Yohana 4
4
Yesu Azungumza na Mwanamke Msamaria
1Yesu akatambua ya kwamba Mafarisayo wamesikia habari kuwa alikuwa anapata wafuasi wengi kuliko Yohana na kuwabatiza. 2(Lakini kwa hakika, Yesu mwenyewe hakumbatiza mtu yeyote huko; bali wafuasi wake ndiyo waliowabatiza watu kwa niaba yake.) 3Hivyo akaondoka Uyahudi na kurudi Galilaya.
4Barabara ya kuelekea Galilaya ilimpitisha Yesu katikati ya nchi ya Samaria. 5Akiwa Samaria Yesu akafika katika mji wa Sikari, ulio karibu na shamba ambalo Yakobo alimpa mwanawe Yusufu. 6Mahali hapo ndipo kilikuwapo kisima cha Yakobo. Kutokana na safari yake kuwa ndefu Yesu alichoka, hivyo akakaa chini kando ya kisima. Nayo ilikuwa saa sita adhuhuri. 7Baadaye mwanamke Msamaria akaja kisimani hapo kuchota maji, na Yesu akamwambia, “Tafadhali nipe maji ninywe.” 8Hili lilitokea wakati wafuasi wake walipokuwa mjini kununua chakula.
9Mwanamke yule akajibu, “Nimeshangazwa wewe kuniomba maji unywe! Wewe ni Myahudi nami ni mwanamke Msamaria!” (Wayahudi hawana uhusiano na Wasamaria.#4:9 Wayahudi … Wasamaria Au “Wayahudi hawatumii vitu ambavyo Wasamaria wametumia.”)
10Yesu akajibu, “Hujui kile Mungu anachoweza kukukirimu. Na hunijui mimi ni nani, niliyekuomba maji ninywe. Kama ungejua, nawe ungekuwa umeniomba tayari, nami ningekupa maji yaletayo uzima.”
11Mwanamke akasema, “Bwana, utayapata wapi maji yaliyo hai? Kisima hiki kina chake ni kirefu sana, nawe huna kitu cha kuchotea. 12Je! wewe ni mkuu kumzidi baba yetu Yakobo? Yeye ndiye aliyetupa kisima hiki. Yeye alikunywa kutoka kisima hiki, na wanawe, na wanyama wake wote.”
13Yesu akajibu, “Kila anayekunywa maji haya ataona kiu tena. 14Bali yeyote anayekunywa maji ninayompa mimi hatapata kiu tena. Maji ninayowapa watu yatakuwa kama chemichemi inayobubujika ndani yao. Hayo yatawaletea uzima wa milele.”
15Mwanamke akamwambia Yesu, “Bwana, nipe maji hayo. Kisha sitapata kiu na sitapaswa kuja tena hapa kuchota maji.”
16Yesu akamwambia, “Nenda kamwite mumeo kisha urudi naye hapa.”
17Mwanamke akajibu, “Lakini mimi sina mume.”
Yesu akamwambia, “Uko sahihi kusema kuwa huna mume. 18Hiyo ni kwa sababu, hata kama umekuwa na waume watano, mwanaume unayeishi naye sasa sio mume wako. Huo ndiyo ukweli wenyewe.”
19Yule mwanamke akasema, “Bwana, naona ya kuwa wewe ni nabii. 20Baba zetu waliabudu katika mlima huu. Lakini ninyi Wayahudi mnasema kuwa Yerusalemu ndipo mahali ambapo watu wanapaswa kuabudia.”
21Yesu akasema, “Mwanamke! Niamini mimi, wakati unakuja ambapo hamtakwenda Yerusalemu wala kuja kwenye mlima huu kumwabudu Baba. 22Ninyi Wasamaria hamwelewi mambo mengi kuhusu yule mnayemwabudu. Sisi Wayahudi tunamfahamu vizuri tunayemwabudu, kwa maana njia yake ya kuuokoa ulimwengu imepatikana kupitia Wayahudi. 23Lakini wakati unakuja wenye nia halisi ya kuabudu watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa hakika, wakati huo sasa umekwishafika. Na hao ndiyo watu ambao Baba anataka wamwabudu. 24Mungu ni roho. Hivyo wote wanaomwabudu wanapaswa kumwabudu katika roho na kweli.”
25Mwanamke akasema, “Naelewa kwamba Masihi anakuja.” (Ndiye anayeitwa Kristo.)
“Atakapokuja, atatufafanulia kila kitu.”
26Kisha Yesu akasema, “Mimi ninayezungumza nawe sasa, ndiye Masihi.”
27Wakati huo huo wafuasi wa Yesu wakarudi toka mjini. Nao walishangaa kwa sababu walimwona Yesu akiongea na mwanamke. Lakini hakuna aliyemwuliza yule mwanamke, “Unataka nini?” Wala Yesu, “Kwa nini unaongea naye?”
