TKU
Markering
Del
Kopiér
Vil du have dine markeringer gemt på tværs af alle dine enheder? Tilmeld dig eller log ind
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International