Logo YouVersion
Eicon Chwilio

Mwanzo 7

7
1Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Nuhu, “Ingia katika safina, wewe na jamaa yako yote, kwa sababu katika kizazi hiki nimeona ya kuwa wewe ni mwenye haki. 2Chukua wanyama saba walio safi wa kila aina, wa kiume na wa kike; na wanyama wawili wawili wa kila aina walio najisi, wa kiume na wa kike. 3Pia uchukue ndege saba walio safi wa kila aina, wa kiume na wa kike, ili kuhifadhi aina zao mbalimbali katika dunia yote. 4Siku saba kuanzia sasa nitaleta mvua juu ya dunia kwa siku arobaini, usiku na mchana; nami nitafutilia mbali kutoka uso wa dunia kila kiumbe hai nilichokiumba.”
5Nuhu akafanya yote Mwenyezi Mungu aliyomwamuru.
6Nuhu alikuwa na umri wa miaka mia sita gharika ilipokuja juu ya dunia. 7Nuhu na mkewe, na wanawe na wake zao, wakaingia katika safina ili waepuke ile gharika. 8Jozi ya wanyama walio safi na walio najisi, ndege na viumbe vinavyotambaa ardhini, 9wa kiume na wa kike, walikuja kwa Nuhu, wakaingia katika safina kama Mungu alivyomwamuru Nuhu. 10Baada ya siku saba, maji ya gharika yakaja juu ya dunia.
11Katika siku ya kumi na saba ya mwezi wa pili, mwaka wa mia sita wa maisha ya Nuhu, siku hiyo chemchemi zote za vilindi zilibubujika kwa nguvu, na malango ya mafuriko ya mbinguni yakafunguliwa. 12Mvua ikanyesha juu ya dunia siku arobaini usiku na mchana.
13Siku hiyo Nuhu na mkewe, na wanawe Shemu, Hamu na Yafethi pamoja na wake zao, wakaingia katika ile safina. 14Nao walikuwa pamoja na kila mnyama pori kufuatana na aina yake, wanyama wote wafugwao kufuatana na aina zao, kila kiumbe kinachotambaa juu ya ardhi kwa aina yake, na kila ndege kufuatana na aina yake, naam kila kiumbe chenye mabawa. 15Viumbe vyote vyenye pumzi ya uhai vikaja kwa Nuhu viwili viwili, vikaingia katika safina. 16Wanyama walioingia katika safina walikuwa wa kiume na wa kike, wa kila kiumbe chenye uhai kama Mungu alivyomwamuru Nuhu; ndipo Mwenyezi Mungu akamfungia ndani.
17Kwa siku arobaini mafuriko yaliendelea kujaa duniani; maji yalivyozidi kuongezeka, yaliinua safina juu sana kutoka uso wa dunia. 18Maji yakajaa na kuongezeka sana juu ya dunia, na safina ikaelea juu ya maji. 19Maji yakazidi kujaa juu ya dunia, yakaifunika milima yote mirefu chini ya mbingu yote. 20Maji yakaendelea kujaa, yakaifunika milima kwa kina cha zaidi ya dhiraa kumi na tano#7:20 Dhiraa 15 ni sawa na mita 7.. 21Kila kiumbe hai kinachotambaa juu ya dunia kikaangamia: ndege, mifugo, wanyama pori, viumbe vyote juu ya nchi, na wanadamu wote. 22Kila kiumbe juu ya nchi kavu chenye pumzi ya uhai kikafa. 23Kila kitu chenye uhai juu ya uso wa nchi kilifutiliwa mbali; watu, wanyama pori, viumbe vinavyotambaa ardhini, na ndege warukao angani wakafutiliwa mbali toka duniani. Waliobaki ni Nuhu peke yake na wale waliokuwa pamoja naye ndani ya safina.
24Maji yakaifunika dunia kwa siku mia moja na hamsini.

Dewis Presennol:

Mwanzo 7: NENO

Uwcholeuo

Rhanna

Copi

None

Eisiau i'th uchafbwyntiau gael eu cadw ar draws dy holl ddyfeisiau? Cofrestra neu mewngofnoda