28Yule mwanamke akauacha mtungi wake wa maji na kurudi mjini. Akawaambia watu kule, 29“Mwanaume mmoja amenieleza mambo yote niliyowahi kuyafanya. Njooni mkamwone. Inawezekana yeye ndiye Masihi.” 30Hivyo wale watu wakatoka mjini wakaenda kumwona Yesu!
31Wakati huyo mwanamke akiwa mjini, wafuasi wa Yesu wakamsihi Bwana wao wakamwambia, “Mwalimu, ule chakula chochote.”
32Lakini Yesu akawajibu, “Mimi ninacho chakula ambacho ninyi hamkijui.”
33Hapo wafuasi wake wakaulizana, “Kwani kuna mtu yeyote hapa aliyemletea chakula mapema?”
34Yesu akasema, “Chakula changu ni kuimaliza kazi ile ambayo aliyenituma amenipa niifanye. 35Mnapopanda mimea, huwa mnasema, ‘Bado miezi minne ya kusubiri kabla ya kuvuna mazao.’ Lakini mimi ninawaambia, yafumbueni macho yenu na kuyaangalia mashamba. Sasa yako tayari kuvunwa. 36Hata sasa, watu wanaovuna mazao wanalipwa. Wanawaleta ndani wale watakaoupata uzima wa milele. Ili kwamba watu wanaopanda waweze kufurahi wakati huu pamoja na wale wanaovuna. 37Ni kweli tunaposema, ‘Mtu mmoja hupanda, lakini mwingine huvuna mazao.’ 38Mimi niliwatuma kukusanya mazao ambayo ninyi hamkuyahangaikia. Wengine waliyahangaikia, nanyi mnapata faida kutokana na juhudi na kazi yao.”
39Wasamaria wengi katika mji huo wakamwamini Yesu. Wakaamini kutokana na yale ambayo walisikia yule mwanamke akiwaambia juu ya Yesu. Aliwaambia, “Yeye amenieleza mambo yote niliyowahi kuyafanya.” 40Wasamaria wakaenda kwa Yesu. Wakamsihi akae pamoja nao. Naye akakaa nao kwa siku mbili. 41Watu wengi zaidi wakamwamini Yesu kutokana na mambo aliyoyasema.
42Watu hao wakamwambia mwanamke, “Mwanzoni tulimwamini Yesu kutokana na jinsi ulivyotueleza. Lakini sasa tunaamini kwa sababu tumemsikia sisi wenyewe. Sasa tunajua kwamba hakika Yeye ndiye atakayeuokoa ulimwengu.”
Yesu Amponya Mwana wa Afisa
(Mt 8:5-13; Lk 7:1-10)
43Siku mbili baadaye Yesu akaondoka na kwenda Galilaya. 44(Yesu alikwishasema mwanzoni kwamba nabii huwa haheshimiwi katika nchi yake.) 45Alipofika Galilaya, watu wa pale walimkaribisha. Hao walikuwepo kwenye sikukuu ya Pasaka kule Yerusalemu na waliona kila kitu alichofanya huko.
46Naye Yesu akaenda tena kutembelea Kana huko Galilaya. Kana ni mahali alikoyabadili maji kuwa divai. Mmoja wa maafisa muhimu wa mfalme alikuwa anaishi katika mji wa Kapernaumu. Mwanawe afisa huyu alikuwa mgonjwa. 47Afisa huyo akasikia kwamba Yesu alikuwa amekuja kutoka Uyahudi na sasa yuko Galilaya. Hivyo akamwendea Yesu na kumsihi aende Kapernaumu kumponya mwanawe, aliyekuwa mahututi sana. 48Yesu akamwambia, “Ninyi watu ni lazima muone ishara zenye miujiza na maajabu kabla ya kuniamini.”
49Afisa wa mfalme akasema, “Bwana, uje kabla mwanangu mdogo hajafa.”
50Yesu akajibu, “Nenda, mwanao ataishi.”
Mtu huyo akayaamini maneno Yesu aliyomwambia na akaenda nyumbani. 51Akiwa njiani kwenda nyumbani watumishi wake wakaja na kukutana naye. Wakasema, “Mwanao ni mzima.”
52Mtu huyo akauliza, “Ni wakati gani mwanangu alipoanza kupata nafuu?”
Wakajibu, “Ilikuwa jana saa saba mchana homa ilipomwacha.”
53Baba yake akatambua kuwa saa saba kamili ulikuwa ndiyo ule wakati aliposema, “Mwanao ataishi.” Hivyo afisa huyo na kila mmoja katika nyumba yake wakamwamini Yesu.
54Huo ulikuwa muujiza wa pili ambao Yesu aliufanya baada ya kufika kutoka Uyahudi na Galilaya.
Valgt i Øjeblikket:
Yohana 4: TKU
Markering
Del
Kopiér
Vil du have dine markeringer gemt på tværs af alle dine enheder? Tilmeld dig eller log ind
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International